Sunday, July 1, 2012

HOTUBA YA RAIS JAKAYA KIKWETE KWA WATANZANIA MWISHO WA MWEZI WA 6 2012


Ndugu Wananchi,

Kama ilivyo ada naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa
Rehma, kwa kutujaalia uzima na kutuwezesha kumaliza nusu ya kwanza ya
mwaka 2012 salama. Kwa kutumia utaratibu wetu wa kuzungumza nanyi kila
mwisho wa mwezi, leo napenda kuzungumzia mambo mawili. Jambo la kwanza
ni suala la usafirishaji haramu wa binadamu nchini na la pili ni la
mgomo wa madaktari.

Usafirishaji Haramu wa Binadamu Nchini

Ndugu Wananchi;
Bila ya shaka mtakuwa mmezisikia taarifa za tukio la kushtusha na
kuhuzunisha la kukutwa maiti 43 za watu wasiojulikana, zilizotupwa
katika kichaka kilichopo kijiji cha Chitego, Wilayani Kongwa, Mkoa wa
Dodoma tarehe 26 Juni, 2012. Pamoja na maiti hao, walipatikana watu 84
wakiwa hai lakini wote wakiwa wamedhoofu na baadhi yao wakiwa
mahututi. Hatua za haraka zilichukuliwa kuwasafirisha watu hao hadi
Dodoma ambapo wale waliokuwa mahututi walifikishwa Hospitali Kuu ya
Mkoa wa Dodoma kwa matibabu na wengine walihifadhiwa katika Kituo cha
Kati cha Polisi, Dodoma. Maiti 22 zilipelekwa Dodoma na 21 zilipelekwa
Morogoro kuhifadhiwa.

Taarifa zilizopatikana kutoka kwa wale walionusurika zimebainisha kuwa
watu hao ni raia wa Ethiopia ambao walikuwa safarini kwenda Malawi na
baadaye Afrika ya Kusini ambako wangetengenezewa utaratibu wa kwenda
kuishi Marekani na Ulaya. Kwa mujibu wa maelezo yao, safari yao
ilianza miezi mitano iliyopita. Mwezi mmoja waliutumia Ethiopia na
miezi minne waliitumia Kenya kabla ya kuletwa Arusha ambako walipakiwa
kwenye lori na kuanza safari ya kuelekea Malawi lakini ikaishia
Chitego. Lori walilopanda lilikuwa limezibwa kabisa na hivyo
kusababisha vifo kwa kukosa hewa.

Tukio la Chitego, Dodoma la wahamiaji haramu kukamatwa na wengine
kukutwa wamekufa si la kwanza kutokea hapa nchini. Kwa jumla, katika
kipindi cha takriban miaka 10 sasa kumekuwepo na tatizo kubwa la
wahamiaji haramu kuingia nchini. Kwa mfano, kati ya mwaka 2005 na hivi
sasa jumla ya wahamiaji haramu 19,683 wamekamatwa. Karibu wote
wameshaondoshwa nchini na hivi sasa wapo karibu watu 1,500 tu
magerezani wanaotumikia adhabu na kusubiri kurejeshwa makwao. Wengi wa
watu hao wanatoka Ethiopia na Somalia na baadhi kutoka Pakistan na
Bangladesh.

Wahamiaji haramu wamekuwa wanaingia nchini kwa kupitia njia zisizo
rasmi. Wapo wanaotumia nchi kavu hasa kupitia mikoa ya Mara, Arusha,
Kilimanjaro na Tanga. Na, wapo wanaopitia baharini kwa kutumia fukwe
za Pemba, Unguja na za mikoa ya ukanda wa Pwani ya Tanzania Bara yaani
Tanga, Pwani, Lindi na Mtwara.

Ndugu Wananchi;
Kwa mujibu wa kauli zao, watu hao wamekuwa wanaeleza kuwa hawaji
nchini kuhamia bali wao ni wapita njia tu. Wanaelekea Afrika ya Kusini
ambako wameahidiwa kuwa watatengenezewa mipango ya kuhamia Marekani na
Ulaya. Watu hao pia wamethibitisha kuwepo kwa watu maalum
wanaojihusisha na usafiri wao tangu nchi watokako na zote wanazopitia
mpaka kule waendako. Aidha, wamesema kuwa wao wanawalipa watu hao ili
wawasafirishe na hakika si kiwango kidogo. Kwa jumla ni kwamba hili si
suala la uhamiaji haramu bali ni la biashara haramu ya kusafirisha
binadamu.

