Friday, August 17, 2012

Wizara Ya Nishati Na Madini Yakanusha Uchimbaji Wa Madini Ya URANI Kuanza


Tarehe 16 Agosti, 2012 gazeti la Rai Toleo Na.986 katika ukurasa wake wa kwanza na watatu lilichapisha taarifa yenye kichwa cha habari "UCHIMBAJI WA URANI SERIKALI YAONYWA" na kuwa kumezuka sakata lingine ambapo kampuni ya kigeni imeanza kuchimba madini hatari aina ya urani kwa kile wachunguzi wanasema ni kinyume cha sheria.

Gazeti hilo liliendelea kuandika kwamba Tanzania haina sera ya urani na kwamba hata kama Serikali imeruhusu uchimbaji huo, ni kinyume cha sheria kwa sababu hata Serikali yenyewe haijatunga sheria ya uchimbaji urani. Tunasema habari hii ina malengo ya kuupotosha umma.Mwandishi wa habari hii bila ya kutaja jina lake anaeleza kuwa hakuweza kuwasiliana na viongozi wa Wizara ya Nishati na Madini licha ya yeye kuwaandikia ujumbe kitu ambacho hakina ukweli. Kutokana na unyeti wa habari yenyewe mwandishi alipaswa kuhakikisha anapata taarifa kamili kutoka Wizarani na siyo kutoa taarifa kwa matakwa binafsi.Habari hii imelenga zaidi katika kuupotosha umma badala ya kuuelimisha kama ambavyo mwandishi ameshindwa kueleza kwa ufasaha ni nini hasa kusudio lake.

Tunaheshimu Uhuru wa vyombo vya Habari na tungependa kama kuna suala lolote linalohitaji ufafanuzi, Wizara ipo tayari muda wowote kutoa maelezo badala ya kukimbilia kuandika habari zinazojichanganya na kusababisha usumbufu kwa wananchi.

Tunatumia fursa hii kwa mara nyingine kuufahamisha umma kuwa kama Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Madini Mhe: Prof Sospeter Muhongo alivyosema kwenye hotuba ya bajeti ya mwaka huu kuwa pamoja na kuwepo kwa maeneo mbalimbali hapa nchini yenye madini ya urani ni maeneo mawili yaani Wilaya ya Namtumbo na Manyoni ndiyo yaliyothibitishwa kuwa na kiasi cha kutosha kuweza kuchimbwa kibiashara na si kweli kuwa uchimbaji umeanza.

Eneo la Namtumbo lipo ndani ya Hifadhi ya Taifa na Serikali iliwasilisha maombi UNESCO ya kurekebisha mipaka ya eneo la hifadhi ya Dunia ili kuongeza eneo la mradi, ombi liliridhiwa katika kikao cha UNESCO cha tarehe 02/Julai, 2012 kilichofanyika Saint Petersburg (Urusi).Aidha, Sera ya Madini ya Mwaka 2009 na Kanuni za Madini ya Mionzi Ayonisha za Mwaka 2010 - the Mining (Radioactive Minerals) Regulations, 2010 chini ya Sheria ya Madini, 2010 zinatumika katika kusimamia shughuli za utafutaji na uchimbaji wa madini ya urani nchini. 

Sheria na Kanuni zote zilizotungwa na zitakazoendelea kutungwa zinazohusiana na usimamizi wa madini ya urani pamoja na mambo mengine zinalenga kuzingatia miongozo/taratibu za Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomiki (IAEA) za usimamizi wa madini hayo zinazohakikisha kuwa uchimbaji hauleti athari kwa binadamu na mazingira.Tunaendelea kuwashauri waandishi wa habari kuwa sisi kama wizara na chombo cha Serikali tunawajibu wa kuelimisha umma juu ya shughuli mbalimbali za wizara hivyo tunawashauri kuwa tushirikiane kwa maslahi ya Taifa badala ya kutoa habari zenye malengo binafsi.

Imetolewa na:Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Nishati na Madini

0 comments:

Post a Comment