Sunday, August 18, 2013

Dr.Reginald Mengi mwenyekiti mpya wa bodi TPSF




Dkt. Reginald Mengi mwenyekiti mpya wa bodi TPSF
 Mwenyekiti mpya wa bodi ya Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) Dkt. Reginald Mengi akimkabidhi zawadi Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji na Uwezeshaji), Dkt. Mary Nagu kama njia ya kutambua mchango wake katika kuendeleza sekta hiyo hapa nchini.  Tukio hili lilifanyika jijini Dar es Salaam mwishoni wa wiki wakati wa mkutano mkuu wa 14 wa mwaka wa taasisi hiyo.
 Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Bw. Godfrey Simbeye (kushoto) akimpongeza Dkt. Reginald Mengi baada ya Mkutano Mkuu wa 14 wa mwaka wa taasisi hiyo kumchagua kuwa mwenyekiti wa bodi.  Mkutano huo uliofanyika jijini Dar es Salaam 

Mwenyekiti wa bodi anayemaliza muda wake wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Bi. Esther Mkwizu (kulia) akimpongeza Dkt. Reginald Mengi baada ya kuibuka mshindi wa kiti hicho cha uongozi katika uchaguzi ulifanyika wakati wa mkutano mkuu wa 14 wa mwaka wa taasisi hiyo jijini Dar es Salaam mwishoni wa wiki.  Wengine katika picha ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji na Uwezeshaji, Dkt. Mary Nagu (aliyekaa) na Makamu Mwenyekiti mpya wa taasisi hiyo, Bw. Salum Shamte (wa pili kulia).
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa mwaka wa 14 wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini (TPSF) wamemchakua Dkt. Reginald Mengi kuwa Mwenyekiti mpya wa Bodi ya taasisi hiyo katika uchaguzi uliofanyika mwishoni mwa wiki.
Uchaguzi huo mkuu ulikuwa ni sehemu ya mkutano mkuu wa mwaka ambapo taasisi hiyo ilitumia fursa hiyo kufanya uchaguzi wa kupata bodi mpya baada ya bodi iliyokuwa ikiongozwa na Bi.Esther Mkwizu kumaliza muda wake.
Uchaguzi huo ulioendeshwa kwa njia ya kura ulisimamiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Bi. Joyce Mapunjo.
Wajumbe wa mkutano mkuu waliopiga kura walikuwa 73 ambapo Dkt. Reginald Mengi alipata kura 39 huku mgombea mwingine, Salum Shamte akipata kura 34.  Hapakua na kura iliyoharibika.
"Kulingana na sheria ya taasisi hii aliyepata kura nyingi anakuwa mwenyekiti mpya wa bodi ya wakati aliyepata kura pungufu anakuwa Makamu Mwenyekiti wa Bodi," alisema Bi. Mapunjo alipokua akitangaza matokeo hayo.
Kwa maana hiyo, Bw. Salum Shamte anakua Makamu Mwenyekiti mpya.
Viongozi hao wapya watahudumu katika nafasi hizo kwa muda wa miaka miwili na baada ya kumaliza wanaweza kuingia katika uchaguzi tena kuomba ridhaa ya kuongoza katika kipindi cha pili.
Mkutano huo mkuu pia uliwachagua wajumbe 11 walioomba uongozi kupitia kongano wanazotoka ili kuwa wajumbe wa bodi hiyo.
Wajumbe wa bodi waliochaguli ni pamoja na Bw.Deodatus Mwanyika atakaewakilisha kongano ya Nishati na Madini, Felix Mosha (Uzalishaji/ Viwanda), Bw. Enock Dondole (vikundi vya biashara mikoani), Bi. Anna Matinde (wajasirimali wanawake), Bw. Mbarouk Omar (Taasisi ya Sekta Binafsi Zanzibar).
Wengine ni Eng.Peter Chisawillo (Biashara), Bw. Salum Shamte (Kilimo), Bw. Gaudence Temu (Rasilimali na Utalii), Dkt. Gideon Kaunda (Makampuni), Dkt. Charles Kimei (Benki na huduma za kifedha) na Dkt. Reginald Mengi (huduma).
Baada ya kutangazwa mshindi, Dkt. Mengi alisema katika kipindi chake atashirikiana na bodi na sekretarieti ya TPSF kuhakikisha yale yote mazuri yaliyofanywa na uongozi uliopita yanaendelezwa.
"Tunahitaji kuzidi kuifanya sekta hii kuwa na sauti moja na yenye nguvu ili iweze kushiriki vema katika uchumi wa  nchi yetu," alisema na kuongeza kuwa sekta hiyo ndiyo injini ya uchumi wa taifa.
Alitoa changamoto kwa serikali kutumia fursa za rasirimali zilizopo nchini kwa kuwapa kipaumbele watanzania kwa ajili ya maslahi zaidi ya nchi kama zilivyofanya nchi za Korea kusini na Malasia.
Alisema mataifa yote duniani yanaweka kipaumbele zaidi kwa watu wake katika nyanja zote.
Akitoa mfano alisema kwasasa ambapo linaanza kuvuna rasirimali ya gesi na rasirimali nyingine, ni vyema vitalu vitolewe kwa ajili ya kuvuna gesi baada ya kuwa sera inayoongoza uchimbaji huo kupatikana.
"Ili nchi iweze kufaidika zaidi ni vema watanzania wakapewa vitalu vya kuchimba gesi ili wakatafute wabia au fedha toka taasisi za fedha za kimataifa kwa ajili ya kuvuna ili faida kubwa ibakie nchini," alisema.
Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF, Bw. Godfrey Simbeye alisema taasisi hiyo imepata kwa mara nyingine viongozi mahiri katika nyanja ya maswala ya biashara na wenye ushawishi katika kuzungumza na serikali.
"Tunategemea bodi hii itazidi kuwa kichocheo na tutazidi kufanya vizuri zaidi kutokana na uzoefu wa viongozi hawa na mafanikio yatakuwa makubwa kwa faida ya taifa zima," alisema.
TPSF ni taasisi ya sekta binafsi inayoundwa na na vyama vinavyowakilisha sekta binafsi  mbalimbali nchini.




0 comments:

Post a Comment