Tuesday, September 10, 2013

TIMU YA NETIBOLI YA UTUMISHI YATAKIWA KUJINOA ZAIDI



TIMU YA NETIBOLI YA UTUMISHI YATAKIWA KUJINOA ZAIDI
Wachezaji wa timu ya mpira wa pete ya Ofisi ya Rais,Menejimenti ya Utumishi wa Umma wakijadili jambo mara baada ya mazoezi katika viwanja vya Leaders Club jijini Dar es Salaam.

Timu ya mpira wa pete ya Ofisi ya Rais,Menejimenti ya Utumishi wa Umma imetakiwa kujinoa zaidi ili kujiimarisha na kujiweka katika nafasi nzuri ya kupata ubingwa wa mashindano ya michezo ya SHIMIWI yanayotarajiwa kuanza hivi karibuni mjini Dodoma.

Hayo yalisemwa jana na Naibu Katibu Mkuu,Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma Bw.HAB Mkwizu alipotembelea timu hiyo ili kuangalia maendeleo ya timu iliyokuwa katika mazoezi makali kwenye viwanja vya Leaders Club vilivyopo jijini Dar es Salaam.

Bw.Mkwizu alisema ili timu hiyo iweze kupata ushindi inatakiwa ijiimarishe na kujiongezea stamina kwa kufanya mechi nyingi za kirafiki na timu kongwe hapa nchini.

"Mnatakiwa mfanye mazoezi ya ziada na mcheze mechi nyingi za kirafiki na timu ambazo zimekuwa zikicheza ligi mbalimbali kama Filbert Bayi,Ikulu,Wizara ya Elimu,Wizara ya Afya na JKT." Alisema Bw. Mkwizu.

Aliongeza kuwa iwapo timu hiyo itahitaji msaada wowote ili kufanikisha mechi za kirafiki na kufanya mazoezi yatakayoijenga timu ,kocha asisite kuongea na uongozi wa timu .

Naye kocha wa timu hiyo Bw.Mathew Kambona alisema ana mpango wa kuiboresha kiufundi timu hiyo ili iweze kucheza michuano mbalimbali mwakani.

"Nina mkakati wa kuiimarisha timu na kuiandaa ipasavyo ili tuwe na timu ya kudumu itakayoshiriki kwenye ligi mbalimbali "alisema Bw.Kambona.

Aidha,kocha Kambona alisema timu hiyo kwa sasa inakabiliwa na changamoto ya kutokuwa na kiwanja kizuri cha kufanyia mazoezi ili kujiandaa kikamilifu.

"Tunaomba ofisi itusaidie tupate kiwanja cha mazoezi kwani mashindano yamekaribia na ninahitaji kuiandaa timu itakayotoa upinzani kwa bingwa mtetezi" alifafanua Bw. Kambona.

Kwa upande wa wachezaji wa timu hiyo wameuomba uongozi wa michezo wa Utumishi kuhudhuria katika mazoezi na mechi mbalimbali za majaribio na kushiriki na kocha bega kwa bega ili kubaini mapungufu yaliyopo na kuyaboresha kabla ya mashindano kuanza.

Timu ya mpira wa pete ya Ofisi ya Rais,Menejimenti ya Utumishi wa Umma imedhamiria kunyakua kikombe cha ubingwa kwenye michuano ya SHIMIWI ya mwaka huu itakayofanyika katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Dodoma kuanzia Septemba 20 mwaka huu .



0 comments:

Post a Comment