…KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA KWA MWAKA WA FEDHA 2012/2013
1.0 Utangulizi
Mheshimiwa Spika, nachukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu, kwa kunipa afya njema na kuendelea kunisimamia katika shughuli zangu za kutumikia wananchi wa Jimbo la Nyamagana huku nikiamini kwamba hakuna silaha itakayopandikizwa dhidi yangu itakayoniangamiza maana hiyo ni ahadi ya Mungu kwangu.
Mheshimiwa Spika, pia naishukuru familia yangu, mke wangu Flora pamoja na watoto wetu, mama yangu mzazi na wapiga kura wangu wa Jimbo la Nyamagana kwa maombi yao na kwa kunitia moyo siku zote huku wakinikumbusha kuwa imara na jasiri kama Mungu alivyomuagiza Joshua.
Mheshimiwa Spika, namshukuru Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Mhe Freeman Aikael Mbowe (Mb) kwa imani yake kwangu pamoja na Naibu wangu Mhe Raya Ibrahim (Mb) kuwa wasemaji wakuu katika Wizara hii ya Mambo Nje na Ushirikiano wa Kimataifa. Sambamba na hilo ni kwa chama changu- CHADEMA kwa kunipa moyo na kwa maelekezo ya mara kwa mara katika kuhakikisha kuwa CHADEMA kinaendelea kuwa Chama Tawala Wilaya ya Nyamagana. Na tunaamini wakati utafika Watanzania wote watasimama na kupaza sauti zao kwa kusema Nguvu ya Umma (People's Power).
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge, kanuni ya 99(7) toleo la mwaka 2007, napenda kutoa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani kama ifuatavyo:
2.0 Diplomasia yetu na sura yetu Kimataifa
Mheshimiwa Spika, kutokana na mabadiliko ya kiuchumi, kijamii na kisiasa kimataifa, Tanzania kama ilivyokuwa kwa nchi nyingi duniani, ililazimika kufuata upepo kwa kukubaliana na kitu kinachoitwa Diplomasia ya Kiuchumi, ambayo kwa hakika, moja ya malengo yake hasa ni kuhakikisha masuala na maslahi ya msingi ya taifa huru yanazingatiwa kwa nguvu zote.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha unaoisha, 2011/2012, tumeshuhudia nchi yetu ikiendelea kuzungumza kwa maneno na maandishi kuwa nchi yetu inatekeleza diplomasia ya kiuchumi wakati katika matendo ya serikali yetu hasa wakiongozwa na viongozi wakuu wa nchi, tunaonekana tukitekeleza sera ya diplomasia ya ombaomba!
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaona kuwa sababu ya serikali hii hasa kupitia kwa viongozi wake wakuu, kutekeleza kwa vitendo sera ya kuombaomba kimataifa, kwa Nchi za Magharibi na Asia, ni mojawapo ya sababu kubwa ya Tanzania kupoteza heshima katika siasa za dunia, na kwa hakika sasa mahusiano yetu na nchi nyingi za nje yamejengeka kiutegemezi zaidi, kupungua kwa urari wa kibiashara na kuachia mianya ya uporwaji wa rasilimali zetu.
Mheshimiwa Spika, historia iko wazi kuwa sauti ya leo ya Tanzania katika mahusiano na nchi za nje, si ile iliyokuwa ikitufanya tutembee na kujitapa kifua mbele kimataifa kwa Utanzania wetu wakati wa uongozi wa awamu ya kwanza wa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere.
Mheshimiwa Spika tutatoa mifano miwili hapa iliyotokea katika mikutano ya kimataifa ambayo inadhihirisha kuwa Tanzania imepoteza sauti yake katika medani mbalimbali za kimataifa na hata viongozi wetu kupoteza heshima mbele ya macho ya kimataifa.
Mheshimiwa Spika, wakati wa Mkutano wa Davos, hasa wakati ambapo aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Gordon Brown alipokuwa akiongoza mdahalo juu ya Afrika, kuliibuka mjadala katika Mtandao wa Gazeti la The Guardian (itakumbukwa kuwa hili ndilo gazeti ambalo liliandika sana juu ya ufisadi wa rada uliofanywa na BAE Systems na baadhi ya viongozi wa serikali hii), Mheshimiwa Spika kwa faida ya bunge lako na Watanzania, tutanukuu baadhi ya maoni ya gazeti hilo; Baadhi ya maoni hayo ni kama ifuatavyo;
"Rais Kikwete wa Tanzania ni mmoja wa viongozi wa Afrika ambao dhaifu/pathetic katika nyakati hizi, ni kiongozi wa nchi ambayo ni moja ya nchi zenye utajiri wa mkubwa wa rasilimali duniani, lakini bado anaongoza duniani kwa kuomba. Kampuni nyingi za kigeni zinaijua Tanzania kama moja ya nchi yenye mianya myepesi ambayo unaweza ukaingia na ukachukua unachotaka bila kuulizwa chochote.
Nashindwa kabisa kuelewa juu ya akili za viongozi wa nchi hiyo ambao wanaabudu wazungu…nimefanya kazi katika nchi hiyo kwa miaka 8, nikiwa mtumishi wa UNDP. Niligundua jinsi uongozi wa nchi hiyo usivyokuwa na ufanisi na ulivyoathiriwa na rushwa. Mawaziri wake waliokula rushwa katika kashfa ya rada kutoka Kampuni ya BAE hawajawahi kushtakiwa mahali popote pale, pamoja na kuwepo kwa ushahidi ulio wazi dhidi yao.
Walipa kodi wa Uingereza lazima waache kuendelea kusapoti ziara za nje za viongozi hawa wala rushwa. Rais Kikwete hana sababu yoyote ya kwenda Davos kuomba misaada kwa mataifa ya nje. Nchi yake tayari ni ya tatu kwa kuongoza kupokea misaada. Anapaswa kuona aibu kusema mbele ya dunia nzima kuwa watu wake ni maskini. Watu wake kuendelea kuishi maisha ya umaskini…ni uzembe wa viongozi. Huo ni mzigo wake mwenyewe.
