Tuesday, July 10, 2012

Kuhusu Migomo Sehemu Za Kazi


Hivi karibuni kumekuwepo na wimbi la kuitishwa migomo isiyozingatia
taratibu zilizowekwa kisheria.

Kwa mujibu wa kifungu cha 80(1) cha Sheria ya Ajira na Mahusiano
Kazini Na.6/2004 ili mgomo uwe halali ni budi mambo yafutayo
yazingatiwe:

    Ni lazima kuwepo na mgogoro wa maslahi baina ya wafanyakazi na
mwajiri.

    Mgogoro huo uwe umeishawasilishwa kwa kutumia fomu maalum katika
Tume ya Usuluhishi na Uamuzi.

    Mgogoro uwe haujapatiwa ufumbuzi baada ya siku thelathini (30)
kupita tangu ulipopokelewa na Tume au katika muda wa siku thelathini
za ziada zilizoongezwa na Tume.

    Mgogoro uwe haujapokelewa na Tume au katika muda wa siku
thelathini zilizoongezwa na Tume.

    Mgomo uwe umeitishwa na Chama cha Wafanyakazi na kura imepigwa kwa
mujibu wa Katiba ya Chama cha Wafanyakazi husika na wengi wa wanachama
wawe wanaunga mkono.

    Taarifa ya masaa arobaini na nane (48) itolewe kwa mwajiri
ikielezea nia ya wafanyakazi kugoma.

Hata hivyo kwa mujibu wa kifungu cha 76(1) cha sheria hiyo hiyo
wafanyakazi walio katika huduma muhimu hawaruhusiwi kugoma isipokuwa
tu baada ya kukidhi vigezo kadhaa vinavyosimamiwa na kamati ya huduma
muhimu.

Kupitia gazeti la Mwananchi la tarehe 09/07/2012 Chama cha Walimu
Tanzania Wilaya ya Geita kimeazimia kufanya mgomo usio na kikomo
kutokana na kile kilichodaiwa kuwa ni madai ya muda mrefu.

Tayari Chama cha Walimu Tanzania kimeishawasilisha mgogoro katika Tume
ya Usuluhishi na Uamuzi – Dar es Salaam wenye namba za usajili CMA/
DSM.ILA/369/12 na Tume inaendelea kuushughulikia.

Tunachukua fursa hii kuwataarifu wafanyakazi wote kuwa migomo ambayo
si halali inamadhara yake ikiwa ni pamoja na kuchukuliwa kwa hatua za
kinidhamu dhidi ya wahusika.

Mgomo uliozungumziwa kupitia gazeti la Mwananchi ni BATILI.  Hivyo
Serikali inawataka wahusika wote kutojihusisha na vitendo vya uvunjaji
wa sheria na badala yake Sheria na Kanuni zinazotawala mahusiano
sehemu za kazi ziheshimiwe na kuzingatiwa.

                     09/07/2012
S.H. Kinemela
KAMISHNA WA KAZI

0 comments:

Post a Comment