Saturday, August 24, 2013

UNAJUA NI KWA SABABU GANI AFANDE SELE ALIGOMA KUHAMA MORO NA KUHAMIA DAR? BASI SOMA HAPA ALICHOKISEMA




UNAJUA NI KWA SABABU GANI AFANDE SELE ALIGOMA KUHAMA MORO NA KUHAMIA DAR? BASI SOMA HAPA ALICHOKISEMA
https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEhpwGTLTdhm_O1zvDOhofPDq8FQJ7D6favBXhJ9FKe0T1fqD29LV4P9pIqS6pmvtbUnlqxhzUddfa-8wFH2AYydnKqxXJFQe7f5wIdux7KyVmrY01Lu_uAJMMoTpzXxgKm5eihrnZUCl-yS/s320/%253D%253Futf-8%253FB%253FQUZBTkRFIFNFTEUgQU5EIEhFUiBEQVVHSFRFUiBUVU5EQS5qcGc%253D%253F%253D-735278Sifa kubwa ya wasanii wa muziki wa kizazi kipya ni pamoja na kutaka kukaa katika majiji makubwa, pengine kwa kupenda kufanya kazi sehemu ambayo ina kila kitu, kwa maana ya studio nzuri na zenye vifaa bora na mambo kama hayo.
Hata hivyo, hicho kinapingwa na mkali wa muziki wa hip hop kwenye anga ya muziki wa kizazi kipya hapa nchini mwenye majina ya kisanii lukuki, Mfalme wa Rhymes, Simba Mzee, Afande Sele au Baba Tunda, hapa namzungumzia Selemani Msindi, ambaye alifanya mazungumzo na Starehe akielezea sababu zinazomfanya asihame Morogoro.
Starehe: Mambo vipi Baba Tunda?
Afande Sele: Kicheko, mambo safi wanasemaje Mwananchi?
 Starehe: Hawajambo, mbona umecheka?
Afande Sele: Nimefurahi kuniita Baba Tunda, kwani napenda kuitwa hivyo ingawa watu wengi wananiita Afande Sele, jina la kazi.
Starehe: Tuachane na hayo, wasanii wengi wanafanya kazi zao katika majiji makubwa kama Dar, Arusha na mengineyo, lakini wewe bado upo Moro licha ya kuwa katika tasnia hii kwa muda mrefu.
Afande Sele: Duh, sina mpango wa kuhama Moro kwa jinsi yoyote ile kwa kuwa huku ni nyumbani na mimi najivunia kufanya kazi nyumbani.
Starehe: Huoni kama unapata shida kufanya kazi nje ya jiji hasa Dar ambako kila kitu kinapatikana tofauti na huko Moro.
Afande Sele: Ni kweli siku za nyuma nilikuwa napata tabu kufanya muziki au video kwa kuwa hakukuwa na studio nzuri, lakini siku hizi zipo tena nzuri na zinakidhi haja, hivyo sioni sababu ya kuhama huku, pili mimi ni msanii mkubwa, kukaa kwangu huku kunawavutia vijana kufanya kazi na wale wanaotaka ushauri wanakuja kuniuliza, huu ni mpango wangu wa kuhakikisha kila kijana anayetaka kufanya muziki hakati tamaa, nitampa ushauri wa kikazi, kubaki au kuondoka baada ya kufanikiwa ni juu yake.
Starehe: Kwa hiyo huji Dar kabisa?
Afande Sele: Siyo kama siji na siyo Dar bali naenda mikoa mbalimbali kufanya kazi, lakini Dar ndiyo naenda sana hata kwa mwezi mara nne kutokana na shoo nyingi kuwa huko.

Starehe: Huoni kama ni gharama, nenda rudi za kila mara?
Afande Sele: Gharama siyo kubwa kulingana na ninachokifuata mara nyingi inakuwa ni kufanya shoo pamoja na matangazo kwa kuwa huku bado hakuna redio nyingi zinazofika mbali kama Dar, sijutii kwa kuwa nimeamua mwenyewe kuishi huku.
Starehe: Mazingira ya maisha yana tofauti gani kati ya Dar ambako unaenda kwa ajili ya kazi na matangazo na Moro ambako unaishi?
Afande Sele: Tofauti ni kubwa kwani Moro kumetulia na hivi ninavyokwambia ni lazima mchana kama sina kazi ninapata muda wa kupumzika japo kwa saa mbili kitu ambacho kwa Dar ni kigumu sana, kuna pilika nyingi, foleni ndiyo usiseme, kwa kweli siwezi kuishi Dar.
Starehe: Mara nyingi nimekuwa nikikusikia ukilalamikia suala la starehe au hilo ndiyo linakufanya uogope kuishi huko?
Afande Sele: Haswaa, Dar kunaongeza matumizi, kwa kipato changu nikiishi huko nitapata tabu, kwa kuwa wasanii karibu wote wanakutana katika nyumba ya starehe kitu ambacho kinahitaji fedha, ni wachache sana ambao wanakubali kushindwa kwa kukaa nyumbani baada ya shoo, sasa kwa kuwa napenda kujichanganya na kubadilishana mawazo na wenzangu sintoweza kukaa nyumbani nitakwenda nao viwanjani hayo ndiyo mambo nisiyoyataka.
Ninaamini vijana wengi wanashindwa kufikia malengo yao kutokana na kuendekeza anasa zinazopatikana huko, bila kujali wapo na wasanii gani, kuna wengine wakubwa na wanapata fedha nyingi sasa bila kujua wengine wanajiingiza katika matumizi na kujikuta wakiishia kuvaa na kufanya starehe tu.
Starehe: Ni shoo zipi zinazokufanya usafiri katika mikoa mbalimbali?
Afande Sele: Nafanya shoo za matamasha  za kuhamasisha na zile ninazoalikwa na kampuni mbalimbali.
Starehe: Katika hizo shoo zipi zinakulipa fedha nyingi?
Afande Sele: Duh! za kampuni kwa kweli ndiyo zinanilipa fedha nyingi, sikosi milioni mbili au tatu kwa mwezi, kulingana na mwezi wenyewe unakuwa na shoo nyingi kiasi gani.
Starehe: Umesema kuna shoo za kuhamasisha, nazo unakusanya kiasi gani kwa mwezi?

Afande Sele: Hizo mara nyingi zinakuwa vijijini na zinaweza kuwa ni za kuhamasisha masuala ya kijamii au za burudani, ambapo huwa ni kama najitolea kwa kupewa fedha kidogo ya kula ikiwa ni katika kutimiza mpango wangu wa kuhamasisha vijana kujiajiri kwa kufanya muziki na hapa napenda niwapongeze mapromota wote wanaoandaa shoo za nje ya mji kwani muziki wetu unasikika hadi huko, lakini mashabiki wetu hawapati nafasi ya kutuona 'laivu'.
 SOURCE : MWANANCHI



0 comments:

Post a Comment