Watanzania wana matatizo yao, Waingereza nao wanayo ya kwao, lazima tutambue hilo. Hatuwezi kugharamia ziara zake za nje ya nchi. Anapaswa kutumia vyema rasilimali za nchi yake. Badala ya kuachia maofisa wake wala rushwa na wageni kuendelea kupora nchi yake, anapaswa kufikiria vyema asiendelee kuwa mtu wa ajabu duniani. Niliwahi kusoma katika moja ya magazeti ya Kenya yakidhihaki ziara zake nje ya nchi. Uchumi wa nchi Lebanon, Haiti, Palestina hata Rwanda ni mzuri kuliko Tanzania.
Kunapaswa kuwepo na sheria kuwazuia viongozi wote wala rushwa na watoto wao kuingia Ulaya. Simlaumu Kikwete, nawalaumu Watanzania kwa kuachia haya yatokee. Wanapaswa kuwajibika asilimia 100 kwa umaskini na matatizo yanayowakabili. Tusingependa waendelee kuombaomba, Wapo Waingereza hawana kazi, tungetumia fedha hizo (za misaada) kuwalipa malipo yao ya kutokuwa na ajira." LindaCroucher
(www.guardian.co.uk/business/2012/jan/26/davos-2012-day 2)
Mheshimiwa Spika, Tanzania iliyokuwa na sauti katika Mazungumzo baina ya Nchi za Kusini(Nchi zinazoendelea) na Nchi za Kaskazini (Nchi zilizoendelea) Tanzania iliyokuwa na sauti mstari wa mbele Kusini mwa Afrika, sasa imekuwa nchi ya kunyamaza kwenye masuala ya msingi kabisa kama haya. Kambi Rasmi ya Upinzani inauliza i-wapi sauti ya Watanzania katika anga la kimataifa? Serikali ya CCM imeipeleka wapi sauti hiyo ya Watanzania iliyokuwa ikiheshimika miaka ile wakati wa Mwalimu?
Mheshimiwa Spika, hali ya Tanzania kupoteza sauti katika medani ya kimataifa pia ilidhihirika katika mkutano kuhusu mabadiliko ya tabia- nchi (COP 17) uliofanyika nchini Afrika Kusini; wakati nchi yetu ikiwa ni miongoni mwa waathirika wakubwa wa mabadiliko ya tabia nchi kutoka hewa chafu inayozalishwa na mataifa makubwa (ambayo ndiyo tunayakimbilia kuomba misaada), Tanzania haikuweza kusema lolote. Tunaweza kukubaliana na watu wengine wanaotoa maoni kuwa ujumbe wetu katika masuala muhimu ya kimataifa kama hili ya namna ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia-nchi unahusisha watu wasiokuwa na ushawishi na diplomasia hitajika.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaona kuwa iwapo hatua za makusudi hazitachukuliwa kurejesha heshima na sauti ya Tanzania kimataifa maamuzi mengi yatafanyika yenye athari kwa wananchi wengi bila ushiriki wao thabiti kama yanayoendelea hivi sasa kuhusu Mikataba ya Kiuchumi na Nchi za Jumuia ya Ulaya (EPA) yenye madhara kwa wakulima na wenye viwanda nchini.
3.0 Balozi zetu nje ya nchi
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa ya Serikali ni kuwa kwa kipindi cha miaka 50 ya uhuru tumefanya ufunguzi wa balozi mbalimbali katika nchi za nje, na zipo balozi 32; balozi ndogo tatu; Vituo viwili vya Biashara; na Konseli za Heshima 17. Aidha, Serikali, kwa kupitia Wizara, inamiliki majengo yake yapatayo 90 nje ya nchi. Kati ya hayo 22 ni ofisi za balozi, 20 ni makazi ya balozi na 48 ni makazi ya maofisa. Kambi Rasmi ya Upinzani tunataka kujua majengo haya yako nchi gani na je? Yana hatimiliki au yako hali gani mpaka sasa?
Mheshimiwa Spika, kwa sababu sera ya Tanzania katika mahusiano ya kimataifa sasa inaongozwa na diplomasia ya uchumi, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kujua ni kwa kiwango gani serikali hii kupitia kwa mabalozi wetu, hususan katika nchi ambazo ni maeneo maalum katika mikakati yetu ya kunufaika kiuchumi, imefanikiwa kutekeleza dira na dhima ya sera yetu hiyo mpya tangu mwaka 2004?
Mheshimiwa Spika, tunasema hivyo kwa sababu, pamoja na serikali kusisitiza sana sera yetu katika mahusiano ya nje kuwa ni diplomasia ya kiuchumi, mpaka sasa tunazo taarifa za balozi hizi kutokuwa katika hali yoyote ya kuweza kufanikisha lolote katika utekelezaji wa vitendo wa sera hiyo, kwa sababu ofisi zao hazitengewi fedha, hazina watumishi wa kutosha, hazina vitendea kazi. Kutokana na ukweli huo, imefikia hatua waambata katika baadhi ya balozi zetu hawawezi kufanya kazi, hata inapolazimika kusafiri, wanashindwa kwa sababu hawana mafungu.
Mheshimiwa Spika, Hali hii inadhihirisha kuwa hii dhana ya diplomasia ya uchumi inayozungumziwa sana na serikali hii, haiko katika uhalisia wake kimatendo bali iko zaidi katika maneno na maandishi.
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inahoji ni kwa nini serikali haioni kuwa ni wakati mwafaka sasa wananchi wakapata tathmini ya kina namna gani kila balozi yetu nje ya nchi imeweza kutekeleza kwa vitendo dhana hii, wakijielekeza katika kuhakikisha nchi inanufaika kiuchumi katika kila uhusiano inaofanya nje ya nchi katika mataifa na taasisi mbalimbali duniani.
