Mbunge wa CHADEMA anusurika kukatwa mapanga
• Polisi wakwepa kukamata diwani wa CCM
Na Waandishi wetu, Iringa
MBUNGE wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa, amenusurika kucharangwa mapanga, baada ya kundi la vijana wanaoaminika kuwa wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kumvamia baada ya kukerwa na hatua ya kuhama kwa karibu uongozi mzima wa chama hicho Kata ya Nduli.
Kundi hilo lilimvamia Msigwa alipokuwa akijiandaa kuondoka akiwa na viongozi wanane waliokuwa wa CCM wa kata hiyo, ambao walihamia CHADEMA jana, ambapo walianza kuwashambulia watu walioandamana naye na kuwajeruhi vibaya kwa mapanga watu wawili, kiasi cha kulazimika kukimbizwa hospitalini kwa matibabu.
Polisi ambao walipigiwa simu mara baada kuanza kwa vurugu hizo, hawakuweza kujitokeza, hali iliyozusha taharuki kubwa kutoka kwa wananchi waliolazimika kukimbia ovyo ili kuokoa maisha yao. Vijana wanaodaiwa kuumizwa vibaya zaidi ni Oscar Sanga na Seleman Komba, ambao walikuwa miongoni mwa wananchi waliohudhuria mkutano huo.
Taarifa za awali zimedai kuwa kundi hilo la vijana lilitumwa na mmoja wa viongozi wa ngazi ya juu wa chama hicho, kwa madai ya kukasirishwa na hatua ya kuhama kwa mwenyekiti, katibu na wajumbe sita wa CCM Kata ya Nduli, ambao waliwaongoza zaidi ya wanachama 90 kukihama chama hicho na kujiunga na CHADEMA.
Mchungaji Msigwa ambaye aliandamana na Diwani wa Kata ya Mivinjeni, Frank Nyalusi (CHADEMA), alifanya mkutano huo akilenga kuwataka wananchi wawe jasiri wa kutambua haki zao na kudai maelezo sahihi ya matumizi ya fedha za miradi ya maendeleo inayotolewa na serikali katika ngazi za kata na vijiji.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Evarist Mangalla, hakuweza kupatikana mara moja kuzungumzia vurugu hizo, lakini mmoja wa maofisa wa jeshi hilo alidai hawana taarifa na kwamba watazifuatilia kwa makini kujua kilichotokea na kuahidi kuchukua hatua za kisheria kwa waliohusika na vurugu hizo.
Wakizungumza mara baada ya kujiunga na CHADEMA, aliyekuwa mwenyekiti wa CCM wa kata hiyo, Ayub Mwenda na katibu wake, Godwin Sanga, walisema kuwa wao na viongozi wameamua kukihama chama hicho, baada ya kugundua kuwa kimejaa viongozi wasiokuwa wakweli na wasiojali maendeleo ya wananchi waliowapigia kura.
Mwenda pamoja na aliyekuwa mjumbe wa kata hiyo, Temina Ndete, walidai kuwa kwa muda mrefu wamejitahidi sana kupigania haki za wanyonge, lakini hawakuweza kufua dafu kwa sababu uongozi wa juu wa CCM umewatupa na kujali masilahi ya wachache.
Uteuzi wa Mbatia wamkimbiza kigogo
Wakati huo huo, wimbi la wanachama wa vyama vya siasa kutimkia CHADEMA linazidi kushika kasi baada ya aliyekuwa mgombea ubunge wa Jimbo la Buyungu (NCCR-Mageuzi), mkoani Kigoma, Mawazo Metusela, kujivua uanachama.
Metusela (28), alitangaza uamuzi huo jana jijini Dar es Salaam, akidai kuwa sababu kubwa iliyomsukuma kujiondoa kwenye chama hicho ni kutokana na hatua ya Mwenyekiti wao, James Mbatia, hivi karibuni kukubali uteuzi wa Rais Jakaya Kikwete wa kuwa mbunge.
Alisema kuwa alithibitisha tuhuma za muda mrefu kuwa NCCR-Mageuzi ni tawi la CCM baada ya uteuzi huo wa Mbatia kuonekana kushangiliwa na kuungwa mkono na viongozi wenzake.
Katika uchaguzi mkuu wa 2010, Metusela alikabana koo na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Injinia Christopher Chiza, akiwa amejizolea kura 11,514 dhidi ya 17,040 za mpinzani wake.
"Mimi wakati huo nilikuwa mwanafunzi katika Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) na kimsingi nilishinda uchaguzi huo, ila sema Tume ya Uchaguzi ilinipora ushindi wangu na wananchi walinitaka nifungue kesi kupinga matokeo," alisema.
Alisema kuwa alipokwenda kuomba msaada kwenye chama wa kufungua kesi, Mbatia alimshawishi aachane na uamuzi huo, akidai Chiza alikuwa ni naibu waziri pekee kutoka mkoani Kigoma, hivyo amwache aendelee na majukumu yake.
Metusela aliongeza kuwa wananchi wa Buyungu walijitahidi kumchangia fedha afungue kesi hiyo, lakini fedha hazikutosha, hivyo baada ya siku 14 Mahakama Kuu Kanda ya Tabora iliifuta.
"Kwa mazingira hayo, wananchi wa Buyungu wamepoteza imani na NCCR-Mageuzi, hiki si chama cha upinzani tena bali ni kibaraka wa CCM. Mimi sasa nimechukua uamuzi wa kujiondoa kabla hatujaanza kuzomewa," alisema.
Alipoulizwa ni chama gani atajiunga nacho, mwanasiasa huyo alisema kwa sasa anatafakari kwanza wakati akiangalia chama makini chenye upinznai wa kweli cha kujiunga nacho.
Chanzo: Tanzania Daima.
0 comments:
Post a Comment