Na Ezekiel Kamanga,Mbeya
Ajuza mwenye umri wa miaka 80 aliyefahamika kwa jina la Bi. Janeth Nenje, amenusurika kifo baada ya kucharangwa na mapanga na mtu aliyefahamika kwa jina la Pato Lwiza Mkazi wa Kitongoji cha Chang'ombe,Kijiji cha Mbuyuni Wilaya ya Chunya Mkoani Mbeya.
Tukio hilo la kusikitisha limetokea kijijini hapo Septemba 19 mwaka huu majira ya saa mbili usiku ambapo mtuhumiwa alimfuata ajuza huyo nyumbani kwake na kuanza kumcharanga kwa mapanga na kisha kumjeruhi vibaya hali iliyopelekea kukimbizwa katika Kituo cha Afya kilichopo kijijini hapo.
Imedaiwa kuwa siku za hivi karibuni mtuhumiwa Bwana Lwiza alimtuhumu ajuza huyo kuwa ni mshirikina hali iliyomfanya kuingiwa na hasira na kumtendea ukatili huo sehemu mbalimbali za mwili wake.
Aidha Bi. Nenje hivi sasa amelazwa katika kituo hicho cha afya cha Mbuyuni na hali inaendelea vema.
Baada ya msako mkali wananchi walifanikiwa kumkamata Bwana Lwiza na kuanza kumsulubu kabla ya kuokolewa na Afisa Mtendaji wa Kijiji Bwana Mwashiuya kwa kushirikiana na Mgambo wa Kijij hicho kabla ya kukabidhiwa mikononi mwa polisi wa Kituo cha Mkwajuni.
Katika tukio jingine Mwananchi mmoja Mkazi wa Kijiji cha Lulasi,Kata ya Mpombo Wilaya ya Rungwe Mkoani hapa ameuawa na mtu au watu wasiuofahamika kisha kutumbukizwa katika Kisima cha Maji safi kinachomilikiwa na mmoja wa wakazi wa kijiji hicho.
Tukio hilo limegunduliwa na wananchi wa kijiji hicho waliokuwa wakiteka maji katika kisima hicho na kubaini harufu kali katika maji hayo yanayotumika katika matumizi ya nyumbani kama vile kunywa,kupikia na kufulia.
Hali ilizidi kuwa mbaya Septemba 22 mwaka huu majira ya saa 8 mchana baada ya wananchi kadhaa waliokuwa wakiteka maji hayo kuambua kukivunja kisima hicho kinachomilikiwa na Bwana Noah Mwambalaswa na kuukuta mwili wa marehemu ukiwqa kichwa chini miguu juu,hivyo taarifa kutolewa kwa viongozi wa kijiji hicho.
Mwenyekiti wa Kijiji hicho Bwana Jimmy Mwalupaso amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo Daktari wa Hospitali ya Wilaya hiyo alifika eneo la tukio na kuufanyia uchunguzi mwili wa marehemu na kubaini kuwa alipingwa na kitu kizito(nondo) kichwani hali iliyompelea marehemu kuvuja damu nyingi mpaka mauti yalipomfika.
Hata hivyo baada ya uchunguzi wa daktari mwili wa marehemu ulikabidhiwa kwa ndugu wa marehemu kwa ajili ya mazishi yaliyofanyika kijijini hapo Septemba 23 mwaka huu.
0 comments:
Post a Comment