Wednesday, May 21, 2014

SPIKA KIFICHO AKEMEA WAWAKILISHI WANAOZUNGUMZIA MASUALA YA BUNGE MAALUM LA KATIKA NDANI YA BARAZA LA WAWAKILISHI

 
 
 

kificho-feb25-2014

Na Miza Kona – Maelezo Zanzibar
Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Pandu Ameir Kificho amekemea tabia ya baadhi ya wajumbe  kutofuata muongozo na kanuni za Baraza hilo kwa kuzungumzia mambo ya siasa. Amewataka wajumbe  kujadili mambo ya maendeleo ya nchi na kufanya kazi waliyotumwa na wananchi na kuacha  kujadili mambo ya siasa yanayoweza kupelekea ubaguzi nchini. Spika  Kificho ametoa maelezo hayo  katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi  Chukwani  kufuatia baadhi ya wajumbe  kuzungumzia masuala  ya Muungano na Bunge la Katiba wakati kikao hicho kilipokuwa katika kipindi cha  masuala na majibu.Amesema kuzungumzia mambo ya Bunge la Katiba na Muungano wakati huu sio mahala pake kwani inaweza kuleta ubaguzi na kutoweza kufikia lengo la kikao hicho kinachoendelea kujadili mambo ya maendeleo."Sipendi kusikia wazanzibari, sipendi kusikia watanzania wanafika pahala kubaguana nasema haya kwa manufaa ya watanzania wote," alikemea Spika Kificho.

Amefahamisha kuwa kufanya hivyo  ni kutowatendea haki wananchi na kuliweka pabaya taifa kwani wao ni viongozi   wanaotegemewa na jamii  hivyo ni vyema wakajenga heshima ili kutekeleza vyema majukumu yao.
Aidha Spika Kificho amekataza masuala ya Bunge la Katiba na Muungano yasijadiliwe wakati kikao hicho kinaendelea na mijadala ya Bajeti ya Serikali  kwa mwaka 2014/2015. 
Wakichangia kuhusu  Mpango wa Maendeleo ya Bajeti ya mwaka wa fedha 2014/2015 mwakilishi wa Jimbo la Konde Suleiman Hemed Khamis amesema miradi ya wananchi ni muhimu sana lakini miradi hiyo huwa haimaliziki kutekelezwa na kufikia lengo lililokusudiwa.
"Miradi huwa haimaliziki kutekelezwa kwa jamii kwani miradi hiyo inashindwa kuwezeshwa na serikali na kutoweza kufika lengo lililokusudiwa mfano mradi wa MECO wa barabara ya Wete Gando umeshindwa kumalizika kutokana na kutolipwa pesa na bank kuwawezeshwa", alifahamisha Mwakilishi huyo.
Mwakilishi huyo amesema kuwa ili uchumi  uweze kukuwa zaidi  nchini,  Serikali na jamii zinapaswa kudhibiti vitendo vya uhalifu kwa watalii kwa kuondosha vitendo vya wizi, uvamizi pamoja na wanasiasa kuacha kuzungumzia mambo ya ugaidi.
Nae Mwakilishi wa Jimbo la Kiwani Hijja Hassan Hijja amesema biashara nchini imekuwa ngumu kutokana na kuwepo kwa ushuru mkubwa unaosababisha Mamlaka ya Mapato  Tanzania  (TRA) kwa upande wa Zanzibar kushindwa kufikia malengo ya kukusanya  mapato  iliyojiwekea.
                              IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI MAELEZO ZANZIBAR

0 comments:

Post a Comment