GORDON KALULUNGA. KWASABABU tunaishi katika jamii, lazima tuwe makini kuzungumzia pia uhalisia wa mambo yaliyopo katika jamii zetu kuliko kukalia kuzungumzia siasa kila mawio na machweo na hatimaye tukajikuta muda umetutupa mkono na hatimaye tukaanza kuilaumu Serikali inayokuwepo madarakani huku tukisahau kuwa hatukutimiza vema majukumu yetu tukiwa vijana. Nalisema jambo hilo kutokana na swali moja pana ambalo ni smtambuka na suala lenyewe si linguine bali ni uzee. Nikisema uzee naamini wengi wenu mnanielewa Mwalimu wenu mkuu, na katika kulifahamu hili tumeshuhudia wazee wengi wakilalamikia Serikali kuhusu pensheni yaani malipo ya uzeeni na kusema kuwa mafao wanayopewa ni kidogo mmno na baadhi kuelekeza hasira zao kwa Chama Cha Mapinduzi na Serikali yeke. Siwaungu mkono hata kidogo wale wote wanaoichukia Serikali na chama kilichounda Serikali kutokana na madai ya pensheni bali nasema hivi wanapaswa kujilaumu wenyewe maana wengi walikuwepo serikalini na walishiriki kupanga kiasi hiccho cha penshini kama kuwakomoa waliokuwa wakistaafu huku wakisahau kuwa nao umri ukifika watastaafu. Kulielezea hilo kwa undani ngoja nijitoe kidogo na hapa nitoe tafsiri ya neon uzee. Uzee na kuzeeka ni dhana inayoelezea hatua ya mwisho ya makuzi ya binadamu kuanzia utoto, ujana hadi kufika uzee ambapo hapa Tanzania mtu anaitwa mzee kutokana na ama umri mkubwa, majukumu aliyonayo na pia hadhi yake, kwa mfano mkuu mahali pa kazi au katika ukoo. Katika makala haya napenda kuelezea zaidi wazee tulionao aidha walikuwa wanafanya kazi za kuajiriwa au kujiajiri na wale walioko vijijini ambao kuzeeka kwao ni matokeo ya kupungukiwa nguvu za kufanya kazi. Katika nchi zilizoendelea kama Uingereza na Marekani, suala la uzee linahusishwa na umri wa kustaafu ambao ni miaka 60 - 65. Katika nchi nyingine umri wa kustaafu unatofautiana kijinsi, kwa mfano, nchini Latvia wanaume wanastaafu wakiwa na miaka 55 wakati wanawake wanastaafu wakiwa naumri wa miaka 60. Pamoja na ukweli kwamba watumishi walio katika Serikali na Taasisi zake wanastaafu wanapofikia miaka 60 na kwamba wazee wa vijijini na wale waliojiajiri wanakoma kufanya kazi kutokana na kuishiwa nguvu, ukweliunabaki kwamba binadamu mwenye umri wa miaka 60 anaonyesha dalili 2 dhahiri za kuishiwa nguvu. Sera ya Taifa ya Afya na sheria ya utumishi wa umma zinazingatia umri wa miaka 60 kuwa ni kigezo cha uzee. Kwa madhumuni ya sera iliyopo hapa nchini dhidi ya wazee, mzee ni mtu mwenye umri wa miaka 60 na kuendelea. Karne ya ishirini imeshuhudia ongezeko kubwa la idadi ya wazee ambapo Tanzania ni moja wapo na takwimu zinaonesha kuwa, Tanzania yenye kukadiriwa kuwa na jumla ya watu milioni 36,000,000 ina wazee wenye umri wa miaka 60 na zaidi wapatao milioni 1.4 (asilimia 4 ya watu wote). Aidha inaelezwa kwamba ifikapo mwaka 2050 idadi itaongezeka kufikia milioni 8.3 (asilimia 10 ya watu wote). Katika maisha ya kila siku ya jamii wazee wanakubalika kuwa ni watoaji wa habari, ujuzi na uzoefu. Katika maisha ya kijadi wazee na vijana waligawana majukumu, wazee walikuwa walinzi wa mila na desturi, washauri/wapatanishi, na walezi wa watotowadogo. Vijana wenye nguvu walikuwa na jukumu la kuwahudumia wazee hao kwa kuwapatia mahitaji ya msingi ya maisha ikiwa ni pamoja na malazi, mavazi na ulinzi. Wazee wa Tanzania wako katika makundi mbalimbali. Makundi hayo ni pamoja na Wazee Wastaafu, Wakulima, Wafugaji, Wavuvi na wale wasio na ajira. Kukua kwa miji na utandawazi uzee sio mhimili tegemezi katika maisha ya kila siku na hivyo kizazi cha sasa hakitegemei tena wazee kama mwongozo wa maisha katika jamii jambo ambalo linajidhihilisha baada ya vijana walio wengi wapo kuwa mbali na wazee na hawaonyeshi heshima kwa wazee na mara nyingi wanawadharau. Kiuchumi wazee ni miongoni mwa watu masikini zaidi katika jamii. Makundi mbalimbali ya wazee kama wakulima, wafugaji, wavuvi na wale wasiokuwa na ajira hawamo katika mfumo wowote rasmi au usio rasmi wa hifadhi ya jamii. Wazee wengi wastaafu walio katika mpango wa hifadhi ya jamii wanakumbwa na matatizo yanayotokana na kutotosheleza kwa