Monday, October 1, 2012

WASINDIKAJI ALIZETI SINGIDA WAHIMIZWA KUSINDIKA KWA KIWANGO KINACHOKUBALIKA KIMATAIFA.




Katibu tawala mkoa wa Singida Liana Hassan akifungua mafunzo ya usindikaji bora wa mafuta ya Alizeti yaliyohudhuriwa na wasindikaji wadogo na wakaguzi wa vyakula.Kushoto ni meneja usalma wa chakula (TFDA) Raymond Wigenge.
Baadhi ya wasindikaji wadogo wa mafuta ya Alizeti na wakaguzi wa vyakula kutoka halmashauri ya wilaya ya Singida na manispaa ya Singida.
Katibu tawala mkoa wa Singida,Liana Hassan (katikati walioketi) akiwa kwenye picha ya pamoja na wasindikaji wadogo wa mafuta ya Alizeti na wakaguzi wa vyakula kutoka halmashauri ya wilaya ya Singida na manispaa ya Singida,waliohudhuria mafunzo ya siku mbili ya usindikaji wa mafuta yanayokidhi vigezo vya ndani na nje ya nchi.(Picha zote na Nathaniel Limu).
Na Nathaniel Limu.
Katibu tawala mkoa wa Singida Liana Hassan amewahimiza wasindikaji wa mafuta ya alizeti kuhakikisha wanasindika mafuta yenye viwango vinavyokubalika katika soko la ndani na nje ya nchi, ili pamoja na mambo mengine waweze kujipatia soko kwa kiurahisi.
Hassan ameyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati akifungua mafunzo ya siku mbili ya wasindikaji wadogo wa mafuta ya alizeti na wakaguzi wa vyakula kutoka halmashauri ya wilaya ya Singida na manispaa ya Singida.
Mafunzo hayo yameandaliwa na kufadhiliwa na mamlaka ya chakula na dawa Tanzania (TFDA).
Amesema pamoja na wasindikaji kuhakikisha mafuta yanakidhi vigezo vyote vya ubora, pia mafuta hayo yanapaswa kuwa  salama kwa maana ya kulinda afya ya walaji.
Kwa upande wa wakaguzi wa vyakula, amesema wakaguzi wana wajibu wa kuhakikisha kuwa sheria na kanuni zinazingatiwa wakati wote ili kumlinda mlaji wa mafuta ya alizeti.
Awali Mkurugenzi Usalma wa Chakula (TFDA) Raymond Wigenge, amewataka wasindikaji wa mafuta ya alizeti kuangalia uwezekano wa kuunganisha nguvu zao ili waweze kusindika mafuta yenye kukidhi vigezo.
Kuhusu walaji, Meneja huyo amewataka wajenge utamaduni wa kununua bidhaa ikiwemo mafuta ya alizeti zenye lebo ili waweze kujua muda wake wa kutengenezwa, muda wake wa kumalizika, wapi imetengenezwa n.k.
Amesema mteja akifahamu yote hayo basi endapo kutatokea tatizo itakuwa rahisi kufuatilia.

Related Posts:

0 comments:

Post a Comment