Thursday, August 22, 2013

USANII, UJANJA NA UTAPELI UNAVYOTUTIBULIA MAPENZI!


USANII, UJANJA NA UTAPELI UNAVYOTUTIBULIA MAPENZI!

 
NDUGU zangu, tafsiri ya mapenzi kwa harakaharaka ni hisia ambazo zipo moyoni mwa mtu kwenda kwa mwingine, hisia hizi ili ziweze kuwa mapenzi ni lazima ziwe na ukweli na za dhati huku moyo ukiwa na nafasi kubwa katika hilo.

 
Pamoja na ukweli huo juu ya mapenzi lakini hivi sasa maana halisi ya mapenzi imepotoshwa, imebadilishwa na kuwa nyingine. Mapenzi ya siku hizi yamejaa ulaghai mtupu, hayana ukweli, kila siku ni maumivu juu ya maumivu. Kwa nini watu wanaharibu maana halisi ya mapenzi?
Kuna matatizo mengi ambayo yanaweza kutokea ikiwa utakosa uaminifu kwa mpenzi wako, wakati mwingine matatizo hayo huweza kumlenga mwenzi wako moja kwa moja bila kukusumbua wewe lakini mwisho wa siku wewe utakuja kuwa na matatizo zaidi ya hayo unayoyafanya nyuma ya pazia hivi sasa.
Unaweza kujifanya mjanja sana kwa kuunganisha wapenzi zaidi ya kumi huko gizani ukiamini huonekani na hakuna matatizo yoyote ambayo unaweza kuyapata, kumbe unajidanganya maana kuna siku utakuja kuumbuka kwa kuonekana kwako huna uaminifu!
Hivi ni kwa nini maana halisi ya mapenzi hivi sasa imepotoshwa? Ni nani muanzilishi wa upotoshaji wa maana halisi ya mapenzi, utagunduaje kama mpenzi wako ni msaliti wa penzi lako. Haya na mengineyo utayapata katika mada hii, unachotakiwa kufanya ni kufuatana nami.

UTAPELI, UJANJA, USANII...
Wengine huwa ni tabia yao ya asili, siyo mkweli kuanzia malezi ya wazazi wake kwani hayasisitizi juu ya ukweli. Ameshazoea kufanya mambo kiujanja ujanja! Kwa mpenzi wa aina hii ni vigumu sana kudumu naye.
Ni mwepesi wa kutamka maneno ya mapenzi lakini ndani ya moyo wake kuna vitu viwili, kwanza anakutamani wewe na pesa zako na wakati huohuo anatamani kuwa na bwana mwingine kwa ajili ya kuongeza kitega uchumi, hili ni tatizo!
Mwanamke wa aina hii siyo vigumu kukuita majina mazuri ya kimapenzi lakini akiwa hamaanishi kutoka moyoni mwake kwamba anakupenda. Hawa wapo wengi lakini ni vigumu sana kuwagundua mapema. Hawa huharibu kabisa maana halisi ya mapenzi.
Ngoja nikuulize wewe unayemsaliti mpenzi wako, unavyomfanyia mwenzako hivyo unadhani yeye hana moyo? Hivi hujui kuwa mwenzako anakupenda kwa mapenzi yake yote na amekuchagua wewe uwe mwandani wake? Siku akijiua kwa sababu yako utakuwa katika hali gani? Hebu acha utapeli wako wa mapenzi haraka sana!
Kuwa muwazi na kama unadhani haupo tayari kuwa na mpenzi basi mwache huru atafute mwingine mwenye msimamo uendelee na mambo yako na kama ni kujiuza ujiuze vizuri lakini ukijua kuwa siku moja utakuja kuingia mahali pabaya. Achana na tamaa za muda mfupi ambazo mwisho wake ni mbaya.
Huyo mwanaume anayekudanganya leo, ujue kabisa kesho hayupo na wewe na atakuwa amekuachia virusi vyako vya kutosha! Kama umeamua kujitoa sadaka ni bora ukafa peke yako kuliko kumwangamiza na mwenzako ambaye hana hatia zaidi ya penzi lake la dhati kwako.

USHAWISHI...
Hili ni tatizo lingine linalochochea kuharibu maana ya mapenzi, ushawishi ni sumu nyingine katika hili. Hapa nitazungumzia pande mbili, ya kwanza ni ya mshawishi na mshawishiwa! Naweza kusema wote wana makosa maana anayeshawishi hutumia kila njia kumpata anayemhitaji lakini wakati huohuo anayeshawishiwa kukubali wakati akijua ana mpenzi ni kosa kubwa sana.
Wanaume wengi watu wazima tena wenye familia zao hivi sasa ndiyo wanaoongoza kutafuta dogodogo wakidai kuwa damu zao zinachemka! Hutumia fedha, magari na kila aina ya vishawishi ili waweze kuwanasa wasichana hao wadogo wakitafuta penzi. Sijui wanaume wa aina hii wanatafuta nini kwa hao mabinti?

Itaendelea wiki ijayo.



0 comments:

Post a Comment