mafao na urasimu wa kupata huduma. Wakati huo huo watu wengi huzeeka na kuwa na afya dhaifu kutokana na maisha na matunzo duni wakati wa ujana wao,lishe duni wakati wa utoto au kwa wanawake mimba za mara kwa mara na kazi ngumu huongeza kasi ya kuzeeka. Magonjwa ya muda mrefu/kuendelea ni jambo la kawaida kwawazee walio wengi. Pamoja na ukweli huo huduma za afya hazipatikani kwa urahisi kwa wazee walio wengi na mara nyingi huduma hizo ni ghali na watumishi wa afya wanaohudumia wazee hawaonyeshi mwamko na hawana mafunzo ya kutosha katika eneo hili la huduma. Kutokana na utamaduni na mazingira yetu, wanawake, watu wenye ulemavu na wazee wamekuwa hawapati fursa sawa ya kushiriki katika maamuzi mbalimbali yanayohusu maendeleo na ustawi wao. Kutokana na hali na mazingira ya wazee niliyoeleza hapo juu, upo umuhimu sasa wa kuwa na sera ya Taifa ya Wazee inayoweza kuwakwamua kikamilifu na si kinadhalia katika utoaji huduma na ushiriki wa wazee katika maisha ya kila siku. Wazee wa mkoa wa Mbeya kwa kushirikiana na mwongozo wa serikali wa sera ya wazee wameamua kuanzisha mwongozo wa elimu juu ya sera hiyo ili kuweza kujenga mahusiano kati ya wazee na viongozi wa serikali za mitaa. Umoja wa wazee hao unaojulikana kwa jina la Mbeya Older Persons Care (Mopec) umeanza kueneza sera hiyo ya wazee ili kujenga pia dhana nzima ya utawala bora wa kidemokrasia. Kati ya moja ya majukumu ya Mopec ni kuainisha majukumu ya serikali za mitaa ambayo ni kutekeleza miakakati ya kupambana na umasikini kwa kuwahamasisha wazee ama wananchi kufanya kazi kwa bidii na kujituma. Mikakati inayoendeshwa na kufafanuliwa na Mopec ni kuwajulisha wazee na wananchi wote kwa ujumla majukumu ya Serikali za mitaa, majukumu ya Afisa mtendaji wa Kijiji au mtaa,Afisa mtendaji wa kata, Mwenyekiti wa serikali ya kijiji au mtaa. Sanjari na hayo majukumu mengine yanayoenezwa sambamba na sera ya wazee ya taifa kwa wazee ni kujua majukumu ya Diwani, wajibu na haki nza wananchi kwa ujumla wakiwemo wazee na nafasi ya wananchi kuwadhibiti viongozi wanaoenenda kinyume na majukumu yao. Mmoja wa wanaharakati wa haki za wazee kutoka katika asasi ya kuwajali wazee Edmond Mpoto(61) anasema kuwa kwa sasa asasi yao imeanzisha mradi wa kueneza sera ya wazee ya mwaka 2003. Mpoto anasema kwamba mradi huo wa kuwajali wazee unalenga kutoa mafunzo kwa wazee kujishughulisha na kujua haki zao za msingi zilizoainishwa katika sera hiyi ya taifa ya wazee ya mwaka 2003. ''Lengo letu kuu ni kuibua na changamoto zinazowakabili wazee hasa vijijini na kuwaeleza haki zao ambazo hawazijui ingawa zimetolewa na serikali'' anasema mzee huyo. Sanjari na hayo Mpoto alieleza kuwa kati ya matatizo makubwea yanayowakabili wazee ni pamoja na Afya, Umasikini unaowasababisha wazee wengi kuwa wapweke hasa wanapokosa mahala pazuri pa kulala. ''Kwa mfano suala la uchumi ninalolizungumzia hapa ni kwamba uchumi unaosemwa na watu wa University ni tofauti na uchumi unaotakiwa kuwa na wazee bali wazee wanatakiwa kuwezeshwa kwa kuwaibulia miradi ya kilimo cha miti ya matunda nk'' alieleza Mwanaharakati huyo aliyesema kuwa anachukia sana anapoona mzee haenziwi. Pamoja na hayo alishauri pia kuwa umefika wakati kwa serikali kutunga mitaala ya shule za msingi na sekondari itakayohusu elimu ya uzee na kuzeeka. Kutokana na hayo yote ndiyo maana katika makala haya ninasema kuwa sera ya Taifa ya wazee inapaswa kuwa dira ya jamii katika kujiweka tayari kukabiliana na maisha wakati wa uzee na tusipolijua jambo hili kuwa ni la muhimu tabu zao zilizopo sasa, zitakuwa zetu. Mwandishi wa makala anapatikana 0754440749 ama kalulunga2006@yahoo.com. www.kalulunga.blogspot.com |
Unapokea Email hizi kwa sababu umejiunga na Jukwaa la 'Mabadiliko'.
Kuchangia mada tuma kwenye Email hii: mabadilikotanzania@googlegroups.com
Kujiondoa Tuma Email kwenda; mabadilikotanzania+unsubscribe@googlegroups.com
Utapokea Email ya kudhibitisha kujiondoa kwako.
This years motto: 'WALK THE TALK'
For more options, visit this group at:
http://groups.google.com/group/mabadilikotanzania?hl=en?hl=en
0 comments:
Post a Comment