Friday, June 22, 2012

SERIKALI YAFANYA MABADILIKO MAKUBWA YA WAKURUGENZI WA HALMASHAURI NCHINI‏

Na Masoud Masasi, Dodoma 
SERIKALI imefanya mabadiliko katika halmashauri hapa nchini kwa kuwateua wakurugenzi wapya 14 huku ikiwavua madaraka wengine nane ambao walionekana kushindwa kuwajibika ipasavyo katika halmashauri zao na kufanya ubadhirifu wa fedha za halmashauri zao. 

Pia katika mabadiliko hayo wakurugenzi kumi na moja wamepewa onyo kali huku wengine 22 wakihamishwa vituo vya kazi ambapo wakurugenzi watatu wakipumzishwa kufanya kazi katika halmashauri hizo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ubadhilifu wa fedha . 

Akitangaza mabadiliko hayo mbele ya waandishi wa habari jana mjini Dodoma Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(Tamisemi)Hawa Ghasia alisema mabadiliko hayo yanatokana na 
kuboresha nidhamu na utendaji wa kazi kwa wakurugenzi hao. 

''Wakurugenzi 14 wameteuliwa ili kuziba nafasi zilizoachwa wazi huku
 wakurugenzi nane wakivuliwa madaraka hayo na Waziri Mkuu wengine watatu wakipumzishwa kabisa ambapo wakurugenzi 22 wakihamishwa katika vituo vyao na kupelekwa sehemu nyingine" 

"Mabadiliko haya ni kuboresha utendaji wa kazi katika halmashauri zetu
 pamoja na kuongeza nidhamu na uwajibikaji wa kazi kwa wakurugenzi ambao walikuwa si waadilifu katika kutelekeza majukumu yao"alisema 
Ghasia. 

Waziri huyo aliwataja wakurugenzi wapya walioteuliwa kuwa ni Jenifer
 Omollo ambaye anakuwa mkurugenzi wa Mji wa Kibaha,Fidelica MyovelaMkurugenzi mtendaji Halmashauri ya Musoma na Khadija Maulid Makuwani ameteuliwa mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora. 

Aliwataja wengine kuwa ni Ibrahim Matovu ameteuliwa kuwa mkurugenzi
 halmashauri ya Muheza,Idd Mshili halmashauri ya Mtwara,Julius Madiga Mkurugenzi Halmashauri ya Manispaa yaMorogoro na Kiyungi Mohamedi Mkurugenzi mtendaji halmashauri ya Shinyanga. 

Wengini ni Lucas Mweri ameteuliwa Mkurugenzi mtendaji halmashauri ya
 Nanyumbu,Miriam Mmbaga halmashauri ya Kigoma,Mwamvua Mrindoko Mkurugenzi mtendaji Nachingwea,Pendo Malembeja Halmashauri ya Kwimba huku Pudenciana akiteuliwa mkurugenzi wa Ulanga.



Ruben Mfume Halmashauri ya Ruangwa na Tatu Selemani amekuwa mkurugenzi mtendaji halmashauri ya wilaya ya Kibaha ambapo waziri Ghasia alisema uteuzi huo ulifanyika april 24 mwaka huu. 

Waziri huyo alisema wakurugenzi waliovuliwa madaraka kutokana na
 makosa mbalimbali katika Halmashauri zao kuwa ni Consolata Kamuhabwa(Karagwe),Ephraim Kalimalwendo(Kilosa),Elly Jesse 
Mlaki(Babati),Eustach Temu(Muheza),Jacob Kayange(Ngorongoro),Hamida Kikwega. (Chato),Majuto Mbuguyu(Tanga) na Raphael Mbunda halmashauri ya Manispaa ya Arusha. 

Waziri Ghasia aliwataja wakurugenzi ambao wamepewa onyo kali kuwa ni
 Judetatheus Mboya(Newala),Lameck Masembejo(Masasi),Abdallah Njovu(Tandahimba),Jane Mutagurwa(Shinyanga),Silvia Siriwa(Sumbawanga),Kelvin Makonda(Bukombe),Alfred Luanda(Ulanga),Fanuel Senge(Tabora),Maurice Sapanjo(Chunya),na Beatrice Msomisi halmashauri ya Wilaya ya Bahi. 

Pia waziri huyo alibainisha kuwa katika mabadiliko hayo wakurugenzi
 watatu ambao ni Xavier Tiweselekwa wa halmashauri ya Wilaya ya Misungwi,Erica Mussica kutoka halmashauri ya Sengerema na Theonas 
Nyamhanga wamepumzishwa kufanya kazi katika halmashauri hizo. 

"Maamuzi haya yalifanyika katika kipindi cha mwaka 2011/12 na hawa waliopewa onyo walitendeka makosa yao katika halmashauri zao hivyo pia wakurugenzi 22 wamehamishwa katika vituo vyao vya kazi na kupangiwa sehemu nyingine ili waweze kuimarisha utendaji kazi wao"alisema. 

Alisema tayari wakurugenzi wanne waliotuhumiwa katika ubadhilifu mbalimbali katika halmashauri zao wameshafikishwa mahakamani huku wengine wakiendelea kufanyiwa uchunguzi ambapo amesema wakibainika watapelekwa mahakamani pia. 

Alisema wale ambao walionekana hawakuhusika katika ubadhilifu katika
 vituo vyao vya kazi walipangiwa kazi nyingine huku wale walionekana utendaji wao sio mzuri walipumzishwa kabisa. 

Waziri huyo pia aliwataka wakurugenzi wapya walioteuliwa na wale wa zamani kuhakikisha wanafanya kazi kwa uhadilifu ili kuweza kuendelea kuboresha utendaji wa kazi katika mamlaka za serikali za mitaa nchini. 

Hata hivyo alisema hataweza kumchukulia hatua yoyote mkurugenzi kwa kusikia taarifa za mitaani na kuwataka wale wenye malalamiko kupeleka ushahidi kwake ambapo atafanya uchunguzi kabla ya mhusika kuchukuliwa hatua za kisheria. 

''Tukisema tuanze kuchukuwa hatua kwa kusikia taarifa za mitaani basi
 tutajikuta tukifukuza wakurugenzi wote kinachotakiwa ni kuwa na ushahidi uletwe na utafanyiwa kazi na hatua zitachukuliwa kwa Yule 
atakayebainika"alisema waziri Ghasia.


0 comments:

Post a Comment