Thursday, December 11, 2014

Majibu ya Hoja za wadau kwa mwezi Oktoba na Novemba, 2014.



Majibu ya Hoja za wadau kwa mwezi Oktoba na Novemba, 2014.
Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, inapenda kuwashukuru wadau wote waliouliza maswali pamoja na kutuandikia maoni mbalimbali kwa njia ya simu na barua pepe kwa kipindi chote cha miezi miwili. 
Pia tunapenda kuwajulisha wale wote waliotuandikia maoni na maswali kwa kutumia baruapepe zao kuwa wazifungue kwani tulijibu kila swali na kuwatumia katika anwani husika, na baadae kuyaunganisha maswali na maoni yanayofanana na kuyatolea majibu ya jumla kwa faida ya wasomaji wetu wengine ili kuendelea kuelimishana kuhusu masuala yanayohusu mchakato wa ajira Serikalini. 
Aidha, tunapenda kukaribisha maoni na ushauri zaidi wenye kujenga chombo hiki na kuboresha huduma inayotolewa na chombo hiki ili kuhakikisha Serikali inaendelea kuajiri Watumishi wa Umma ambao wana sifa na vigezo stahili vya kuajiriwa Serikalini na walio tayari kuwatumikia wananchi.
Swali la 1.
Habari,  naomba kufahamu, nyie tume mnatoa nafasi za udereva mara kwa mara.je unapotuma barua mara moja inatosha au inabidi utume kila unapoona nafasi imetangazwa? Kwa sababu nimeshatuma barua zaidi ya 7, lakini kila ninapoingia kwenye mtandao naona nafasi za udereva barua zitumwe kupitia tume ya utumishi.sasa naomba msaada wako, kazi njema.
Jibu.
Tunashukuru kwa swali lako la kutaka ufafanuzi, Ni kweli hivi karibuni Sekretarieti ya Ajira imekuwa ikitangaza nafasi mbalimbali za kazi mara kwa mara zikiwemo za udereva. Tunapenda kukufahamisha kuwa kila unapoona tangazo la kazi linatokana na mahitaji ya waajiri ni tofauti, hivyo haikuzuii kuomba mara nyingi uwezavyo lakini pia tunakushauri ukishatuma maombi yako uwe unafuatilia mara kwa mara kwenye tovuti yetu ya www.ajira.go.tz  ili kufahamu wakati waombaji wanapoitwa kwenye usaili kwa kuwa tayari umeshatuma maombi mengi. Jambo la msingi wakati wa kutuma maombi yako ya kazi hakikisha unaweka viambatanisho vyote vinavyohitajika kwa mujibu wa tangazo la kazi ili uweze kukidhi mahitaji ya tangazo na kazi husika.
Swali la 2.
Naitwa IGNATUS J KAJORO nimeshafanya interview mara 4 za Supplies Assistant na Assistant Procurement and logistics officer baada ya hapo nikapigiwa simu kwa namba ya ttcl +255222153517 lakini sikuweza kupokea simu badae nilifuatilia nikaambiwa nilikuwa naitwa kazini. Pia nikaambiwa nitapigiwa simu pindi nafasi zikipatikana lakini mpaka sasa sijapigiwa simu tena na niko kwenye kazidata. Naomba kujua ni lini nitaitwa kuja kuchukua barua ya kuitwa kazi. wako mtiifu, asante mungu awabariki kazi njema.
Jibu.
Nakupa pole kwa jambo hilo inawezekana ni kweli ulipigiwa simu mara kadhaa lakini hukuweza kupokea simu au hukupatikana hewani kama ulivyoeleza na kupelekea nafasi yako kupangiwa mtu mwingine, Aidha kwa kuwa upo kwemye kanzidata tunaendelea kukushauri kuvuta subira na endapo itapatikana nafasi nyingene ya kazi  utajulishwa kama ulivyofahamishwa hapo awali.  Pamoja na kuvuta subira ni vizuri ukafahamu pia kuwa matumizi ya kanzidata yana muda maalum na pale muda unapokwisha utaratibu huanza upya. Aidha tunakushauri kuhakikisha simu yako inakuwa hewani muda wote ili isije ikatokea ukakosa fursa nyingine.
Swali la 3.
habari! jina langu ni Farida Hamis, nimechaguliwa kujiunga na TBC lakini sijatumiwa barua mpaka sasa, je naweza kuripoti bila barua?
Jibu
Asante kwa swali lako,Jibu ni kwamba kama ulifaulu usaili na kupangiwa kituo cha kazi barua yako yako itakuwa imeshatumwa kwenye anuani uliyotumia wakati wa maombi ya kazi, Aidha kama hadi sasa hujapata barua hiyo unapaswa  kufika Ofisi za Sekretarieti ya ajira kwa ajili ya msaada zaidi.
