GAZETI la Mwananchi linalochapwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL), juzi liligeuka bidhaa adimu mjini Dodoma baada ya watu wasiojulikana, kulihujumu na kununua nakala zote. Haijafahamika hasa sababu za mtu au watu hao kukusanya nakala zote za gazeti hilo na kuziondoa katika mzunguko, lakini taarifa zinadai lilikuwa na habari ambazo zilikuwa zikitishia masilahi yao. Katika ukurasa wa kwanza kulikuwapo na habari tatu kubwa; moja ikihusu kushamiri kwa vitendo vya rushwa katika uchaguzi wa wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki uliomalizika juzi usiku. Licha ya habari hiyo, kulikuwapo na habari iliyomhusu Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkullo, kuhusishwa na kashfa ya uuzaji wa kiwanja kimoja kilichopo Barabara ya Nyerere, Dar es Salaam. Habari hizo mbili ndizo ambazo zinahisiwa zilisababisha watu hao kununua magazeti hayo, wakihisi ama zingevuruga harakati zao za uchaguzi au zingewafunua wabunge kuhusu kashfa hiyo ya kiwanja. Waandishi wa habari wa Mwananchi waliokuwapo katika viwanja vya Bunge walikuwa na wakati mgumu kujibu maswali ya wabunge waliotaka kufahamu sababu ya kutokuwapo kwa gazeti hilo mjini hapa. Mbunge wa Vunjo, Augustine Mrema, alihoji sababu ya mtu mmoja kuwanyima Watanzania wote walioko Dodoma fursa ya kupata habari kutokana na hofu anayoijua mwenyewe. "Mimi kila nikiuliza naambiwa kuna watu wamelinunua gazeti lote wamekwenda kulichoma, nikawauliza kwani limeandika nini kibaya dhidi yao? Lakini hawanijibu!"alisema Mrema. Habari zisizo rasmi zilidai kuwa magazeti hayo yalinunuliwa na mawakala wa kigogo mmoja ambaye anahusishwa na uuzaji au ununuzi wa kiwanja hicho kilichopo Barabara ya Nyerere. Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali, ukusanyaji wa gazeti hilo ulianzia eneo la usambazaji katikati ya mji na kila muuza magazeti aliyekuwa akiuziwa alikuwa akidakwa na kutakiwa kuyauza. |
Thursday, April 19, 2012
Gazeti la Mwananchi lahujumiwa Dodoma
By Gemmstore at 4:06 PM
No comments
0 comments:
Post a Comment