Monday, May 12, 2014

THT yatoa vitabu kwa maktaba ya walemavu wa ngozi Kanda ya Ziwa

 
 
 

3

Mlezi wa Umoja wa Wake wa Viongozi Tanzania, Mama Tunu Pinda, akizungumza na waandishi wa habari baada ya kupokea msaada wa vitabu kutoka Tanzania House of Talent. Kushoto kwake ni Mwenyekiti wa Umoja huo, Mama Germina Lukuvi na kulia kwake ni Meneja Mkuu wa Tanzania House of Talent, Mwita Mwaikenda.

4

Mwakilishi wa Kampuni ya Opportunity Education akikabidhi vitabu kwa Mama Tunu Pinda.

7

Nyumba ya vipaji Tanzania (THT) imetoa vitabu vya Sayansi, Sanaa na Hesabu kwa maktaba ya walemavu wa ngozi inayotarajiwa kujengwa na taasisi isiyo ya Kiserikali ya New Millennium Group.

Vitabu hivyo vyenye thamani ya jumla ya shilingi milioni 35 vimetolewa kwa lengo la kusaidia kukuza elimu Tanzania hasa kwa jamii ya walemavu wa ngozi, ikiwa ni mchango wa THT kwa huduma za jamii.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Meneja Mkuu wa Nyumba ya Vipaji Tanzania, Mwita Mwaikenda alisema taasisi yake iliona changamoto ya vitabu baada ya taasisi ya New Millennium Group kutembelea vituo vya maalbino vya kanda ya ziwa mwanzoni mwa mwaka huu.

'Msaada huu wa vitabu sisi kama THT tumeutoa ili kuiwezesha maktaba ya walemavu kupata vitabu vya kujisomea na hivyo kujiongezea maarifa baina yao' alisema Mwita.

Kwa upande wake Mlezi wa Taasisi ya New Millenium Group, Mama Tunu Pinda, alisema wanaishukuru THT kwa msaada huo ambao alisema ni muhimu sana kwa ajili ya lengo lao la kusaidia kuiwezesha kielimu jamii ya watoto wenye ulemavu wa ngozi.

'Hakika msaada huu utasaidia kwa kiasi kikubwa katika kufanikisha lengo la kuanzisha maktaba kwa watoto wenye ulemavu wa ngozi, na tunaaamini msaada huu utawapa changamoto wadau wengine kusaidia kukamilisha maktaba hii ya kwanza kabisa kuhudumia watu wenye ulemavu wa ngozi' alisema Mama Pinda.

Naye Mwenyekiti wa New Millennium Group, Mama Germina Lukuvi anasema pamoja na vituo hivyo kuwa na sehemu ya malazi kwa maalbino bado kumekuwa na changamoto ya sehemu za kujisomea na New Millennium Group itaendelea kushirikiana na wadau wengine kuhakikisha changamoto hizo zinatatuliwa.

0 comments:

Post a Comment