Mheshimiwa Spika, ukiangalia katika randama ya serikali, mbali ya kutengewa fedha za posho, hakuna mahali popote ambapo serikali imethubutu kufanya uamuzi wa busara wa kutenga fungu kwa ajili ya utekelezaji kwa vitendo wa sera ya diplomasia ya uchumi.
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inazo taarifa namna ambavyo balozi zetu nje ya nchi, zikiwemo kwenye balozi muhimu kabisa, zimeshindwa kutekeleza sera yetu hiyo kwa vitendo kwa sababu hakuna fedha zilizotengwa. Maana yake ni kwamba watu wanaoitwa waambata wa masuala ya uchumi hawana fedha hata za kuwawezesha kusafiri kutoka sehemu moja kwenda nyingine.
Mheshimiwa Spika, wakati Wizara ya Mambo ya Nje inaomba jumla ya fedha Tshs. 81,686,503,000 katika fungu 34 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na mishahara, hakuna mahali popote ambapo serikali imeona kuna umuhimu wa kuziwezesha balozi zetu kufanya kazi zake kwa ufanisi katika kuhakikisha tunanufaika kiuchumi katika mahusiano yote ambayo nchi hii inafanya.
Mheshimiwa Spika, wakati Wizara hii katika kasma 6391 inaomba jumla ya Tshs. 16,653,204,000, kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ambayo pia inahusisha ujenzi na ukarabati wa majengo ya balozi zetu mbalimbali nje ya nchi, hakuna mahali popote katika randama ambapo serikali imeomba fedha kwa ajili ya ujenzi au ukarabati wa majengo kwenye balozi muhimu kama Ujerumani, Urusi, Canada, Ubelgiji, London, Kuala Lumpar na nyingine ambazo majengo mengine yanavuja, yamebomoka na hata kunuka.
Kambi Rasmi ya Upinzani tunajiuliza ni mtu gani mwelewa katika nchi za Asia, Ulaya na kwingineko ambaye anaweza kwenda kufanya mazungumzo ya maana kiuchumi katika jengo linalonuka au ambalo limewahi kumkosa kosa kumwangukia balozi wake (Mfano Ubalozi wa Urusi, ambako silingibodi ilikosa kumwangukia balozi wetu)!
3.1 Utendaji mbovu wa Wizara kuhusiana na Balozi zetu
Mheshimiwa Spika, balozi zetu na mabalozi wetu wana hali mbaya sana huko waliko na hii inatokana na ukweli kuwa Serikali haipeleki fedha kwa ajili ya kuwawezesha kufanya kazi zao kwa mujibu wa sheria na mikataba mbalimbali ya kimataifa kama ule wa Vienna Convention ambao unataja haki na stahiki zao. Nitatoa mifano michache hapa.
Mheshimiwa Spika, mnamo mwaka 1975 Msumbiji chini ya FRELIMO walitoa jengo na kutupatia ili liwe ubalozi wetu nchini humo na mpaka leo ndilo tunalitumia. Jambo la aibu ni kuwa tangu tupewe jengo hilo bure tumeshindwa hata kulikarabati na hali hii imepelekea hata wapangaji waliokuwa wamepanga kwenye jengo hilo hususani Ubalozi wa Uganda sasa wameondoka kutokana na ubovu wa jengo hilo. Kambi Rasmi ya Upinzani tunataka kujua ni kiasi gani cha fedha kinahitajika kwa ajili ya kulikarabati jengo hilo na ni kwa nini mpaka leo fedha hazijapelekwa. Aidha fedha za kodi tulizokuwa tunalipwa na wapangaji wetu zimetumika kufanya nini, zimekwenda wapi?
Mheshimiwa Spika, Balozi wetu wa Japan ambaye anahudumia pia nchi ya New Zeland, Balozi wetu wa India ambaye pia anahudumia nchi ya Bangladesh, Nepal na Sri Lanka wote wameshindwa kwenda kujitambulisha kwenye nchi hizo kutokana na hati za utambulisho kukosewa kwenye uchapaji na tayari Wizara ilishaletewa taarifa hizo ili warekebishe lakini mpaka leo hakuna hatua zilizochukuliwa kurekebisha makosa hayo. Kambi Rasmi ya Upinzani, tunataka kujua ni lini hati hizo zitaweza kurekebishwa ili mabalozi wetu waweze kwenda kujitambulisha kwenye nchi hizo na hatimaye huduma za kibalozi ziweze kupatikana.
Mheshimiwa Spika, tulipewa kiwanja nchini Dubai kwa ajili ya kujenga jengo la kitega uchumi lakini mpaka leo hatujaweza kujenga jengo hilo ambalo pia lingekuwa sehemu ya kuhifadhi ubalozi wetu. Kambi Rasmi ya Upinzani tunaishauri serikali kama inaona haiwezi kujenga jengo hilo peke yake na kutokana na umuhimu wa mji huo kibiashara kwa sasa basi serikali iingie ubia na wawekezaji binafsi (PPP) ili kukiendeleza kiwanja hicho
Mheshimiwa Spika, serikali ya Uingereza ilitupatia kiwanja namba 19 barabara ya Denewood Jijini London kwa ajili ya sisi kujenga jengo la Ubalozi wetu ili tuweze kupunguza gharama kubwa za kupangisha ila mpaka leo tumeshindwa kujenga na nchi ya Uingereza imetuandikia barua ya kukitaka kiwanja hicho kwani kimekuwa maficho ya wahalifu kutokana na sisi kushindwa kukiendeleza, Kambi Rasmi ya Upinzani tunataka kujua ni kwa nini serikali imeshindwa kujenga kwenye kiwanja hicho na badala yake tunaendelea na utaratibu wa kupanga ambao unatugharimu fedha nyingi kila mwaka?
