Thursday, July 31, 2014

AJIRA: Watu 6,740 kuwania nafasi 47 tu za kazi TBS




AJIRA: Watu 6,740 kuwania nafasi 47 tu za kazi TBS LEO

Watu 6,740 leo wanatarajia kufanyiwa usaili wa kuwania nafasi 47 zilizotangazwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Aprili, mwaka huu. 
 
Usaili huo unataka kufanana na ule wa Idara ya Uhamiaji ambao ulihusisha waombaji 10,000 waliokuwa wakiwania nafasi 70, utafanyika leo na kesho katika Ukumbi wa Yombo wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
 
Ili kuepuka kuchaguliwa kwa waombaji wenye uhusiano na wafanyakazi wa shirika hilo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wake, Joseph Masikitiko amesema kuwa kazi ya usaili itafanywa na taasisi nyingine na TBS itapelekewa majina 47 ya watakao kuwa wamekidhi vigezo.
 
Masikitiko alisema ili kuepuka upendeleo pia, wameamua kujivua kusimamia mchakato huo na utafanywa na taasisi mbalimbali, na akiitaja moja ya taasisi hizo kuwa ni ya Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (Sua).
 
"Kuna taasisi tumezichagua zisimamie usaili huo, wao watasimamia na wakikamilisha watatuletea majina hayo," alisema.
 
Alisema wameamua kufanya hivyo ili kuepuka yale yaliyowakumba wenzao wa Idara ya Uhamiaji.
 
Aliongeza: "Hata hizo taasisi tulizoomba zinapaswa zitende haki na ziepuke kutumiwa na baadhi ya watu ambao siyo waaminifu, tunahitaji wafanyakazi watakaopatikana wawe wenye sifa zinazotakiwa."
 
Usaili wa Uhamiaji uliofanyika katika Uwanja wa Taifa Dar es Salasam, ulihusisha zaidi ya watu 6,000 kati ya watu 10,000 walioomba nafasi hizo.
 
Baada ya usaili wa watu 6,115, walipatikana 1,681 ambao waliingia katika kinyang'ayiro cha kusaka watumishi 70.
 
Kati ya nafasi za kazi 22 zilizoombwa, nafasi iliyoombwa na watu wachache ni ya ofisa maabara msaidizi ambayo imeombwa na watu 61 na anatakiwa mtu mmoja.
 

Katika nafasi ya mhasibu msaidizi, wameomba watu 1,360, lakini wanaotakiwa kuajiriwa ni watu watatu tu.


Nafasi zilizotangazwa na shirika hilo na idadi ya walioziomba katika mabano ni ya mhasibu msaidizi (1,350), mkaguzi msaidizi wa ndani (266), msaidizi wa mahesabu (305), ofisa rasilimali watu (857), Ofisa viwango (211), maofisa ubora wa viwango (752) na wataalamu wa hali ya hewa (117).
 
Wengine ni mhandisi wa mitambo (89), fundi mchundo (88), ofisa maabara msaidizi (61), msaidizi wa maabara (141), Mtaalam wa mifumo ya kompyuta (307), katibu muhtasi (247) na ofisa uhusiano wa kampuni na umma (342).
 
Pia kuna nafasi ya dereva (408), wahariri (71), mwanasheria (140), mkutubi (80), msimamizi msaidizi wa kumbukumbu namba moja (230), msimamizi msaidizi wa kumbukumbu namba mbili (501) na ofisa masoko mwandamizi (167).


0 comments:

Post a Comment