Hujuma ya Miundombinu ya Majisafi, wizi wa Maji ni vitendo vinavyoendelea kufanywa na wananchi licha ya juhudi mbalimbali zinazofanywa na serikali kuhakikisha huduma ya Majisafi ni muhimu kwa kila kaya.
Hayo yameelezwa na Afisa Uhusiano wa DAWASCO Bi, Everlasting Lyaro wakati wa operesheni maalumu inayoendelea ya kuwabaini na kuwakamata wananchi wanaojihusisha na vitendo vya uhujumu wa shirika hilo. Alisema katika zoezi hilo maalum jumla ya watu na vifaa mbalimbali vilivyokuwa vinatumika kinyume na taratibu zilikamatwa.
"Zoezi hili limeanza kwa maeneo yote ya Jiji na jana tulikuwa Kimara Michungwani ambapo tumekamata watu kadhaa na kuchukua matanki manne yenye ukubwa wa lita za ujazo 10,000, pampu 2 na mipira yenye ubora pungufu ya mipira inayotumiwa na inayoshauriwa kutumiwa na DAWASCO" Alisema Lyaro.
"Sisi tunaita huu ni ujangili maana ujangili sio tu kwa wanyama hata kwa maisha ya kawaida binadamu tunafanyiana ujangili mkubwa tu, leo hii mtu anaenda kukata mipira ya Maji ya kaya nzima ambayo wameungiwa kihalali na DAWASCO ili atengeneze mazingira ya yeye kuweza kufanya biashara ya Maji kirahisi hii haikubaliki hata kidogo, biashara ya Maji watuachie DAWASCO wenyewe" alifafanua Lyaro.
Aliongeza kwa kutoa wito kwa wanachi kutoa ushirikiano kwa serikali yao yenye mipango mingi mizuri ya kuwapatia wananchi wake uhakika wa Maji kwa kutoa taarifa za wizi wa Maji na uharibifu wa miundombinu kwa mamlaka husika ili kuleta usawa kwa wananchi katika upatikanaji wa huduma hiyo.
"Changamoto zipo bado katika upatikanaji wa Maji kwa wananchi hasa suala la Migao ya Maji, ila bado juhudi binafsi za wananchi zinahitajika katika kuelewa na kupunguza kero nyingine ambazo si za lazima katika kuipa DAWASCO nguvu ya kufikia malengo yake" alisema Lyaro Upatikanaji wa Majisafi na Salama kwa mkoa wa Dar umekuwa na changamoto mbalimbali, huku suala kubwa ikiwa ni Wizi wa Maji na uhujumu miundombinu ya Maji kwa maeneo mengi ya Jiji la Dar es Salaam.
Nyumba iliyokamatwa kwa uhujumu wa miundombinu ya Maji pamoja na wizi wa Maji eneo la Kimara Michungwani ambapo ilikutwa na tanki 4 zenye ujazo wa lita 10,000 kila mmoja huku wananchi wa eneo hilo wakikosa huduma hiyo kwa takribani miezi 3 kutokana na uhujumu huo.
Sehemu iliyojengwa na wezi wa maji kama kituo cha kusambaza Maji (Pumping Statiion) kwa wateja waliofanya maungio kinyume na taratibu. Ilibainika zaidi ya wananchi wanne katika eneo la Kimara Michungwani.
Afisa uhusiano wa Dawasco, Bi Everlasting Lyaro akionyeshwa sehemu ya maungio ya wezi wa Maji ambapo mipira na pampu zilizotumika kufanya uhujumu uchumi zilikamatwa kwa ushirikiano wa wananchi na kikosi maalum cha DAWASCO.
0 comments:
Post a Comment