Meneja Uhusiano wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), Bw. Amini Mbaga (kulia) akijadiliana swala na Mwenyekiti wa kituo cha watoto cha Mama wa Huruma, Mtawa Berna Mdendemi mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam. TTCL ilitoa msaada wa mifuko 70 ya sementi kuwezesha kituo hicho kuwa na majengo yake.
Meneja Uhusiano wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), Bw. Amini Mbaga (kushoto) akiwasalimia watoto wa kituo cha Mama wa Huruma mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam. TTCL ilitoa msaada wa mifuko 70 ya sementi kuwezesha kituo hicho kuwa na majengo yake.
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Watu binafsi na taasisi mbalimbali nchini zimetakiwa kuendelea kusaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu ili kuwaendeleza ili hatimaye waje kuwa na mchango kwa taifa. Wito huo umetolewa na Meneja Uhusiano wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), Bw. Amini Mbaga alipokuwa akikabidhi msaada wa saruji wa mifuko 70 kwa ajili ya kukisaidia kituo cha kituo cha Mama wa Huruma kuwa na majengo yake.
Bw. Mbaga aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki kuwa kampuni yao imetoa saruji hiyo kwa kituo hicho ili watoto waweze kukuzwa katika mazingira bora na yenye heshima zaidi.
"Pamoja na kutoa huduma ya mawasiliano kwa jamii pia huwa tunashiriki katika maswala ya kusajidia jamii,"alisema, huku akitoa changamoto kwa wadau wengine kuiga mfano huo. Kituo hicho kilianzishwa na watawa wa Kanisa Katoliki na kinahudumia watoto hao mahitaji ya elimu, chakula na malazi ili waweze kuja kuwa raia wema hapo baadaye.
"Watoto hawa wakiachwa wanazagaa mitaani bila ya huduma yoyote ni hatari kwa maisha yao na taifa...tuwasaidie kwa faida yao na nchi kwa ujumla," alisema. Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kituo hicho Mtawa Berna Mdendemi alisema kituo hicho kinawatoto 70 ambao hawana wazazi, watoto wa mitaani na wale wanaoishi mazingira magumu.
"Tuligundua kuwa watoto wengi katika maeneo haya walikuwa wanazagaa na hivyo tukaguswa na kuamua kuanzisha kituo hiki,"alisema. Watoto hao wanasaidiwa kupata elimu ya awali, msingi, elimu ya stadi za maisha pamoja na malazi, chakula, na huduma za afya.
Mipango ya badaye ni kujenga shule ya sekondari na maarifa ya nyumbani ili kusaidia kuwakomboa watoto hao na kuwa na taifa lenye vijana wanaojiweza. "Tunaishukuru kampuni ya TTCL kwa msaada wao ambao utatusaidia sana katika ujenzi huu ambao tumeuanza kwa kiasi fulani,"alisema.
Aliomba watu na taasisi mbalimbali kuendelea kukisaidia kituo hicho ili kiweze kufikia malengo yake. Kituo hicho kilicho katika eneo la Madale kilianza mwaka 2010.
0 comments:
Post a Comment