Swali la 4.
Habari za majukumu, poleni na ubize wa kazi,naomba kufahamishwa ni lini watu wa supplies assistant kule gpsa wataitwa kazini..nategemea sana majibu yenu.
asanteni
Jibu.
Asante kwa swali lako waombaji kazi wa nafasi mbalimbali waliofanya usaili kuanzia tarehe 21Oktoba hadi tarehe 05 Novemba, 2014 wakiwemo watu wa Supplies Assistant  wa GPSA tangazo la kupangiwa/kuitwa kazini lilishatolewa tangu tarehe 20 Novemba, 2014 hivyo tunakushauri kuangalia tangazo hilo katika tovuti ya Sekretarieti ya Ajira www.ajira.go.tz.
Swali la 5.
Naomba msaada kwa hiyo chuo cha ilemi polytechnic college ndo hataomba tena ajira.na je tufanyeje hapa sasa kuhusu mstakabari wa maisha?
Jibu.
Kuhusu chuo cha Ilemi Polytecnic college tunachoweza kukujibu ni kwamba hakikuwa miongoni mwa vyuo vinavyotambuliwa na Wizara ya Kilimo, chakula na Ushirika lakini kinatambuliwa na Mamlaka ya Mafunzo ya Ufundi stadi (VETA) hivyo Sekretarieti ya Ajira bado inafanya mawasiliano na Wizara husika na taarifa kuhusu wahitimu wanaomba ajira na wamesoma katika chuo hicho, watapewa taarifa baada ya kupata muongozo wa Wizara husika.
Swali la 6.
Mimi naitwa samwel mhadisa nilimaliza chuo kikuu cha Dar es saalam mwaka2013 katika bachelor of science general (specialing applied microbiology with chemistry) sasa nilikuwa naomba unipe nafasi ya kuja kuonana na wewe hapo ofisini kwako na mimi sasa hivi nipo hapa Dar es salaam.nitashukru sana endapo ukinipa nafasi hii ya kuja kuzungumza na wewe
Jibu.
Ombi lako limepokelewa, Sekretarieti ya Ajira ni Taasisi ya serikali hivyo haina kizuizi kwa mwananchi yoyoye kufika kwa ajili ya kutaka kupata ufafanuzi wa jambo lolote linalohusiana na mchakato wa ajira serikalini, hivyo hata kama hutampata katibu wa Sekretarieti ya ajira wakati mwingine kutokana na majukumu yake unaweza kukutana na wasaidizi wake ambao pia unaweza kuonana nao na kukupatia ufafanuzi unaouhitaji.
Swali la 7.
 Kutofautiana majina, asante kwa kazi ngumu mnayoifanya ya kutoa maelekezo kwetu sisi wadau wa secretariat ya utumishi. Mimi cheti cha form four nilitumia majina mawili yaani AMANI JONAS, lakini chuoni liliongezeka jina la tatu yaani AMANI JONAS NYABUZOKI
Kwa hiyo natakiwa kwenda kuapa mahakamani au? kwani hilo jina la tatu ni ubini na liko pia kwenye cheti cha kuzaliwa. Natumaini nitapata majibu sahihi. Asante na kazi njema.
Jibu.
Asante kwa kuuliza swali hili, kwa kuwa cheti cha kumaliza kidato cha nne kina majina mawili tu yaani (Amani Jonas) wakati vyeti vingine vya kitaaluma na cha kuzaliwa vinasomeka kwa majina ya Amani Jonas Nyabuzoki hapo tayari  utaona kuna utofauti wa majina na mtu anaweza kudhani ni watu wawili tofauti, Hivyo unashauriwa kwenda mahakamani kuapa (Deed Poll) na utapewa hati inayokutambulisha kwamba majina katika vyeti hivyo yote ni ya kwako.
Swali la 8.
Nauliza hivi karibuni nilituma maombi kwenye zile nafasi 100 za NAO. Jina langu halijatoka ktk majina ya usaili. Je Inawezekana ni kwa sababu niliweka transcript peke Yake? Na kuna mchujo huwa unafanyika kabla ya interview? Mwisho kwenye bahasha yangu natakiwa kuandika post ninayoomba kwa mbele au nyuma ya bahasha? Kazi njema. Joshua Mchiwa, mbeya.
Jibu.
