Saturday, April 21, 2012

Waziri aingizia Serikali deni la Sh15 bilioni

Waziri aingizia Serikali deni la Sh15 bilioni
Apr 20th 2012, 17:34

Joseph Zablon
MZIMU wa mikataba mibovu inayoigharimu Serikali mabilioni ya fedha, unaendelea kulitafuna taifa baada ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kupitia Wizara ya Uchukuzi kudaiwa Dola 10 milioni za Marekani (takriban Sh15 bilioni) kutokana na kuvunja mkataba.

TPA kupitia Wizara ya Uchukuzi, imejikuta matatani baada ya kuvunja mkataba wa ujenzi wa jengo la kisasa la kuhifadhi magari katika Bandari ya Dar es Salaam, lililokuwa lijengwe na Kampuni ya MJ Group Co. Ltd ya Mombasa nchini Kenya.

Chanzo chetu cha habari kutoka ndani ya Wizara ya Uchukuzi, kilidokeza kuwa jengo hilo la kisasa la ghorofa 10, lilipangwa kujengwa ndani ya eneo la Bandari ya Dar es Salaam likiwa na uwezo wa kuhifadhi magari 8,000 kwa wakati mmoja, lengo likiwa ni kupunguza msongamano mkubwa wa magari bandarini.

Hata hivyo, mradi huo ulishindwa kuendelea baada ya agizo kutoka kwa Waziri mwenye dhamana na uchukuzi Mhandisi Omar Nundu la kuusitisha.Chanzo hicho kilisema hatua ya kusitishwa kwa mradi huo, ilichukuliwa na Nundu, katika barua yake aliyomwandikia Mwenyekiti wa Bodi ya TPA, Raphael Mollel.

Katika barua hiyo kumb. Na CCB 52/364/01 ya Januari 21, 2011 ambayo Mwananchi imefanikiwa kuiona, Nundu alimtaka mwenyekiti huyo kupitia mradi huo na kumpa maoni yake na atakaporidhika, amwagize Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo kusitisha mara moja azma ya ujenzi wa jengo hilo na kumweleza mwekezaji aliyemchagua pamoja na kumpa sababu za usitishaji huo.

Mbali na hilo,Nundu aliweka wazi kuwa alishamwagiza Mkurugenzi Mkuu wa TPA kusitisha hatua iliyofikiwa na mwekezaji bila ya kutakiwa kulipa fidia zisizoendana na makubaliano bali, kama ingebidi kufidia chochote, Serikali itakuwa tayari hata iwe Sh4 bilioni ili mradi huo usitishwe.

Kufuatia agizo hilo la waziri, mwenyekiti huyo wa bodi, katika barua yenye kumb. DG/3/3/06 ya Januari 27, 2011 alimwandikia Mkurugenzi Mkuu wa TPA kuhusu kusitisha mradi huo.

Sehemu ya barua ya Mwenyekiti huyo inasomeka; " Katika Kikao Maalum cha 31 cha Bodi ya Wakurugenzi kilichofanyika jana , (Januari 26, 2011), Bodi ilijadili utekelezaji wa maagizo ya Omari Nundu (MB), Waziri wa Uchukuzi kuhusu mradi wa "Mult Storey Car park" kama yalivyo kwenye barua ya CCB 52/364/01 ya tarehe 21 Januari ambayo iliandikwa kwako."

"Bodi imezingatia maelezo yaliyotolewa na Waziri ya kusitisha utekelezaji wa mradi huo. Kwa barua hii nakuomba usitishe mara moja utekelezaji wa mradi huu."

Kutokana na agizo hilo, mkurugenzi huyo wa TPA, aliwaandikia barua MJ Group yenye kumb. No.DG/3/3/06, Januari 27 kutengua barua ya TPA ya Desemba 13, 2010 iliyoipa kampuni hiyo tuzo huku akieleza kuwa suala hilo limetokana na sababu zisizoweza kuzuilika.

Uongozi TPA
Mkurugenzi wa TPA, Ephraim Mgawe akizungumza kupitia kwa Mwanasheria Msaidizi wa mamlaka hiyo, Koku Kazaura alikiri ofisi yake kupokea hati ya Mahakama inayowataka kumlipa fidia mwekezaji huyo, MJ Group na kueleza kwamba wanaijadili kwanza.

"Ni kweli tumepokea hati hiyo ya Mahakama ambayo inatutaka tulipe fidia hiyo ndani ya siku 14 na tumezipokea nyaraka hizo za Mahakama tokea Aprili 16, mwaka huu" alisema mwanasheria huyo na kuongeza kuwa wanatakiwa kutekeleza agizo hilo ndani ya siku 14.

Waziri Nundu
Waziri wa Uchukuzi Omary Nundu Jumanne iliyopita alipoulizwa kuhusu suala hilo alikataa kusema lolote. Awali, alipigiwa simu yake ya mkononi bila ya kupokea na alipotumiwa ujumbe na kuelezwa juu ya suala hilo ilia toe ufafanuzi alijibu kwa ujumbe wa simu unaosomeka; "Naona umeamua kunichafulia ushiriki wangu bungeni leo asante sana."

Alipotafutwa kwenye Viwanja vya Bunge, Dodoma siku hiyohiyo alisema: "Siwezi kuzungumza na mtu (Mwandishi) wa Mwananchi maana mmenisumbua kwa kunipigia simu hovyo wakati niko kwenye uchaguzi. Ondoa upuuzi hapa siwezi kukuambia chochote nyie wasumbufu!"

Naibu Waziri wa Uchukuzi, Athuman Mfutakamba alikiri kuwapo kwa mgogoro huo lakini akasema yeye si msemaji wa wizara. "Ndiyo kuna mgogoro lakini hakuna msemaji zaidi ya Katibu Mkuu wa Wizara," alisema.

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Omari Chambo hakupatikana kuzungumzia sakata hilo kutokana na kila anapopokea simu kueleza kuwa yuko mkutanoni. alijibu hivyo mara kadhaa kwa siku tatu mfululizo

Chanzo: Mwananchi


0 comments:

Post a Comment