Mheshimiwa Spika, mpaka leo tumeshindwa kupata hati miliki ya jengo la ubalozi wetu nchini Kenya. Aidha makazi ya Balozi wetu nchini Canada yana hali mbaya sana na mpaka leo hatujaweza kuyakarabati. Kambi Rasmi ya Upinzani tunataka kupata majibu ya kina kuhusiana na hatua ambazo serikali imefikia katika kuitafuta hati miliki za majengo yetu ya balozi mbalimbali ulimwenguni pamoja na mpango wa kukarabati na kuweka ofisi na makazi ya mabalozi wetu kwenye hali nzuri zaidi.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa sheria zetu, moja ya stahiki za mabalozi wetu ni pamoja na watoto wao kusomeshwa na serikali, ila ukweli ni kuwa wako watoto wa mabalozi wetu ambao wanarudishwa nyumbani kutoka kwenye shule kutokana na serikali kushindwa kupeleka fedha kwa ajili ya ada na mifano ni mingi, Kambi Rasmi ya Upinzani haiwezi kuendelea kuona hali hii ikiendelea kuvumiliwa tena kwani ni vitendo vya kuwadhalilisha mabalozi wetu katika nchi wanakotuwakilisha.
Mheshimiwa Spika, kuna taarifa kuwa baadhi ya balozi zetu zinatuhumiwa kwa kutoa hati za kusafiria kwa wananchi wa mataifa mengine na hasa ya Afrika ya Magharibi na baadhi ya balozi hizo ni zile zilizoko China, Uingereza na Hong Kong. Kutokana na uzito wa tuhuma hizi, Kambi Rasmi ya Upinzani tunataka ufanyike uchunguzi mara moja ili kuweza kubaini ukweli wa tuhuma hizi na kuliondolea taifa aibu hii.
Mheshimiwa Spika, katika hali ya ajabu ambayo inahitaji majibu ya kina kwelikweli kuweza kueleweka ni juu ya ubalozi wetu nchini China, mbali ya majengo ya ubalozi huo kuwa na nyufa na kuvuja wakati wa mvua, ubalozi wetu nchini China hauna hata samani za kawaida za ofisi na nyenzo muhimu kama mashine ya nukushi (fax) au mashine za kurudufu. Tunajiuliza, hivi ubalozi wa namna hii unaweza kufanya kazi gani katika kutekeleza Diplomasia ya kiuchumi.
Aidha, tunaitaka serikali hii itoe kauli bungeni, inapata wapi uhalali wa kuzuia magari ambayo muda wake wa kutumika umepita, wakati nchini China magari yetu matatu pekee yaliyopo katika ubalozi wetu yanavunja sheria mpaka muda huu tunapozungumza kwa sababu yametumika tangu mwaka 2001 na sheria ya nchi hiyo zinasema magari hubadilishwa kila yanapotumika kwa miaka 10!
Mheshimiwa Spika, katika randama ya serikali hakuna mahali popote ambapo ubalozi huu umetengewa fungu kwa ajili ya kufanyia ukarabati wa jengo hilo lenye nyufa na linalovuja, wala hakuna fedha zilizotengwa kwa ajili ya kununua magari, badala yake serikali inaomba Tshs 32, 400,000 kwa ajili ya kununulia mafuta na vilainishi vya magari na Tshs 10,000,000 kwa ajili ya kulipia bima ya magari! Tunauliza hivi hatuoni aibu kuendelea kuvunja sheria huko? Tutakuwa wapi na jeuri ya kuwakemea Wachina pale watakapokuwa wanavunja sheria zetu hapa nchini kama balozi wetu anaongoza kuvunja za kwao?
Mheshimiwa Spika, kama hiyo haitoshi, ubalozi huu pamoja na umuhimu wa China katika mahusiano yetu hasa kutekeleza sera ya diplomasia ya kiuchumi, haina mtaalam yeyote wa masuala ya uchumi, achilia mbali kwamba hata wafanyakazi waliopo bado hawawezi kumudu majukumu yao kusafiri kwenda maeneo mbalimbali, kutokana na ukubwa wa nchi hiyo! Hali hii inakwamisha kwa kiasi kikubwa sana utendaji kazi wa ubalozi huu.
4.0 Kashfa ya Rada na Mabilioni ya Gesi
Mheshimiwa Spika, kwa mara nyingine tena, bila kuchoka, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inalazimika kuzungumzia moja ya kashfa kubwa kuwahi kutokea katika nchi yetu, kashfa inayotokana na rushwa ya rada tuliyouziwa na Kampuni ya BAE Systems ya Uingereza. Tunaendelea kuhoji kwa nini mpaka sasa watuhumiwa wa kashfa hiyo wanaendelea kutembea kifua mbele dhidi ya serikali bila hatua zozote kuchukuliwa.
Mheshimiwa Spika, mpaka sasa haieleweki ni kwa sababu gani nchi hii pamoja na kudai kuwa ina uhuru wa kujiamulia mambo yake yenyewe, iliamua kuliachia suala hili kufanyiwa kazi na Serikali ya Uingereza, kuanzia uchunguzi hadi mashtaka ya kurudishiwa fedha zilizotokana na rushwa ya rada, ambazo kwa sasa zimebatizwa jina tamu la 'chenji ya rada'.
Mheshimiwa Spika, katika hali inayoonesha kuwa baniani mbaya kiatu chake dawa, pamoja na serikali hii kushindwa kufanya uchunguzi na hatimaye kuwashtaki watuhumiwa wa rada, bado ilipobainika mahakamani kuwa tunatakiwa kurudishiwa chenji iliyotokana na rushwa, serikali ilikuwa msitari wa mbele kwelikweli katika kufuatilia chenji ya rushwa na katika kuipangia matumizi.
