Wednesday, August 14, 2013

Sitta: Bil 8/- zimekwenda na kampuni hewa; CAG: Sijapokea taarifa ya kuchunguza



Sitta: Bil 8/- zimekwenda na kampuni hewa; CAG: Sijapokea taarifa ya kuchunguza
MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh, amesema hajapokea taarifa rasmi ya kutakiwa kuzifanyia uchunguzi sh bilioni 8 zilizotumika wakati wa Mkutano wa Smart Partnership Dialogue uliohusisha viongozi wa Afrika.

Hivi karibuni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, akifungua mkutano wa siku tatu wa Baraza la Vijana la Katiba aliitaka ofisi ya CAG, kuchunguza kashfa ya matumizi tata ya sh bilioni 8.

Akizungumza jana wakati wa mafunzo ya wajumbe wa kamati za Bunge Bagamoyo, mkoani Pwani, Utouh alisema kuwa taarifa kuhusu pesa hizo zilitumika kwenye mkutano hivi karibuni amezisoma kupitia vyombo 
vya habari lakini ofisi yake haijapokea taarifa ya kuhitaji uchunguzi huo.

Utouh ambaye alitoa kauli hiyo kwa kifupi alisema kwa kuwa wanatarajia kufanya uchunguzi wa mwaka katika Ofisi ya Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje wanategemea kulifanyia kazi suala hilo: "Ingawa ofisi yangu haijapokea taarifa yoyote inayotaka tufanyie uchunguzi suala hilo lakini naaahidi kuwa jambo hilo tutalitazama katika ukaguzi wetu wa mwaka tunaotarajia kuufanya katika wizara hiyo," alisema Utouh.

Katika mkutano wake Sitta alidai kuwa fedha hizo zimefujwa na baadhi ya watumishi wa serikali ambao walijitengenezea kampuni bandia ambazo hazijasajiliwa: "Shilingi bilioni nane zimekwenda kutokana na kampuni hewa baada ya Rais kuwakaribisha wageni nchini hivi karibuni.... kisa Rais kapata wageni watu wametengeneza kampuni hewa za mapambo, machapisho na fedha zimeliwa. Hivi sasa uchunguzi unaendelea, lakini hatuwezi kuwa kila siku ni uchunguzi tu na wakati mwingine uchunguzi umekuwa hauna matokeo," alisema Sitta.

Alisema watumishi kama hao hawafai kwa kuwa wanatumia nafasi muhimu kwa nchi kujinufaisha wao binafsi.

Mkutano wa Smart Partnership Dialogue ulifanyika Dar es Salaam kuanzia Juni 28 hadi Julai Mosi mwaka huu. --- Betty Kangonga, Bagamoyo, TANZANIA DAIMA.



0 comments:

Post a Comment