Wednesday, August 14, 2013

RITA yafuta ada ya cheti cha usajili kwa watoto



RITA yafuta ada ya cheti cha usajili kwa watoto 
Meneja Masoko na Mawasiliano RITA, Josephat Kimaro, jana jijini Dar es Salaam akizungumzia mfumo mpya wa usajili wa vizazi vya watoto walio chini ya miaka mitano ambao utafanyika katika ofisi za watendaji kata na katika vituo vya tiba vinavyotoa huduma ya afya ya mama na mtoto amesema Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA), imefuta ada ya cheti kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano.

Amesema lengo la kubadili mfumo ni ili kuondoa changamoto zilizosababisha wananchi wengi kutosajiliwa na 
kupata vyeti nchini: "Kumekuwa na changamoto ya kupatikana taarifa za waliosajiliwa kwani katika mfumo wa awali wasajili wa wilaya wamekuwa hawaziwakilishi kwa wakati," alisema Kimaro.

Alieleza kuwa tafiti zinaonesha asilimia 23 ya Watanzania wamesajiliwa na kupata vyeti vya kuzaliwa kutokana na umbali mrefu kutoka maeneo wanayoishi hadi kwenye ofisi za wasajili wa Wilaya, ada ya cheti, taratibu za usajili zisizorafiki, sambamba na elimu ndogo kwa wananchi kuhusu umuhimu wa cheti cha kuzaliwa.

Alisema kutokana na changamoto hiyo RITA katika awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mfumo huo mpya inajumuisha mikoa mitano ya Mbeya, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Geita ambayo inategemea kukamilika Julai mwaka 2015 na katika mikoa hiyo tayari wameshaanza na mkoa wa Mbeya ambapo wanatarajia hadi kufikia Juni mwakani wawe wameshasajili watoto 230,000. --- Zawadi Chogogwe, TANZANIA DAIMA.



0 comments:

Post a Comment