Wednesday, August 22, 2012

HABARI KUHUSU MTOTO WA AJABU ALIYE ZALIWA SUMBAWANGA HII HAPA



Katika hali isiyo kawaida msichana mmoja mkazi wa kijiji cha Mpasa mwambao mwa Ziwa Tanganyika Kata ya Kala wilayani Nkasi mkoani Rukwa amejifungua mtoto wa ajabu kufuatia ujauzito anaodai kuwa nao kwa kipindi cha miaka mitatu.


Mtoto huyo wa ajabu amezaliwa akiwa na idadi kamili ya meno ya mtu mzima na nywele zenye mvi katikati ya kichwa chake huku msichana huyo Lucia Sabastiano (18) akidai kuwa hawajawahi kukutana na mwanaume yeyote maishani mwake.


Mtoto huyo wa ajaabu ambaye alifariki baada ya siku mbili alikuwa wa kiume, pia alizaliwa akiwa na sehemu za siri zilizokomaa kama za mtu mzima ambazo zilikuwa na nywele ndefu katika sehemu hiyo.


Maumbile mengine ambayo yalionekana kuwa ya ajabu ni pamoja na mdomo wake kuwa na na rangi nyekundu, viganja na miguu yenye kucha ndefu na viungo vyake vikionekana kukomaa kama vya mtu mzima.


Akizungumzia tukio hilo Afisa Mtendaji wa kijiji cha Mpasa Privatous Maliyatabu alisema kuwa msichana huyo ambaye alipata ujauzito huo akiwa mwanafunzi wa darasa la tano alijifungua mwanzoni mwa mwezi huu, saa 10 alasiri nyumbani kwa mjombake aliyetajwa kwa jina moja la Mwelela.


Maliyatabu alisema kuwa Lucia alijifungua kwa msaada wa Mkunga wa jadi anayefahamika kwa jina la Mama Pashaa baada ya kupewa dawa ya kunywa na Mganga wa jadi Maneti Mazimba.


Kwa mujibu wa msichana licha ya kupata ujauzito huo lakini hajawahi kuwa na mahusiano ya kimapenzi na mwanaume yeyote yule maishani kwake na kuongeza kuwa hafahamu ni kwa jinsi gani alipata ujauzito huo aliokuwa nao kwa miaka mitatu mfululizo.


“Nakumbuka siku moja nilisimama mlangoni mwa nyumba yetu na ghafla niliona kama miujiza kwa kuona mwanga mkali mbele yangu hatimaye ilijitokeza sura ya mwanaume ambaye siwezi kuhadithia jinsi alivyo na baadaye akatoweka na kuanzia hapo nikaanza kuhisi tumbo langu limejaa na ndani kuna kitu kinacheza cheza”.


Baadaye aliwaeleza wazazi wake ambao waliamua kumpeleka hospitali baada ya kuona tumbo lake linazidi kukua siku hadi siku mithili ya mama mjamzito lakini kila hospitali kwa nyakati tofauti Lucia alipimwa na aliambiwa kuwa hakua na ujauzito wowote.


Alisema……..“ Kila waliponipima waliniambia kuwa sina mimba lakini me nilikuwa nahisi kuna kitu kama mtoto kinacheza tumboni mwangu kwa kipindi chote cha miaka mitatu, hali hiyo ilizidi kunishangaza”.


Mmoja wa ndugu wa Lucia ambaye hakutaka jina lake litajwe alisema kuwa wana uhakika ndugu yao hajawahi kukutana na mwanaume yeyote maishani mwake na familia nzima inashangazwa na ujauzito wake.


“Lucia ni miongoni mwa watoto watatu katika tumbo la mama yetu na amekuwa akitushangaza kwa yale ambayo yalikuwa yakimtokea tangia apate ujauzito huu kwani mara nyingi usiku amekuwa akiweweseka hali ilitofanya tuanze kuhangaika naye kwa waganga wa jadi baada ya hospitali kutueleza kuwa hana kitu chochote tumboni .” Alisema mwanadugu huyo aliyejitambulisha kuwa ni dadake.


Kwa upande wake Kaimu Mganga mkuu wa mkoa wa Rukwa Dk. Emmanuel Mtika alisema kuwa kitaalamu ujauzito unatakiwa kuwa wa muda wa wiki 38 hadi 40 na ikizidi sana wiki 42 hadi kujifungua , na kuongeza kuwa hakuna ujauzito wa miaka mitatu.


“Inawezekana huyu mwanamke alikuwa na matatizo ya uvimbe tumboni mwake kwa muda mrefu na akapata ujauzito uliodumu kwa muda wa kawaida ihali yeye akiamini kuwa alikuwa mjamzito kwa kipindi kirefu kumbe sivyo”Alisema Dk.Mtika.


Alisema kinachoshangaza ni maelezo ya kudai kuwa mjamzito pasipo kukutana na mwanaume kwani hakuna mwanamke anayeweza kupata ujauzito kwa hali hiyo.


“Inawezekana kuna mwanaume alitaka kufanya naye mapenzi kwa nguvu lakini hakuweza kumfikia kwenye sehemu muafaka ya sehemu ya siri , labda manii zinaweza kumwagika sehemu ya karibu na sehemu ya siri na zikamiminika hadi ndani,hapo uwezekano wa kupata ujauzito upo.”Alisema


Hatahivyo Dk. Mtika alisema mwanamke huyo hakuweza kwenda kwenye hospitali kubwa kupata vipimo ili kubaini tatizo liliokuwa likimsumbua kwa kipindi chote.

0 comments:

Post a Comment