Sunday, August 18, 2013

SHEIKH PONDA ISSA AZUSHA MAPYA





SHEIKH PONDA ISSA AZUSHA MAPYA
Masheikh waitahadharisha Serikali
*Polisi waweka doria misikitini Dar
SAKATA la Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda, limeendelea kuwa gumzo katika maeneo mbalimbali, huku matamko makali yakitolewa dhidi ya Serikali.

Sakata hilo limeonekana kutikisa na kutawala vyombo vya habari, baada ya kiongozi huyo wa dini kudaiwa kupigwa risasi, kusomewa mashtaka kitandani na baadaye kupelekwa gerezani chini ya ulinzi mkali akitolewa katika Taasisi ya Tiba na Mifupa (MOI).

Suala hilo limeibua hisia nyingine baada ya masheikh jijini Dar es Salaam, kutoa tamko lenye mwelekeo wa kupinga udhalilishwaji wa kiongozi huyo na kuionya Serikali juu ya mwenendo huo.

Mbali na masheikh kutoa tamko jana, Jeshi la Polisi kwa upande wake nalo liliimarisha ulinzi katika Msikiti wa Kichangani, uliopo Magomeni na ule wa Mtambani uliopo Kinondoni, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Msemaji wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Rajab Katimba, alisema kitendo hicho ni kibaya kwani kinapandikiza chuki baina ya Waislamu na Serikali.

Sheikh Katimba ambaye alikuwa ameongozana na masheikh kadhaa akiwamo Amiri wa Shura ya Maimamu, Sheikh Musa Kundecha, alitoa tamko hilo katika Msikiti wa Mtambani, Kinondoni jijini Dar es Salaam jana.

"Tunalaani kitendo alichofanyiwa Sheikh Ponda, tukio la kupigwa risasi na baadaye kudhalilishwa kwa kuondolewa hospitali wakati akipatiwa matibabu, ni jambo baya linakwenda kinyume na haki za binadamu.

"Tukio hili limeibua hisia kali kwa Waislamu, hivyo tunaitaka Serikali kuacha kuwatesa na kuwadhalilisha viongozi wa dini ya kiislamu, kwani kufanya hivyo ni kupandikiza chuki miongoni mwa Waislamu. 

"Waislamu wamekuwa wakiamini kwamba, ufumbuzi wa suala la amani ya kweli na ya kudumu ya nchi ni kuweza kushughulikia madai ya msingi ya Waislamu dhidi ya Serikali ambayo ndio chanzo cha madai ya kupigwa risasi kwa Sheikh Ponda," alisema Sheikh Katimba wakati akisoma tamko hilo lililosainiwa na Sheikh Juma Said Ally.

Source:Mtanzania




0 comments:

Post a Comment