Mheshimiwa Spika, Tunashindwa kuelewa umakini wa serikali hii uko wapi kwamba inaweza kuweka msisitizo pekee katika kuhakikisha fedha za rushwa ya rada zinarejeshwa nchini, lakini haiwezi kuthubutu kabisa kushughulikia wale waliosababisha upotevu huo wa fedha za nchi kwa njia ya mikataba.
Mheshimiwa Spika, tunahoji usikivu wa serikali hii ambayo pamoja na kelele zote za wananchi walioiweka madarakani kutaka watuhumiwa ufisadi kupimwa kwa kipimo kile kile katika mizani ya sheria na utoaji haki, kama wanavyofanyiwa Watanzania wengine wanyonge, bado serikali imetia masikio pamba na kufumba macho yake kwa mikono, kwamba haiwaoni mafisadi hao wala haisikii kelele za wenye nchi.
Mheshimiwa Spika, taarifa mbalimbali zinazotokana na utafiti na uchambuzi wa kina, zimeweka wazi wahusika wa kashfa ya ununuzi wa rada, zikieleza mchakato mzima namna wizi huo ulivyofanyika, ukiwahusisha Watanzania, wengine wakiwa ni viongozi waandamizi wa Serikali ya CCM na sasa Watanzania wanashangaa kuona watuhumiwa haohao waliopaswa kuwa mikononi mwa sheria, sasa wanachaguliwa kuongoza mhimili muhimu wa bunge! Kambi Rasmi ya Upinzani tunahoji je hii ni dalili ya kuwa dola imetekwa na mafisadi?
Mheshimiwa Spika, zipo taarifa zilizoandikwa na vyombo mbalimbali vya habari kuwa kuna zaidi ya shilingi bilioni 315 kwenye Mabenki ya nchini Uswisi na wanaotuhumiwa na fedha hizi ni pamoja na wanasiasa na wafanyabiashara wa Tanzania. Aidha, taarifa hizo zinabainisha kuwa sehemu ya fedha hizo imetokana na uwekezaji unaofanywa kwenye sekta ya Gesi na mafuta nchini.
Kambi Rasmi ya Upinzani inataka kujua nini msimamo wa serikali kuhusiana na tuhuma hizi na Wizara ilichukua hatua gani katika kufuatilia tuhuma hizi nzito.
4.1 Matumizi ya Fedha za Rushwa ya Rada
Mheshimiwa Spika, taarifa za Serikali zinaeleza kuwa fedha za RADA zilizokuwa zimeporwa na Kampuni ya BAE Systems ya Uingereza inayotengeneza na kuuza vifaa vya kijeshi ilirejesha shilingi bilioni 72.3 ili zitumike katika sekta ya elimu. Katika Kauli ya Serikali iliyotolewa Bungeni na Mhe. Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa alisema, nanukuuu "….Serikali ya Uingereza na Serikali yetu zilijadiliana na kukubaliana kuwa ni vyema fedha hizi za wananchi wa Tanzania zikarejeshwa kupitia Serikali ya Tanzania. Serikali hizi mbili zilikubaliana kuwa fedha hizo zitumike kwenye Sekta ya Elimu. Mpango huo ulikuwa moja ya ushahidi muhimu uliotolewa Mahakamani kumshawishi Jaji kutoa uamuzi wa kuridhia makubaliano kati ya SFO na BAE ….. Kununua vitabu 4.4 milioni kwa ajili ya wanafunzi, vitabu 192,000 Kwa ajili ya walimu kufundishia, madawati 200,000, kujenga nyumba 1,196 za walimu wa shule za msingi vijijini, kujenga vyoo 200,000 kwenye shule za msingi".
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inasikitika sana kwamba, serikali yetu imekiuka makubaliano ya namna ya kuzitumia fedha hizo, kama yalivyofikiwa Mahakamani, hali ambayo ni sawa na kusema kuwa lengo lilikuwa kumdanganya Jaji ili fedha hizo zirejeshwe serikalini na hasa ikizingatiwa kuwa Kambi Rasmi ya Upinzani, wananchi na wadau mbalimbali walipinga fedha hizo kurejeshwa kupitia Serikalini kwani tulijua kwa uhakika kuwa hazitatumika kwa malengo tarajiwa kama ambavyo sasa imedhihirika.
Mheshimiwa Spika, lakini habari mbaya zaidi katika matumizi ya chenji hii iliyotokana na kashfa ya viongozi wa serikali hii kuhongwa, taarifa za serikali ambazo mpaka sasa hazijabadilishwa ni kwamba zabuni ya kuchapa vitabu ilitolewa kwa Kampuni ya Kiingereza ya Oxford University Press, kwa maana hiyo fedha zote hizi kwa kiwango cha thamani ya vitabu zitarudi Uingereza.
Mheshimiwa Spika, mbali ya kwamba msimamo wa Kambi Rasmi ya Upinzani ni kutaka kuona zabuni ya hiyo itolewe kwa wachapaji wa Vitabu wa ndani na sio Waingereza, ili fedha hizo zibakie kwenye uchumi wa ndani kwa kiasi kikubwa, bado tunahoji ni kwa nini mpaka sasa serikali haijabatilisha maamuzi yake ya kuipatia kampuni hiyo ya kiingereza kazi ya kuchapisha vitabu hivyo baada ya kukumbwa na kashfa inayofanana na namna BAE walivyofanya wakati wa 'deal' ya kuuza rada. Kwa sasa tayari Kampuni hiyo imefungiwa (blacklisted) na Benki ya Dunia pamoja na mamlaka ya manunuzi nchini (PPRA).
