Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Wanawake Tanzania (TWB), Bi. Margareth Chacha akifafanua jambo katika mkutano mkuu wa wanawake Idara ya Takwimu jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki. Kulia kwake ni Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Takwimu, Dkt. Albina Chuwa, Kamishina wa Sensa ya Watu na Makazi, Bi. Amina Said na Mwenyekiti wa Chama cha TUGHE Mkoa wa Dar es Salaam, Bi.Salma Omari.
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Wanawake wametakiwa kujiunga katika vikundi (SACCOS) ili waweze kunufaika na huduma za mikopo yenye riba nafuu kutoka Benki ya Wanawake ya Tanzania (TWB) ikiwa ni juhudi za kujikwamua kimaendeleo.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Wanawake Tanzania, Margareth Chacha jana wakati wa mkutano Mkuu wa Wanawake Idara ya Takwimu uliofanyika jijini Dar es salaam na benki hiyo kutambulisha huduma na bidhaa zake.
"Wakati umefika kwa wanawake kuchangamkia fursa hii kwani Benki ya Wanawake inatoa sio tu mikopo yenye riba nafuu bali pia chaguo la muda wa marejesho kulingana na mkopaji", alisema.
Alisema kuwa inatoa mikopo yenye riba nafuu zaidi kuliko benki nyingine hivyo kuwashauri wanawake kujiuna katika SACCOS ambazo zitawahakikishia kuwa dhamana na amana ya mikopo hivyo kujiendeleza kimaendeleo bila vikwazo vyovyote. "Kitu cha msingi ni kuwa na wanakikundi waamimifu na daftari la akiba zinazokaguliwa..,"alisema.
Akifafanua zaidi alisema kuwa benki hiyo ina huduma mbalimbali ikiwemo mikopo kwa walaji inayotegemea mshahara tofauti na mikopo ya biashara.
Alisisitiza kwa taasisi nyingine za umma na binafsi kuwaalika katika sehemu za kazi ili waweze kutoa elimu kuhusu benki hiyo kwa wanawake waweze kufahamu na kutumia fursa mbalimbali zinazopatikana kupitia benki hiyo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Wanawake TUGHE ofisi ya Taifa ya Takwimu Bi Slyvia Meku alisema kuwa wameamua kuwaalika wawakilishi kutoka benki hiyo ili kujua bidhaa na huduma mbalimbali zinazopatikana ukizingatia kuwa wanawake ndio walengwa wakuu. "Tumeamua kuwaalika ili kujua faida na fursa zinazopatikana kupitia benki hiyo",alisema.
Alisema kuwa Benki ya wanawake imekuwa mdau mkubwa katika juhudi za kumwendeleza mwanamke kwa kutoa elimu hasa kwa wanawake katika kujiendeleza kiuchumi kupitia mikopo yenye riba nafuu hivyo kuchochea kasi ya maendeleo hapa nchini.
0 comments:
Post a Comment