Chama cha kandanda cha FA nchini Uingereza, kimeelezea kwamba kitamshitaki mchezaji wa Manchester United, Rio Ferdinand, kufuatia maandishi yake katika mtandao wa kijamii wa Twitter.
Ferdinand alikanusha habari kwamba yeye ni mbaguzi wa rangi, kufuatia maneno yake kuhusiana na "choc ice", akimaanisha barafu ya kula yenye rangi mbili, katika kuelezea mchezaji wa Chelsea, Ashley Cole, ni mtu wa aina gani.
"Choc ice" ni maneno ambayo hutumia kuelezea juu ya rangi nyeusi na nyeupe katika barafu hiyo, na ni maneno yanayoweza kutumiwa katika kuelezea kwamba mtu fulani juujuu ni mweusi, lakini ndani hasa yeye ni mweupe.
Ferdinand, mwenye umri wa miaka 33, ana muda wa kujitetea, hadi saa kumi, tarehe 2 Agosti, kabla ya kuchukuliwa hatua zaidi.
Taarifa katika mtandao wa FA inaelezea: "Madai ni kwamba mchezaji huyu alionyesha tabia isiyokuwa nzuri/na kwa njia inayouletea mchezo fedheha kwa kuandika maneno hayo kuhusu asili au rangi."
Cole, ambaye ni mchezaji wa ulinzi wa Chelsea, alifika mahakamani kama shahidi wakati wa kumtetea mchezaji mwenzake katika timu, John Terry, na ambaye mahakama ilimuondolea mashtaka kuhusiana na ubaguzi wa rangi.
Terry alikuwa ameshtakiwa kwa kutumia matamshi ya ubaguzi wa rangi dhidi ya mdogo wake Ferdinand, Anton, katika mechi iliyochezwa tarehe 23 Oktoba mwaka jana.
Terry, mwenye umri wa miaka 31, tayari ameshtakiwa na chama cha FA kwa tabia isiyofaa, dhidi ya Anton Ferdinand, na ameapa kujitetea kuhusiana na madai hayo.
SOURCE: BBC
0 comments:
Post a Comment