Wednesday, August 1, 2012

MAGUFULI AMWAGIZA MFUGALE KUKOMESHA RUSHWA KWENYE MIZANI.




Waziri wa Ujenzi Dkt.  John Magufuli (Pichani) amemwagiza mkurugenzi mkuu wa Tanroads nchini,Patrick Mfugale kuhakikisha anakomesha vitendo vya  rushwa vilivyokithiri  kwenye mizani mbalimbali hapa nchini,kunakofanywa na wafanyakazi wasio waaminifu na kusababisha uharibifu mkubwa wa barabara hapa nchini.

Dkt. Magufuli ameyasema hayo leo wakati akifungua mkutano wa siku tatu wa wadau wa bodi ya barabara nchini unaofanyika jijini Arusha.

Alisema kuwa asilimia 80 ya wafanyakazi wa mizani hapa ni nchini ni wala rushwa wakubwa hivyo kusababisha idadi kubwa ya barabara hapa nchini kuharibika vibaya kutokana na kuruhusu magari yenye ujazo mkubwa kupita.

''asilimia 80 ya wafanyakazi wa mizani ni walarushwa wakubwa nakuagiza mkurugenzi haikisha unafanya uchunguzi wa kina na ikiwezekana fukuza asilimia 90 mpaka uhakikishe rushwa inakomeshwa''alisema na kuongeza kuwa "tumekuwa tukituma watu wetu kuchunguza tuhuma hizo lakini cha ajabu nao walikuwa wakiingia kwenye mkumbo wa kupokea rushwa hii ni hatari sana ,sasa tumia mbinu nyingine mpaka vitendo hivyo vikome".

Aidha alimtaka Mkurugenzi huyo kuhakikisha anawatimua kazi mara moja wafanyakazi wasiowaadilifu bila kujali wameingizwa  na Waziri ama kigogo yoyote mwenye cheo kikubwa  hapa nchini,kwani hali hiyo  inachangia kuwepo kwa ufanisi mdogo wa utendaji kazi kwenye mizani.

Waziri  huyo alitolea mfano kuwa barabara ya Chalinze Morogoro imeharibika kwa kulalia upande wa kushoto kutokana na magari yanayotokea  Dar es salaam kuelekea Morogoro yamekuwa yakipita na uzito mkubwa  bila kuchukuliwa hatua na kufanya barabara hiyo kulalia upande mmoja.

Katika hatua nyingine waziri Magufuli amezionya halmashauri zote nchini kuacha mara moja kubadilisha matumizi ya fedha zilizotengwa kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa barabara na kuzielekeza kwenye matumizi mengine ikiwemo kulipana posho za vikao ,manunuzi ya vitafunio, matengenezo ya magari na ununuzi wa vifaa vya ofisi.

Alitolea mfano halimashauri  za Morogoro,Chato,Kigoma,Biharamulo,Misenyi,Dodoma,,Kishapu,Mafya,Mwanga,Geita ,Musoma,Kibondo ,Njombe Bariadi na Tarime kuwa zimetumia vibaya fedha za mradi wa barabara kwa kuelekza kwenye matumizi mengine.

Alitaka bodi ya mfuko wa barabara nchini kuhakikisha inasimamia ipasavyo matumizi ya fedha za barabara ,kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwa wakandarasi wanaopewa tenda za ujenzi wa barabara,miradi ya bara bara kutokamilika kwa wakati.

Hata hivyo alisema kuwa jumla ya barabara za lami hapa nchini zenye urefu wa kilometa 11,154 zimetengenezwa  na kwamba alisema hadi kufikia mwaka 2015 jumla ya barabara zenye urefu wa kilometa 17,500 zitakuwa zimetengenezwa  na kufanya nchi ya Tanzania iwe miongozi mwa nchi 5 za Afrika  zenye mtandao wa barabara za lami.

Mahmoud Ahmad wa MO BLOG, Arusha.

0 comments:

Post a Comment