Tuesday, August 27, 2013

Mmoja wa wanaume waliomwoa mke mmoja atoroka + Katuni ya Gado


Mmoja wa wanaume waliomwoa mke mmoja atoroka + Katuni ya Gado
Imeandikwa na  WINNIE ATIENO, Kenya — MMOJA wa wanaume waliotia saini mkataba kuishi na mwanamke mmoja alitoroka Jumatatu akisema maisha yake yamo hatarini.

Bw Sylvester Mwendwa, mwenye umri wa miaka 26, alisema aliamua kuacha nyumba zake mbili ambazo amempangia Bi Joyce Wamboi, baada ya mwanamke huyo kumfokea kwa kufichua siri ya ndoa hiyo.

Akizungumza na Taifa Leo kwenye ufuo wa bahari Hindi, alikoenda kupitisha siku akifikiria kwa kwenda, Bw Mwendwa alisema Bi Wamboi alikasirika sana hasa baada ya wanawake kumvamia nyumbani kwake mtaa wa Kisimani, Kisauni na kumzoma wakisema amewaaibisha.

Wanawake hao walisema walikasirishwa na habari katika gazeti la Taifa Leo kwamba Wamboi amejumuisha
 mwanamume wa pili - Bw Elijah Kimani - katika ndoa yake.

Walimkemea kwa hasira Wamboi, ambaye alipoteza mumewe kwenye ajali ya barabarani, kwa kumsaliti Bw Mwendwa, ambaye wanasema wamemtambua kuwa mumewe halisi kwa miaka yote minne ambayo wamekuwa pamoja: "Wamekuja nyumbani na kumkemea mke wangu. Wamemwambia kwamba wamekuwa wakinijua mimi tu, kumbe yeye amekuwa na mwanamume mwengine ambaye hawamfahamu," akasema Bw Mwendwa huku akipangusa machozi.

Alisema bado anampenda Wamboi, ambaye amempangishia nyumba mbili - moja yao wawili na nyingine ya watoto na dada yake Wamboi.

Inasemekana kuwa Bw Mwendwa pia alimfungulia Wamboi biashara ya mboga.

Alisema biashara hiyo huleta karibu Sh8,000 kwa siku lakini hachukui hata senti moja ili kumwezesha Wamboi kugharamia mahitaji yake na ya watoto wake ambao anasema anawachukulia kuwa wanawe pia: "Nilimpata na watoto wawili wadogo punde baada ya kufiwa na mumewe. Nilichukua mkopo benki na kumfungulia biashara. Nimewatunza watoto hao kama wangu bila kinyongo. Inasikitisha kwamba sasa ameshikana na mwanamume kutoka kwao na amenikasirikia kwa kutoboa siri," akasema Bw Mwendwa.

Mmoja wa watoto hao pacha yuko mwaka wa pili katika shule moja ya chekechea.

Bw Mwendwa pia alipata pigo jingine Jumatatu alipofutwa kazi katika duka la nyama mjini Mombasa kwa madai kuwa amewaaibisha wanaume kwa ndoa yake hiyo: "Nimefika kazini leo (Jumatatu) na mwajiri wangu akaniambia sina kazi tena kwa sababu kitendo nilichofanya ni cha aibu," akasema.

Na licha ya kufikwa na mikosi yote hiyo, Bw Mwendwa anasema bado anampenda Bi Wamboi na kama si kwa hasira alizonazo, yuko tayari kuishi naye wakati wowote: "Nampenda sana na sitajali kuwa naye wakati wowote. Nimetoroka tu kwa sababu ana hasira na yule mwanamume mwengine ni wa kabila lake. Nahofia wanaweza kula njama waniangamize," akasema.

---via swahilihub.com



Related Posts:

0 comments:

Post a Comment