Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo akizungumza na Ujumbe kutoka Shirikisho la Makampuni makubwa ya Wafanyabiashara kutoka Singapore, walipomtembelea ofisini kwake jijini Dar es Salaam leo.
Na Veronica Simba
Tanzania imealikwa kushiriki katika Kongamano la kimataifa la mafuta na gesi linalotarajiwa kufanyika nchini Singapore mwishoni mwa mwezi Novemba mwaka huu.
Mwaliko huo umetolewa na Shirikisho la Makampuni makubwa ya kibiashara ya nchini Singapore wakati mwakilishi wake Cody Lee alipomtembelea Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na kufanya naye mazungumzo ofisini kwake leo jijini Dar es Salaam.
Lee, ambaye ni Mkurugenzi wa Shirikisho hilo kwa nchi zilizoko Mashariki ya Kati na Afrika, alimwambia Waziri Muhongo kwamba mwaliko huo unahusisha wataalamu wa sekta ya mafuta na gesi kutoka Tanzania na kwamba watajumuika na wenzao kutoka nchi mbalimbali duniani kote.
«Ni Kongamano ambalo linalenga kuwaleta karibu, kufahamiana na kujenga mahusiano kibiashara kwa kubadilishana taarifa mbalimbali wataalamu na wadau wa sekta za mafuta na gesi duniani kote,» alisema Lee.
Pamoja na kushukuru kwa mwaliko huo, Profesa Muhongo alimthibitishia Bw. Lee kwamba wataalamu kutoka Shirika la Maendeleo ya Mafuta na Petroli Tanzania (TPDC) na kutoka Wizarani watashiriki Kongamano hilo.
Aidha, Waziri Muhongo alibainisha kuwa, katika ushiriki wao, wawakilishi kutoka Tanzania watakuwa na banda la maonesho na watawasilisha mada inayohusu upatikanaji wa rasilimali husika nchini.
« Hii ni fursa nzuri kwa nchi yetu kujitangaza kimataifa kuhusiana na rasilimali za mafuta na gesi asilia, hivyo tutakuwa na banda la maonesho kuelezea rasilimali hizo na pia tutatoa mada katika Kongamano hilo. » Alisisitiza Waziri Muhongo.
Aidha, Lee ambaye aliambatana na Mkurugenzi wa mojawapo ya Makampuni yanayounda Shirikisho hilo Bw. G. Jayakrishnan, alitumia fursa hiyo kumweleza Waziri Muhongo nia ya taasisi yao kuwekeza hapa nchini hususan katika sekta ya nishati wakilenga zaidi mafuta na gesi.
Waziri Muhongo alimweleza Mkurugenzi huyo fursa za uwekezaji katika sekta ya nishati zilizopo nchini na kumhakikishia kwamba Makampuni yao yanakaribishwa kuwekeza nchini lakini akamtahadharisha kuwa ni nafasi ya ushindani. « Mtapaswa kushindana na kampuni nyingine mbalimbali zenye nia ya kuwekeza kwetu, nasi tutachagua zilizo bora zaidi » alisisitiza.
0 comments:
Post a Comment