Na Renatus Masuguliko
6th April 2012
Hali ni tete katika mji wa Geita baada ya walinzi watatu wa Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) kucharangwa kwa mapanga na gari la kampuni hiyo kuteketezwa kwa moto katika mapambano baina ya polisi na kundi la wananchi wanaoishi jirani na mgodi huo.Tukio hilo lilitokea jana, baada ya wananchi hao kuvamia kwa nguvu mgodini huo na kuingia hadi kwenye kiwanda cha kuzalishia dhahabu kuchukua mawe yanayodhaniwa kuwa na dhahabu.Wananchi hao ambao ni wachimbaji wadogo wakiwa na silaha za jadi walianza kwa kuandamana kwenda ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Geita kupinga wenzao wawili kujeruhiwa na walinzi wa mgodi huo kwa kupigwa risasi za moto miguuni kwenye vurugu zilizotokea juzi.Mapambano hayo yalianza tangu Jumanne wiki hii kati ya walinzi na wananchi hao, ambapo hata hivyo, polisi wilaya ya Geita walilazimika kuzizima kwa kuwatawanya wananchi hao eneo la mgodi kwa mabomu ya mchozi.
Vurugu hizo jana zilichukua sura nyingine saa 4 :00 asubuhi na polisi kulazimika kufyatua risasi za moto hewani na mabomu ya machozi kuwazuia wananchi hao kuandamana kwenda kwa Mkuu wa Wilaya ya Geita, Philemon Shelutete, huku waandamanaji hao wakiwazuia wafanyakazi na magari ya mgodi kuonekana eneo la mjini.Hali ilizidi kubadilika, baada ya wananchi hao kuvamia mji mzima wa Geita na kuanza msako wa nyumba hadi nyumba za wafanyakazi wa mgodi na kuteketeza kwa moto gari moja la mgodi lenye namba T 577 AQR na namba za ubavuni LV 256 aina ya Toyota Land Cruser lililokutwa limepakiwa nyumbani kwa dereva wa gari hilo Disman Mselabuye.
Hata hivyo, moto huo ulizimwa na polisi waliofika eneo la tukio kabla ya kuwatawanya wananchi hao kwa kufyatua risasi za moto zaidi ya 60 hewani pamoja na mabomu ya machozi, ambapo watu watano waliathirika na mabomu hayo huku gari la polisi namba GP 197 LJQ likinusurika kuteketezwa kwa moto.Katika maandamano hayo yaliyoanzia mjini Geita, wananchi walisikika wakiimba nyimbo za kumkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Geita Said Magalula, akabiliane na matatizo ya siku nyingi ya wana Geita.
"Tunakukaribisha Mkuu wa Mkoa wa Geita na hii ndiyo Geita yetu ya matatizo kibao,'' zilisikika baadhi ya sauti.Kamanda wa Polisi Wilaya ya Geita, Paulo Kasabago, amethibitisha kutokea tukio hilo na kusema wananchi wawili walijeruhiwa vibaya baada ya kupigwa risasi za moto sehemu za miguuni na walinzi wanne wa mgodi huo wamejeruhiwa baada ya kucharangwa kwa mapanga sehemu mbalimbali za miili yao.
Alisema majeruhi wote wamelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Geita kwa matibabu huku hali za wananchi waliopigwa na walinzi kwa risasi za moto zikielezwa kuwa ni mbaya kutokana na kuumia vibaya miguu yao.
"Vurugu zilianza tangu Jumanne…taarifa tulipata tukaenda kuwazuia wananchi hao, lakini leo (jana) waliingia tena mgodini majira ya saa 11 alfajiri na baada ya kuondolewa na walinzi waliandamana kwenda kwa DC na ndipo vurugu zilizidi,'' alisema na kuongeza:
"Walianza kuzuia na kuharibu magari ya mgodini na moja wamelichoma moto, amani imetoweka kwani hawataki kuona mfanyakazi wa mgodi hapa mjini wala gari, tunaendelea kuwazuia madhara yasitokee zaidi."
Hata hivyo, Kamanda Kasabago, alisema watu watano wanashikiliwa na polisi na kwamba uchunguzi bado unaendelea kubaini chanzo cha vurugu hizo.Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow, alipotafutwa jana jioni, simu yake ilikuwa inaita bila majibu.
Shelutete, alipotafutwa na NIPASHE ofisini kwake kuzungumzia tukio hilo hakupatikana na alipopigiwa simu yake ya mkononi alisema hana uhakika kama vurugu hizo zipo ingawa alikiri kuwa na tetesi za tukio hilo.
Jitihada za kuupata uongozi wa GGM kuzungumzia tukio hilo hazikuzaa matunda baada ya Afisa Uhusiano Jamii, Joseph Mangirima, kutopatikana alipopigiwa simu.Wananchi hao walipohojiwa na NIPASHE, walisema chanzo cha kuingia mgodini kwa nguvu ni kutokana na njaa zinazowakabili baada ya serikali wilayani humo kulifunga eneo la Katoma la wachimbaji wadogo na kuchukuliwa na kampuni ya mgodi huo.Walisema kutokana na serikali kuzuia shughuli za uchimbaji katika eneo hilo wamekosa hata mahitaji wa kutunza familia zao na kusomesha watoto.
Serikali wilayani Geita mwanzoni mwa mwaka huu iliwataka wananchi wanaojishughulisha na uchimbaji wa madini katika eneo la Katoma jirani na mgodi wa GGM kusitisha kuendesha uchimbaji wa dhahabu eneo hilo.
Source: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment