Kaimu Mkurugenzi Udhibiti Ubora wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Bi. Mary Meela akiwaeleza waandishi wa Habari (hawapo pichani) kuhusu Mikakati wanayoweka ya kuendelea kudhibiti ubora wa bidhaa nchini ikiwemo kuimarisha ukaguzi kwenye vituo vya mipakani mwa nchi,Kulia ni Afisa Habari Wa Idara ya Habari Bw. Frank Mvungi. |
Afisa Uhusiano wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Bi. Roida Andusamile akitoa wito kwa waandishi wa Habari (hawapo pichani) kuendelea kuelemisha umma kuhusu madhara ya matumizi ya nguo za mdani za mtumba. Kulia ni Kaimu Mkurugenzi Udhibiti Ubora wa Shirika hilo Bi. Mary Meela.Picha na Hassan Silayo
---
Na Frank Mvungi
Shirika la viwango Tanzania (TBS) linatarajia kuajiri watumishi 200 katika harakati za kuimarisha utendaji wa shirika hilo.
Hayo yamesemwa na Kaimu Mkurugenzi wa udhibiti ubora wa shirika hilo Bi Mary Meela wakati wa mkutano na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam.
Akifafanua Meela amesema watumishi watakaoajiriwa watasaidia kuimarisha utendaji kazi wa shirika hilo hasa katika kufanya ukaguzi na kuhakisha tatizo la bidhaa hafifu linapungua au kuondolewa kabisa.
Aidha Bi. Meela alisema kuwa Shirika limeweza kuweka wakaguzi kwenye vituo 5 ambavyo ni Sirari, Namanga, Taveta, Horohoro, Bandari za Tanga na Dar es salaam na kuweka wakaguzi kwenye vituo vya bandari kavu (ICD).
Akizungumzia kuhusu utumiaji wa nguo za ndani za Mtumba Bi. Meela amewataka watanzania kuwa mstari wa mbele kupinga matumizi ya nguo hizo kwani zina madhara kiafya kwa watumiaji na wataendelea kufanya ukaguzi wa nguo hizo na kuziteketeza pindi zinapopatikana.
Shirika la viwango lilianzishwa kwa Sheria ya Bunge Na. 3 ya mwaka 1975, kasha kuundwa upya mwaka 2009 sheria ambayo imelipa shirika uwezo mkubwa zaidi wa utayarishaji viwango na kusimamia utekelezaji wake.
0 comments:
Post a Comment