Mheshimiwa Spika, kufungiwa kwa kampuni hii ambayo ilikuwa imepewa zabuni ya fedha hizo za rushwa ya rada, ni dalili moja tu ya wazi inayothibitisha wasiwasi waliokuwa nao Watanzania wengi namna ambavyo chenji hizo zilizotokana na vitendo vya kifisadi zitakavyoweza kusimamiwa bila kuhujumiwa kifisadi, jambo ambalo ni tabia sugu ya serikali hii ya CCM. Tayari tumeanza kwa mguu mbaya, tunakokwenda mbele katika matumizi ya fedha hizi inaweza kuwa giza tupu, ikizingatiwa kuwa mmoja wa watuhumiwa wa kashfa hiyo kubwa ndiye kwa namna moja ama nyingine anapaswa kuzisimamia namna zinavyotumika, hii ni zaidi ya ajabu!
4.2 Kashfa ya Fedha za Posho za Safari ya Raisi
Mheshimiwa Spika, hivi karibuni kuliandikwa habari juu ya ufisadi uliotokea ndani ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa katika gazeti mahiri kwa habari za uchunguzi la Mwanahalisi kuwa fedha zilizotengwa kwa ajili ya kugharamia safari za Rais Dr. Jakaya Kikwete nje ya nchi zimeibwa. Baada ya taarifa hizo za utafiti wa kina kutolewa, haraka haraka Waziri wa Mambo ya Nje, alijitokeza na kusema kuwa utafanyika uchunguzi kubaini kilichotokea.
Mheshimiwa Spika, baada ya siku chache Waziri Membe akajitokeza, na ambapo safari hii alinukuliwa akisema kuwa baada ya uchunguzi wa mwanzo imebainika kuwa fedha hizo shilingi bilioni 3.5 zilizotengwa kwa ajili ya safari za Rais ndani na nje ya nchi, zipo salama hazijaibwa, bali kilichojitokeza ni kasoro na taratibu za fedha zilizokiukwa na hakuna dalili zozote za wizi.
Mheshimiwa Spika, Gazeti la Mwananchi lilimnukuu Waziri Membe akisema kwamba baada ya kamati aliyounda kumaliza uchunguzi wa mwanzo, ameiagiza kumaliza kazi hiyo mapema iwezekanavyo ili kubainisha kasoro zilizojitokeza. "Kasoro hizo tutakapozibaini tutatoa barua za karipio kali kwa wahusika, hivyo wafanyakazi wa wizara yangu kuweni na amani kwani hakuna aliyehusika."
Kambi Rasmi ya Upinzani inataka kusikia kauli ya serikali juu ya tuhuma hizi za ufisadi ambao sasa unaonekana kukithiri hadi fedha za Rais za safiri nazo zinafisadiwa, kwa sababu kwa nukuu hizi inaonekana dhahiri Waziri Membe anajichanganya. Hatujui hali hii ya Waziri kuwa na tabia ya kutoa kauli zenye utata, zina lengo gani. Aidha, tunamtaka Mthibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya uchunguzi wa kina kuhusiana na fedha hizi kwani ni aibu kwa taifa; na taarifa yake itolewe hadharani.
Mheshimiwa Spika, tunasema hivyo kwa sababu hivi karibuni pia Waziri huyuhuyu alinukuliwa akisema anawataka watuhumiwa wa kashfa ya ufisadi wa rada wajitokeze wao wenyewe la sivyo atawataja! Mheshimiwa Spika, tunapenda kumtaarifu Waziri husika kuwa watuhumiwa kashfa hiyo mbali ya kutajwa katika kitabu hicho alichokinukuu, wametajwa na kuzungumzwa kwa kina katika Orodha ya Mafisadi iliyotangazwa pia na CHADEMA, mwaka 2007, Viwanja vya Mwembeyanga. Hivyo, badala ya Waziri huyu kutumia kipindi cha propaganda za CCM na serikali yake kutishia kutaja majina, tunamwambia majina yapo siku nyingi, serikali itoe kauli hapa inachukua hatua gani dhidi ya watuhumiwa hao?
5.0 Ushirikiano Baina ya SADC na BRICS
Mheshimiwa Spika, BRICS ni ushirikiano wa nchi ambazo kutokana na kukua kwa maendeleo ya viwanda, sayansi na kukua kwa kasi kwa uchumi wa mataifa hayo kwa sasa, kuzikimbilia nchi za dunia ya kwanza ambazo kwa muda mrefu zilikuwa zikiitwa nchi zilizoendelea. BRICS inaundwa na nchi za Brazil, Russia, India, China na South Africa.
Kambi Rasmi ya Upinzani inataka kujua mpaka sasa serikali imeweka mikakati gani ili Watanzania wanufaike kwa kiasi kinachotakiwa kutoka katika soko linalotokana na umoja wa nchi hizo tano, ambazo hakika zinapaswa kuwa mfano wa kupigiwa upatu kwa namna ambavyo serikali zake zimepambana kutoka katika hali ya chini katika maendeleo ya uchumi, mpaka sasa zinatishia mstakabali kwa mataifa makubwa.
Aidha, pamoja na kuitaka serikali kutupatia mikakati ya namna ambavyo taifa limejipanga kunufaika katika soko la BRICS ambalo wataalam wa utafiti wanasema sasa lina watu takribani bilioni 3, ambao kwa vyovyote vile ni soko kubwa na muhimu, bado tunaendelea kuitahadharisha serikali hii kuwa makini katika ushirikiano na jumuiya yoyote ile.
Mheshimiwa Spika, ni muhimu sana katika mahusiano yetu na nchi au jumuiya yoyote, iwe BRICS, iwe EU, au katika mahusiano yoyote ya kibiashara kama AGOA na EPA, jambo la kujiuliza ni kama uwekezaji kutoka nje ya nchi ni kwa ajili ya kuisaidia nchi yetu kukua kiuchumi au ni njia tu nyingine ya kuendeleza ukoloni mamboleo kwa kuchuma rasilimali zetu kupeleka kwao, Ulaya au Asia?
