Na Happiness Shayo
Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika tamasha la michezo (sports bonanza) la uzinduzi wa michezo ya SHIMIWI litakalowashirikisha Watendaji Wakuu wa Serikali na watumishi wa umma litakalofanyika siku ya jumamosi Agosti 24 mwaka huu majira ya saa moja asubuhi katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Hayo yalisemwa na Kaimu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) Bw. Moshi Makuka akiwa ofisini kwake mapema leo.
Alisema dhumuni la michezo hiyo ni kujenga na kulinda afya za viongozi na watumishi,kuboresha mahusiano kazini,kujenga mshikamano kwa watumishi,kujenga utaifa na kuondoa tofauti baina ya watumishi.
Alifafanua kuwa bonanza hilo litaambatana na matembezi na mazoezi ya viungo.
"Bonanza litahusisha matembezi (jogging) kutoka Uwanja wa Taifa kupitia Klabu ya Sigara,mataa ya Chang'ombe polisi hadi Uwanja wa taifa pamoja na mazoezi ya viungo yatayoendeshwa na wakufunzi wa michezo"
Aidha,amewahimiza watendaji wakuu wa Taasisi za Serikali na watumishi wa umma kuhudhuria tamasha hilo la michezo lililoandaliwa kwa ajili yao.
Kufanyika kwa tamasha hilo ni utekelezaji wa agizo la Katibu Mkuu Kiongozi na Mkuu wa Utumishi wa Umma Balozi Ombeni Sefue ambapo aliziagiza taasisi zote za serikali nchini kushiriki kwenye michezo ili kuimarisha afya zao.
0 comments:
Post a Comment