Monday, June 1, 2015

TAHADHARI TOKA UTUMISHI - 6/1/2015

Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma Bwana Xavier Daudi anapenda kutoa tahadhari kwa waombaji kazi wote hususan wale waliofanya usaili ofisi za Sekretarieti ya ajira kuanzia tarehe 18 hadi 29 mei,2015 kuwa Ofisi yake imepata malalamiko kutoka kwa baadhi ya watu waliofanya usaili  ambao wamedai  kupigiwa simu au kutumiwa ujumbe mfupi  na mtu anayejitambulisha kama afisa wa Sekretarieti ya ajira ambaye anaomba Rushwa ili kuwapangia vituo vya kazi wasailiwa.

Kwa mujibu wa malalamiko hayo mtu huyo ambaye anatumia namba za simu 0752152876 na 0673525271 kuwapigia na kuwatumia ujumbe baadhi ya watu waliofanya usaili tarehe 20 Mei, 2015  uliowahusisha Maafisa Watendaji kata daraja la II ambapo anawapigia simu ya kuwapongeza na kuomba kiasi cha Shilingi 50000 kabla ya tarehe 29 Mei, 2015 ili kupangiwa kazi.

Kwa taarifa hii katibu wa Sekretarieti ya Ajira anawafahamisha wadau wote kuwa Ofisi yake haina utaratibu wa kuomba fedha kwa mtu yeyote kama sharti la kuajiriwa katika utumishi wa umma, hivyo waombaji kazi wote waliofanya  na wanaoendelea kufanya usaili waepukane na Matapeli wa aina hiyo ambao hawana nia njema.

Ameongeza kuwa uendeshaji wa mchakato wa ajira katika Utumishi wa Umma unaendeshwa kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu kuanzia hatua ya kutangaza kazi, kupokea na kuchambua maombi ya kazi, kuandaa orodha ya waombaji kazi wanaoitwa kwenye usaili, kufanya usaili na hatimae kupangiwa vituo vya kazi kwa wasailiwa wanaofaulu usaili ambapo matangazo yote hutolewa kupitia tovuti ya Sekretariet ya Ajira.

Aidha, kwa wale wote ambao watapigiwa au kutumiwa ujumbe mfupi wa kuombwa Rushwa na matapeli kama sharti la kupangiwa kazi wawasilishe namba hizo za wahusika katika mamlaka zinazohusika  kwa hatua zaidi za kisheria.
 Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Ofisi ya Rais Sekretarieti ya Ajira katka Utumishi wa Umma.

0 comments:

Post a Comment