Mheshimiwa Spika, tunayasema haya kwa sababu ni ukweli unaodhihirishwa katika mijadala, uchambuzi na tafiti mbalimbali kuwa wenzetu wa nje, kuanzia wale wa zamani kutoka Ulaya hadi hawa wa sasa kutoka Asia, Latini America na Amerika Kusini, pamoja na nia nzuri kama sehemu ya mahusiano yao na sisi, lakini pia wamekuwa na mikakati ya siri ya wao kunufaika na rasilimali za Afrika kuliko Afrika yenyewe.
6.0 Mpango wa Kujitathimini na Utawala Bora Afrika (APRM)
Mheshimiwa Spika, Mpango wa APRM ungeweza kuisaidia nchi yetu kufikia malengo ya Dira ya Taifa, malengo ya Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano na Malengo ya Milenia, iwapo serikali hii ingekuwa makini katika masuala ya maendeleo na utawala bora.
Mheshimiwa Spika, kwa namna ambavyo mpango huu unaendeshwa nchini itakuwa ni vigumu sana kuweza kufikia malengo tarajiwa; mathalani katika Mwaka wa Fedha unaoisha, APRM Tanzania waliomba jumla ya fedha shilingi bilioni 3.835 kwa ajili ya utekelezaji wa mipango mbalimbali iliyokuwa imepangwa ili kutekeleza wajibu wake wa kutusaidia kujitathmini.
Mheshimiwa Spika, pamoja na wajibu mkubwa walionao, mpaka mwaka wa fedha ukielekea mwisho, mpango huu ulikuwa umepelekewa asilimia 53 ya bajeti ambayo ni shilingi bilioni 2.04. Kwa vyovyote vile haimhitaji mtu kuwa mchumi wa kiwango cha juu kujua kuwa APRM-Tanzania, haikuweza kutimiza majukumu yake inavyotakiwa kwa sababu kiwango hiki kilikuwa hakitoshi.
Mheshimiwa Spika, tunataka serikali itoe kauli juu ya tatizo la fedha ambalo limekuwa ni jambo la kawaida sasa tangu mpango huu uanze kufanya kazi hapa nchini, lakini pia serikali inawajibika kusema hapa bungeni ni namna gani majukumu ya APRM-Tanzania ambayo yameathiriwa na kushindwa kufanyika kinyume kabisa na Mkataba wa APRM-AU unavyohitaji na je majukumu hayo sasa yatafanyika lini?
Mheshimiwa Spika, mbali ya suala hilo la kutopata fedha kadri inavyotakiwa kuendelea kukwaza shughuli za APRM-Tanzania, lipo suala jingine ambalo bila shaka linatutia aibu mbele ya watu wengine wa mataifa ya nje na linatia doa nia (kama kweli ipo) ya kujifanyia tathmini katika masuala ya utawala bora na hatimaye maendeleo ya watu wetu, nalo ni deni la miaka minane tunalodaiwa na Makao Makuu ya APRM (Sekretarieti) kama michango ya kila mwaka.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani tunataka maelezo ya serikali ni kwa nini mathalani mpaka sasa, pamoja na mwaka huu tunadaiwa Dola za Marekani 800,000. Ni hali ya kusikitisha kwamba Tanzania ambayo kwa muda mrefu imejijengea heshima katika kutekeleza makubaliano ya kimataifa, katika eneo hili la udhati wa kuchangia uendeshaji wa mpango huu muhimu kwa nchi na Bara zima la Afrika, tumezidiwa na nchi kama Msumbiji, Burkina Faso, Mali, Kenya, Uganda, Lesotho, Ghana, Benin na nyingine katika kulipia michango yao ya kila mwaka.
Mheshimiwa Spika, ni vyema serikali ikatoa kauli kwa nini tumefika mahali Tanzania inashindana katika nafasi za mwishomwisho katika masuala muhimu kama haya na nchi kama, Sao Tome & Principe, Sierra Leone, Mauritius, Kongo na Djibout? Serikali imechukua hatua gani kuondokana na aibu hii ambayo ilianikwa hadharani mbele ya wakuu wa nchi, kwenye Ripoti ya APRM mwaka 2010? Kambi Rasmi ya Upinzani hatukubaliani na udhalilishaji huu ambao unatendeka dhidi ya nchi yetu mbele ya nchi nyingine kwani huku kuendelea kudaiwa na ripoti kuendelea kutusema inatufanya tukose sauti kwenye masuala muhimu barani Afrika na haikubaliki tena kamwe.
Mheshimiwa Spika, bajeti ya mwaka huu serikali imeendelea kupuuza umuhimu wa APRM. Ukisoma katika randama ya bajeti, hakuna mahali popote ambapo mpango huu umepangiwa fungu. Kwa hiyo, ukiongeza na masuala mengine hapo juu ya kupangiwa fedha pungufu na serikali kutokuwa tayari kulipa ada kama inavyotakiwa, kwa pamoja inadhihirika kuwa Tanzania, kupitia serikali ya CCM, haina nia ya kujitathmini juu ya masuala ya utawala bora, hivyo inaweza kuwa nchi ya kwanza kufunga ofisi za APRM hapa nchini!
Mheshimiwa Spika, ni vyema Waziri wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa akaliambia bunge hili ahadi mbili alizozitoa bungeni hapa zimefikia wapi; kwanza aliahidi kuwa ataileta ripoti ya APRM hapa bungeni. Mpaka sasa hatujaona utekelezaji wa suala hilo; tunazo taarifa kuwa Tanzania tayari imeshathibitisha kuwasilisha ripoti yake Januari mwaka ujao, je lini italetwa hapa bungeni?