Ni kweli hivi karibuni nafasi hizo ulizotaja zilitangazwa na tayari walioomba kazi baada ya kufanya usaili na kufaulu tayari walishapangiwa vituo vya kazi, swala la jina lako kutotokea katika orodha ya walioitwa kwenye usaili inawezekana ni kutokana na sababu mbalimbali ambazo zinakufanya usikidhi vigezo ikiwemo uliyoitaja hapo juu kwa kuwa Transcript pekee haitoshi kwa kuwa ni lazima iwe pamoja na cheti chake isipokuwa kama umemaliza mwaka huu na cheti bado hakijatoka ndio unaweza kutumia transcript wakati wa kuomba kazi. Swali lako la pili nafasi unayoomba unatakiwa kuandika juu na mbele ya bahasha.
Swali la 9.
Waliopotelewa na vyeti vya taaluma wanapoomba kazi serikalini
Ndugu Katika mamlaka ya ajira Tanzania. Kutokana natangazo la hivi karibuni linalo eleza mambo ya kuzingatia Mimi ni Hemed A. Kavumo mmoja wa watu waliopotelewa na cheti cha form four na nimefanya taratibu zote na Necta na wakadai wameshatuma taarifa zangu tume ya ajira, tatizo ni kwamba sinahakika kua taarifa hizo zimewafikia tume ya ajira. 
Wakati wa kuomba kazi kwa walio potelewa na vyeti napenda kuuliza maswali ya fuatayo.
Mtu aliye potelewa na cheti nakuripoti necta na akaambiwa taarifa zake zitatumwa nivipi atajua kama taarifa zake zakupotelewa na cheti zimewafikia tume ya ajira pindi anapo omba kazi?
Pili ni nanma gani tume ya ajira itafahamu kuwa mtu flani amepotelewa na cheti na sio kuwa hakutimiza vigezo au viambatanisho pindi anapoomba kazi serikalini?
Ushauri wangu ni kwamba aliyepotelewa na cheti na kutoa taarifa kwenye mamlaka husika na taarifa zake kutumwa mamlaka ya ajira apewe majibu kua taarifa zake zakupotelewa na cheti zimefika tume ya ajira na anapoomba kazi aandike barua kueleza kua taarifa za kupotelewa na cheti husika zimeshaifikia tume ya ajira ili kuepusha usumbufu na kuwezesha tume ya ajira ihakiki taarifa hizo. 
Ahsante.
Jibu.
Tumepokea maswali yako, awali ya yote nikupe pole kwa kupotelewa na cheti cha kidato cha nne, Aidha ni kweli kwamba baadhi ya watu waliopotelewa na vyeti vya kidato cha nne na sita wanapoenda kuripoti Baraza la Mitihani (NECTA) juu ya upotevu wa vyeti vyao na wakaomba taarifa za kupoteza vyeti vyao zitumwe Sekretarieti ya Ajira utaratibu huo huwa unafanyika.
A)    Kama ulipoteza cheti ukaripoti NECTA na ukawaomba taarifa zako wazitume Sekretarieti ya Ajira ili kufahamu unapaswa kuwasiliana na Sekretarieti ya ajira ili kuulizia kama jina lako limefika(unaweza kupiga simu kwa namba hii 0687 624975 au tuma ujumbe kwenye ukurasa wetu wa facebook www.facebook.com/sekretarieti ajiara). Pia unapoitwa kwenye usaili siku ya usaili kabla ya kufanya usaili ni vyema ukauliza ili jina lako liangaliwe kwenye orodha yetu tuliyoipata kutoka NECTA kujiridhisha kabla hujaingia kwenye usaili.
B)    Sekretarieti ya ajira itafahamu kuwa mtu fulani amepotelewa cheti kwa kupata taarifa au jina kutoka mamlaka husika inayotoa cheti baada ya aliyepoteza cheti kutoa taarifa na kuomba jina lake litumwe sekretarieti ya ajira kama nilivyoeleza hapo awali.
C)    Ushauri wako umepokelewa lakini pia unakumbushwa kufuata maelekezo yaliyopo katika maelezo ya awali katika jibu la kipengele (a) ili kujiepushia usumbufu usiokuwa na lazima ikiwemo kupunguza gharama.
Swali la 10.
Habari za kazi, hivi mlitangaza nafasi za kazi katika wizara ya mambo ya nje ya receptionist na wahudumu wa ofisi, hivi mlishatoa majina ya watu watakaoenda kwenye usaili?
Jibu.
Ni kweli nafasi ya mapokezi (receptionist) pamoja na kada nyingine zilitangazwa hivi karibuni katika tovuti ya Sekretarieti ya ajira, Tangazo lenye orodha ya waombaji wanaoitwa kwenye usaili wa kada hizo na nyinginezo tayari limetolewa tangu tarehe 6 Desemba, 2014.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Ofisi ya Rais Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma 8 Desemba, 2014.


0 comments:

Post a Comment