Thursday, August 28, 2014

MAMBO YA KUZINGATIA KABLA YA KUOMBA KAZI SERIKALINI


MAMBO YA KUZINGATIA KABLA YA KUOMBA KAZI SERIKALINI
MAMBO YA KUZINGATIA KABLA YA KUOMBA KAZI SERIKALINI KWA WALIOSOMA NJE YA NCHI, WALIOPOTEZA VYETI NA WENYE MAJINA TOFAUTI NA VYETI VYAO
Sekretarieti ya ajira katika kutekeleza majukumu yake ya uendeshaji wa mchakato wa ajira Serikalini imekuwa ikikabiliana na changamoto mbalimbali ikiwemo tatizo la baadhi ya waombaji kazi kupoteza, kuibiwa, kuharibikiwa au kuunguliwa vyeti vya kitaaluma pamoja na vitambulisho vinginevyo. Kutokana na baadhi ya waombaji kazi kutokufahamu taratibu za kufuata pindi wanapopoteza vyeti vyao au wanapobadilisha majina huamua kuwasilisha nyaraka pungufu Sekretarieti ya Ajira jambo ambalo husababisha kukosa nafasi ya kuchaguliwa au kukosa fursa ya kufanya usaili kwa kutokuwa na nyaraka zinazohitajika.
Hali hii imekuwa ikisababisha malalamiko kutoka kwa waombaji kazi wakati wa uhakiki kutokana na baadhi yao kuwa na nyaraka ambazo hazikidhi vigezo vinavyotakiwa kwa mujibu wa tangazo la nafasi ya kazi. Kasoro hizo zimechangia baadhi ya wadau kuitupia lawama Sekretarieti ya Ajira kuwa ina upendeleo, kwa kutokuwaita kwenye usaili wale waliobainika mapema kutokuwa na sifa au kuwazuia kufanya usaili waombaji wasiokuwa na nyaraka halisi na halali ikiwemo vyeti vya kuzaliwa, vyeti vya taaluma. Ili kuthibitisha alichowasilisha awali kwa kuwa wengi wao huwa na result slip, hati matokeo (partial transcript) barua za utambulisho wa upotevu wa vyeti kupitia polisi ambazo baadhi yake huwa zimeshapita muda wake.
Jambo hili limepelekea baadhi ya wahitimu kujikuta njia panda kwa kushindwa kufahamu hatua za kuchukua ama taratibu za kufuata ili kuweza kupata vyeti vingine au namna ya kufikisha taarifa kwa mamlaka husika ili kuweza kupata msaada ama huduma stahili pindi nyaraka hizo zitakapohitajika mahali fulani. Hivyo, Sekretarieti ya Ajira inapenda kuwafahamisha wadau wake hususani waombaji kazi Serikalini kwamba haipokei barua ya utambulisho kutoka polisi inayohusu kupoteza, kuungua, kuibiwa, utofauti wa majina kati ya cheti kimoja na kingine kutokana na baadhi yao kuzitumia vibaya.
WAHITIMU WALIOPOTEZA VYETI WAZINGATIE YAFUATAYO;-
Sekretarieti ya Ajira inawataka wadau wake wote ambao watakuwa wamepotelewa, wameibiwa, wameharibikiwa ama kuunguliwa na Vyeti vya kitaaluma kutambua kuwa wanapaswa kutoa taarifa katika kituo chochote cha polisi kilicho karibu, pili, kupeleka taarifa za kupotelewa vyeti katika mamlaka zinazohusika kama vile Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) kwa vyeti vya kidato cha nne(4) na sita(6), kwa Elimu ya Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) na kwa elimu ya juu ni Tume ya Vyuo Vikuu(TCU) ili waweze kuelekezwa taratibu za kufuata ikiwemo kutoa tangazo katika vyombo vya habari na maelekezo mengine yatakayomwezesha kupata vyeti vingine ama taarifa za upotevu wa vyeti kutumwa Sekretarieti ya Ajira kwa wakati.
WAOMBAJI WALIOSOMA NJE YA NCHI WAZINGATIE YAFUATAYO;-
Sekretarieti ya Ajira pia inawasisitiza waombaji kazi wote waliosoma Nje ya Nchi iwe ni elimu ngazi ya Sekondari au Vyuo Vikuu kwamba mara tu baada ya kumaliza mafunzo wahakikishe wanapeleka taarifa zao hasa Vyeti vya taaluma kwenye mamlaka husika mapema ili kuhakikiwa taarifa zao na kupewa barua zinazothibitisha kutambuliwa kwa Vyuo walivyosoma ambapo mamlaka zenye dhamana ya kuhakiki taarifa hizo ni Tume ya Usimamizi wa Vyuo Vikuu (TCU), Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) na Baraza la Usimamizi wa Elimu ya Vyuo vya Ufundi (NACTE). Kwa kuwa mamlaka hizo ndio zenye dhamana kuthibitisha ama kuwasilisha taarifa za mhusika za kupotelewa na vyeti katika Ofisi za Sekretarieti ya Ajira kwa mujibu wa taratibu za uendeshaji wa Mchakato wa Ajira Serikalini na sio mtu aliyepotelewa kuwasilisha utambulisho wa matokeo ama nyaraka mbalimbali zikiwemo za kitaaluma wakati anapoomba kazi.
WAOMBAJI WENYE MAJINA TOFAUTI KWENYE VYETI WAZINGATIE YAFUATAYO;-
Kutokana na baadhi ya wadau wetu kubadilisha majina yao kwa kutokupenda kuendelea kutumia majina ya utotoni, ya kinyumbani au kubadili dini, kuolewa na kutumia ubini wa mume au kurithi majina ya walezi hali ambayo imechangia wengi wao kuwa na majina tofauti kati ya cheti kimoja na kingine iwe cha kuzaliwa ama cha kitaaluma, Sekretarieti ya Ajira inawataka wale wote wenye tofauti ya majina katika vyeti vyao kufuata taratibu za kisheria kabla ya kuwasilisha maombi ya kazi Sekretarieti ya Ajira kwa kwenda mahakamani na kula kiapo kwa kamishna wa viapo au kwa Wakili ili waweze kupata (Deedpal) au (Affidavity) kwa mujibu wa sheria, na sio kubadili majina kienyeji hali ambayo inaweza kuwanyima haki zao wakati mwingine. Kwa kuwa kufanya hivyo kutawasaidia kuthibitisha uhalali wa tofauti ya majina au majina yake yote kutambulika kisheria.
Mwisho waombaji kazi wote wenye matatizo ya Vyeti wanashauriwa kuzingatia na kufuata utaratibu ulioelekezwa mara tu baada ya kupata matatizo ili taarifa zao ziweze kufika mapema Sekretarieti ya Ajira na pia inaweza kuzuia uwezekano wa aliyeiba au kuviokota kuvitumia. Aidha, itawasaidia wakati wanapoomba kazi kuepuka usumbufu na gharama zisizokuwa na ulazima.
Imetolewa na; Msemaji wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, Riziki V. Abraham.
Barua pepe: katibu@ajira.go.tz, gcu@ajira.go.tz, Tovuti; www.ajira.go.tz, S.L.P. 63100 Dar es Salaam. Simu; 255-687624975


0 comments:

Post a Comment