Friday, June 29, 2012

SAKATA LA MAPESA YALIYOFICHWA USWISI


  • Ni kati ya watoroshaji sita wakuu
  • Kikao cha Baraza ka Mawaziri kujadili
  • Membe asema mabilioni hayo yatarudi tu

VIONGOZI wawili wastaafu waliopata kuitumikia nchi katika nafasi nyeti za dola ni miongoni mwa vigogo sita walioficha dola za Kimarekani takriban milioni 196.8 (Sh. Bilioni 315) katika mabenki ya Uswisi, RAIA MWEMA limeambiwa.

Habari za uhakika ambazo gazeti hili limezipata zinasema kwamba vigogo hao walifanikiwa kukusanya mabilioni hayo kwa kuwashirikisha baadhi ya wafanyabiashara kupitia mfumo wa ununuzi serikalini (public procurement) kwa nyakati tofauti.

Wakati hayo yakifahamika, Waziri wa Fedha, Dk. William Mgimwa, anatarajiwa kuwasilisha taarifa rasmi kuhusu uporaji huo kwenye Baraza la Mawaziri.

Kwa mujibu wa vyanzo vyetu vya habari, baadhi ya wafanyabiashara walioficha pesa hizo kwenye mabenki ya Uswisi si wenye majina makubwa katika tasnia ya biashara hapa nchini, lakini ni wenye ufahamu wa kutosha katika mifumo ya kibiashara katika nchi mbalimbali duniani.

 "Taarifa za awali zinawahusisha viongozi sita. Serikali ya Uswisi iko tayari kutaja majina ya  wahusika na pia wako tayari kutupatia mchanganuo wa kiasi cha fedha na taarifa nyingine muhimu. Rais ataitisha kikao cha Baraza la Mawaziri kujadili suala hili wakati wowote. Kwa sasa kinachoendelea ni ukusanyaji wa taarifa muhimu",  kilieleza chanzo chetu cha habari serikalini.

Mwandishi wetu alizungumza na Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU), Dk. Edward Hosea, ambaye pia amekwisha kupata kuzungumzia suala hilo na vyombo mbalimbali vya habari nchini.

Katika maelezo yake kwa mwandishi wetu, Dk. Hosea alisema: "Tumekwisha kuwaandikia Uswisi na tunatarajia taarifa kamili kutoka kwao. Tumewaandikia kuhusu maeneo ambayo tungependa kupata taarifa kuhusu suala hili, tunasubiri majibu yao. Tunaamini tutapata ushirikiano mzuri kwa sababu kwa sasa Uswisi imefanya mabadiliko ya sheria zake; tutafanikiwa."

Lakini kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, alipoulizwa kuhusu nafasi yake kama waziri katika kusaka taarifa za kadhia hii alijibu: "Ukizungumzia nafasi za mawaziri kuhusu suala hili...ni sahihi kusema kwamba kwa sasa lipo mikononi mwa Waziri wa Fedha. Sisi Wizara ya Mambo ya Nje tunazingatia taarifa zake (Waziri wa Fedha) ili kujua kwa namna gani tunashiriki."

Membe aliongeza kusema: "Jambo moja la uhakika ni kwamba Serikali ipo tayari na imara kushughulikia suala hili. Kama kuna fedha zitarudishwa tu nchini. Jambo la msingi hapa ni kwamba sheria zote husika zitazingatiwa.

Kama Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa itaingilia suala hilo, itakuwa ni mara ya pili katika utawala wa Rais Jakaya Kikwete kufanya hivyo. Tayari Waziri Membe alikuwa akiratibu namna ya urejeshaji wa fedha zilizozidi wakati wa ununuzi wa kitapeli wa rada ya kijeshi kutoka kampuni ya zana za kijeshi ya BAE-Systems ya Uingereza.

Fedha hizo paundi za Uingereza milioni 29.5 (sawa na Sh bilioni 72.3 za Tanzania) zimekwisha kurejeshwa nchini na tayari zimepangiwa matumizi. Katika matumizi hayo, Sh. bilioni 54.2, sawa na asilimia 75) zimepangwa kutumika kununua vitabu vya kiada kwa shule za msingi na Sh. bilioni 18.1 zitatumika kutengeneza madawati kwa ajili ya shule za msingi.

Pia katika sakata hilo la rada ilibainika kuwa aliyepata kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Andrew Chenge, alihifadhi takriban Sh. bilioni moja katika visiwa vya Jersey nchini Uingereza katika moja ya benki katika kisiwa hicho.

Suala hili pia lilijitokeza jana, Jumanne, bungeni. Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto alimwomba Waziri Mkuu kuagiza mamlaka husika za kiserikali kufuatilia suala hilo na kutoa taarifa kwa umma.

Zitto alisema hizo ni taarifa za kushtusha na kwamba hali hiyo inatia shaka zaidi kwa sababu inajitokeza katika wakati ambao nchi inakwenda kuvuna kiwango kikubwa cha gesi itakayoingiza fedha nyingi za kigeni na akasisitiza mianya ya utoroshaji fedha izibwe.

Taarifa za kuporwa, kutoroshwa na kuhifadhiwa kwa takriban Sh bilioni 315 (dola za Marekani milioni 196.87) zimeanza kuandikwa na vyombo vya habari nchini kwa takriban wiki moja sasa.

Taarifa kuhusu mabilioni hayo ziliwekwa hadharani kwenye ripoti ya Benki Kuu ya Uswisi, zikieleza kuwa si tu Tanzania, bali zipo nchi nyingine 10 ambazo watu mashuhuri katika nchi hizo wamehifadhi mabilioni ya fedha.

Kwa mujibu wa taarifa hizo za Benki Kuu ya Uswisi, katika nchi za Afrika Mashariki Kenya ndio inayoongoza. Takwimu zinaonyesha kuwa kutoka Kenya, benki za Uswisi zimehifadhi dola milioni 857.

Takwimu hizo za Uswisi zinaonyesha kuwa kutoka Uganda zimefichwa dola milioni 154, Misri dola milioni 798, Afrika Kusini dola milioni 795 na Rwanda dola milioni 29, Somalia dola milioni moja na Sudan dola milioni 179.

Hivi karibuni Serikali ya Uswisi ilizielekeza benki zake mbalimbali nchini humo kufichua majina ya vigogo wa nchi mbalimbali walioweka kwa siri mabilioni ya fedha katika benki hizo.

Source; Raia mwema


0 comments:

Post a Comment