HATIMAYE 'ndoa' ya Rio Ferdinand na Manchester United imevunjika rasmi baada ya beki huyo mkongwe kutaarifiwa kuwa klabu haitampa mkataba mpya.
Imefahamika kuwa Mtendaji wa Manchester United Ed Woodward aliwasilisha habari hizo kwa Ferdinand, 35 kwenye vyumba vya kubadilishia nguo Jumapili iliyopita kwenye mchezo wao wa mwisho wa ligi kuu dhidi ya Southamton.
Watu kadhaa walikuwepo wakati Rio akijuzwa juu ya hatma yake na wakashangaa ni vipi Woodward aliamua kutumia njia hiyo isiyo na adabu kwa beki huyo aliyeitumikia United kwa miaka 12.
Beki huyo wa zamani wa timu ya taifa ya England, aliwaambia wachezaji wenzake kuwa mchezo huo ulioisha kwa sare ya 1-1 kwenye uwanja wa St Mary ndio ulikuwa wa mwisho kwake na hivyo kuwataka wamsainie mpira kwaajili ya kumbu kumbu.
Katika taarifa aliyotoa kupitia mtandao wake rasmi Ferdinand alisema: "Katika miezi michache iliyopita, nimefikiri kwa kina na kwa muda mrefu juu ya hatma yangu na baada ya kuichezea kwa miaka 12, kwa klabu niliyoichukulia kama timu bora duniani, nimeamua kuwa ni muda sahihi wa kuondoka.
"Nilijiunga na Machester United ili kushinda mataji, lakini kamwe katika njozi zangu sikutegemea kuwa na mafanikio makubwa kiasi hiki katika muda wangu hapa. Kumekuwa na mambo mengi ya kuvutia, kucheza kando ya wachezaji mashuhuri ambao wakatokea kuwa marafiki zangu wakubwa, kushinda taji langu la kwanza la Ligi kuu pamoja usiku wa kukumbukwa pale Moscow tulipotwaa kombe la Ligi ya Mabingwa ni kumbukumbu zitakazodumu milele.
"Mazingira hayakuniruhusu kusema kwaheri kwa njia ambayo ningependa lakini nachukua fursa hii kuwashukuru wachezaji wenzangu, wafanyakazi, klabu na mashabiki kwa miaka 12 ambayo kamwe sitasahau. Kushinda mataji ilikuwa ni njozi yangu ya utotoni iliyogeuka kuwa kweli katika klabu hii kubwa.
"Najisikia mwenye afya njema na nguvu, nipo tayari kwa changamoto mpya na kuangalia yajayo siku za usoni."
Rio Ferdinand alisajiliwa na United chini ya kocha Sir Alex Feruguson kwa Julai 2, 2002 kutoka Leeds United kwa kitika cha pauni milioni 29.1 na kuwa mmoja wa mabeki ghali duniania.
0 comments:
Post a Comment