Ahadi ya pili ni kuwa watafanya utafiti ili sasa APRM iwe na hadhi ya kisheria, lakini mpaka sasa hili nalo halijafanyika, tofauti na nchi zingine kama Kenya au Uganda, hali ambayo inafanya Tanzania kutoweza kutekeleza mapendekezo au maagizo ya APRM. Hali hii nayo inavunja mkataba wa APRM-AU na miongozo ya kiutendaji ambayo tumeridhia sisi wenyewe.
Kambi Rasmi ya Upinzani hatukubaliani na mwenendo huu kwani ni kuendelea kumdhalilisha Rais wetu anapokuwa kwenye vikao vya APRM, Kila siku ripoti zikitoka zinaonyesha kuwa tunadaiwa deni kwa kipindi cha miaka 8 sasa na huku nchi ndogo zikiwa zinatusema tena nyingine zimetoka kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe, uzembe huu kamwe hatukubaliani nao na hatuko sehemu yake na ndio sababu nchi yetu inakosa ushawishi na sauti yake mbele ya mataifa ya Ulimwengu huu.
Mheshimiwa Spika, tangu kuanzishwa kwa Baraza la Taifa la APRM mwaka 2006 wajumbe wa baraza hili ambao jumla yake ni 20 na ambao kimsingi ndio wenye jukumu la kusimamia utendaji kazi wa Sekretarieti ili iweze kufanya kazi zake kwa ufanisi wameteuliwa kwa muda usiokuwa na ukomo isipokuwa kwa upande wa wawakilishi wa Bunge ambao wana ukomo wa muda.
Mheshimiwa Spika, kutokana na wajumbe hawa kutokuwa na ukomo wa muda wa kukaa kwenye nafasi zao kumelifanya baraza hili kuwa na mawazo yale yale na utendaji wake ni ule ule kutokana na kuwa na wajumbe wale wale na ambao barua zao za uteuzi ziliwateua kwa kipindi kisichokuwa na ukomo.
Kambi Rasmi ya Upinzani inapendekeza sasa ni wakati muafaka kwa wajumbe wa baraza hili kuanza kupimwa utendaji wao wa kazi na wawe wanateuliwa kwa kipindi cha miaka 5 kama inavyofanyika kwa wawakilishi wa Bunge na baada ya hapo wanaweza kuteuliwa ama kuachwa kulingana na utendaji wao wa kazi. Hii italisaidia baraza kuwa na mawazo mapya na hivyo kuboresha utendaji wake kuwa wa ufanisi zaidi.
Mheshimiwa Spika, ipo ripoti ya ndani (Country Self Assessment Report) ambayo iliyoandaliwa na Baraza na kuwasilishwa kwenye Sekretarieti ya APRM ya Umoja wa Afrika tarehe 14 mweziJulai 2009. Ripoti hiyo ilibaini mambo mazuri yaliyofanywa na Serikalikatika miaka mitano.Aidha, ripoti ilibaini mapungufu ya utawala bora nchini ambayoyanatakiwa kufanyiwa kazi.
Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali iiwasilishe ripoti hiyo hapa Bungeni na kuweza kujadiliwa ili tuweze kujitathimini na kupanga mpango wa kuondoa mapungufu yaliyobainika kwenye tathimini hiyo kwa ajili ya kukuza demokrasia hapa nchini mwetu.
7.0 Watanzania Waishio Nje ya Nchi na Vitambulisho vya Uraia
Mheshimiwa Spika, zoezi la vitambulisho vya uraia limeanza hapa nchini mwetu kwa Watanzania kuanza kujiandikisha kwenye Jiji la Dar Es Salaam na kisha zoezi litaendela kwa nchi nzima ili kila mwenye umri wa miaka 18 aweze kujiandikisha na kupata kitambulisho cha uraia.
Mheshimiwa Spika, mpaka sasa taarifa zilizopo ni kuwa zoezi hili la vitambulisho litahusika moja kwa moja na haki ya kupiga kura, na mpaka sasa haujatangazwa utaratibu wowote ule wa wazi ni jinsi gani watanzania waishio nje ya nchi watakavyoweza kushiriki katika zoezi hili.
Kambi Rasmi ya Upinzani inataka kupata majibu Wizara imeweka utaratibu gani wa kuhakikisha kuwa Watanzania waishio nje ya nchi wanapata fursa ya kujiandikisha na kupata vitambulisho vya Taifa.
8.0 Masuala ya Kimataifa
Mheshimiwa Spika, kumekuwapo na changamoto nyingi mbalimbali kutokana na migogoro mbalimbali ya kimataifa ambayo imeendelea kuutikisa Ulimwengu kwa kipindi cha hivi karibuni, na migogoro hii imekuwa ikichochewa na Mataifa makubwa ya Magharibi.
Mheshimiwa Spika, kutokana na migogoro hii ya kimataifa Tanzania kwa sasa haijulikani iko upande gani kati ya wanaoonewa na wale wanaoonea kwani kwa miaka ya hivi karibuni tumekuwa na utamaduni wa kukaa kimya na kuachana na utamaduni wetu wa kusema na kuonyesha tuko upande gani.
Kambi Rasmi ya Upinzani inataka kujua nini msimamo wa Tanzania kuhusiana na migogoro kama ule wa Syria, Iran, Korea Kusini na Korea ya Kaskazini. Tuko upande upi hasa?
Mheshimiwa Spika, upo mgogoro baina yetu na nchi ya Malawi kuhusiana na umiliki wa Ziwa Nyasa na rasilimali zake na huu ni mgogoro wa muda mrefu ambao unatishia amani na usalama wa nchi yetu.
Kambi Rasmi ya Upinzani, inaamini kuwa serikali itatoa taarifa ya kina kuhusiana na mgogoro huu na hatua ambazo kama taifa tutachukua ili kuweza kuumaliza mgogoro huu.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani naomba kuwasilisha.
…………………….
Ezekia Dibogo Wenje(Mb)
Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
06.08.2012
0 comments:
Post a Comment