PONGEZI KWA FRANCIS CHEKA
CHAMA cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) kinatoa pongezi kwa bondia Francis Cheka kwa kuibuka bingwa mpya wa dunia wa WBF katika uzito wa Super Middle.
Cheka alitwaa mkanda huo wa ubingwa baada ya kumshinda Mmarekani, Phil Williams kwa pointi katika pambano la raundi 12, lililofanyika kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam Ijumaa usiku.
TASWA imekunwa na mafanikio hayo na inatoa pongezi za dhati kwa bondia huyo kwa juhudi zake na kulitangaza vyema jina la nchi yetu, hivyo tunasema Cheka atambue familia ya wanamasumbwi na wanamichezo wote Tanzania tumefurahishwa na mafanikio hayo na tunayajali.
(B) MAFUNZO YA WAANDISHI WA HABARI
Kama mnavyofahamu TASWA kwa kushirikiana na Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma (SJMC) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) inaandaa mafunzo ya siku tano kwa waandishi wa habari za michezo nchini.
Mchakato wa mafunzo hayo bado unaendelea kwa uratibu wa karibu kati ya vyombo hivyo viwili, ambapo bado tunaendelea na mazungumzo na wadhamini mbalimbali ili kuyafanya mafunzo hayo yawe bora zaidi na mazungumzo yatakapokamilika tutawajulisha.
Kwa kuwa mafunzo hayo yatakuwa ya mara kwa mara ndiyo sababu mchakato wake unachukua muda mrefu ili pindi yatakapoanza zile ndoto zetu za kusaidia wanahabari wa michezo ziweze kutimia.
UCHAGUZI MKUU
Kamati ya Katiba ya TASWA inatarajiwa kukutana wiki inayoanza kesho kwa ajili ya masuala ya katiba ya chama chetu.
Kama mnavyofahamu chama chetu kimekuwa na utaratibu wa kufanya uchaguzi kila baada ya miaka mitatu na tayari muda umewadia.
Hivyo tunaamini mchakato wa katiba utaenda vizuri na baada ya kamati ya katiba kumaliza vikao vyake, Kamati ya Utendaji ya TASWA itakutana kwa masuala mbalimbali ikiwemo kupanga tarehe ya mkutano wa katiba na pia mkutano mkuu wa uchaguzi wa chama mwaka huu.
Nawasilisha.
Amir Mhando
Katibu Mkuu TASWA
01/09/2013
0 comments:
Post a Comment