Ndugu Wananchi;
Kufuatia vyombo vyetu vya usalama kuwa makini na watu wengi kukamatwa
ndipo wasafirishaji walipobuni njia za kuwasafirisha kama mizigo.
Makontena, malori yaliyofunikwa nyuma na matenki ya mafuta na ya maji
yamekuwa yanatumika kwa ajili hiyo. Usafiri wa aina hiyo ndiyo
uliosababisha vifo vilivyotokea Dodoma tarehe 26 Juni, 2012 na vya
watu 21 vilivyotokea mwezi Desemba, 2011 Mkoani Morogoro, na vile vya
watu 12 vilivyotokea katika matukio mawili ya Mkoa wa Mbeya, mwezi
Mei, 2012.

Ndugu Wananchi;
Tarehe 27 Juni, 2012 nilikutana na wakuu wa vyombo vya ulinzi na
usalama nchini kuzungumzia tukio la Chitego na suala zima la biashara
hii haramu na hasa mbinu mpya inayotumiwa na wasafarishaji. Nilitoa
pongezi kwa vyombo vya dola kwa kazi nzuri waifanyayo kudhibiti
shughuli za biashara hii haramu hapa nchini. Tulielewana kuwa
waendelee kuimarisha udhibiti huo kwa lengo la kukomesha kabisa
biashara hii.

Niliagiza pia kwamba kikundi kazi nilichokiunda mwaka 2006
kushughulikia ujambazi sasa kielekeze sehemu ya nguvu zake kukabili
tatizo hili. Aidha, kwa pamoja tulikubaliana kuwa nchi yetu
ishirikiane na wenzetu wa Ethiopia, Kenya, Malawi, Msumbiji na Afrika
ya Kusini kutambua mawakala na kuwabana kwa mujibu wa sheria. Tayari
nimeshaanza kufanya mawasiliano na baadhi ya Wakuu wa Nchi hizo kuhusu
ushirikiano huo. Nashukuru wote wameafiki nchi zetu zishirikiane kwa
pamoja kuvunja mtandao huu mchafu na kutokomeza biashara hii haramu na
inayodhalilisha utu wa mwanadamu.

Ndugu Wananchi;
Napenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru wenzetu, wakazi wa vijiji vya
Chitego na Mkoka kwa kazi nzuri walioifanya. Kwa kweli, wenzetu
wameonesha uzalendo wa hali ya juu kwa kutoa taarifa mapema juu ya
jambo lenyewe, lakini pia wameonesha utu kwa kuwajali wageni
waliokumbwa na janga hili. Naushukuru pia uongozi wa Mkoa wa Dodoma na
Morogoro ikiwa ni pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama kwa
kulishughulikia tatizo hilo kwa umakini mkubwa. Nimefurahishwa sana na
ushirikiano ulioonyeshwa na vyombo na taasisi mbalimbali za Serikali
katika kushughulikia suala hili.

Mgomo wa Madaktari
Ndugu Wananchi;
Jambo la pili ni kuhusu mgomo wa Madaktari unaoendelea nchini hivi
sasa. Nilipozungumza na Wazee wa Dar es Salaam katika Ukumbi wa
Diamond Jubilee tarehe 12 Machi, 2012, kuhusu mgomo wa Madaktari
uliokuwa unaendelea wakati ule pamoja na kuelezea chimbuko la mgomo na
hatua iliyokuwa imefikiwa, nilielezea mazungumzo yangu na viongozi wa
Chama cha Madakari wakiwemo pia viongozi wa Jumuiya ya Madaktari.
Nilitoa taarifa kuwa tumeelewana kuwa watasitisha mgomo na watarudi
kwenye meza ya majadiliano na Serikali. Siku ile pia nilielezea
matumaini yangu kuwa mgomo ule utakuwa wa mwisho katika nchi yetu.
Bahati mbaya matumaini yangu hayo hayakuwa na hivi sasa tunashuhudia
tena wagonjwa wakiteseka, kuhangaika na wengine kufa kwa sababu ya
kukosa huduma wanazostahili kwa vile madaktari wao wamegoma tena.

Ndugu Wananchi;
Kama walivyoniahidi, madaktari waliacha kugoma na viongozi wao
walirudi kwenye mazungumzo na Serikali. Kama ilivyoagizwa na Mahakama
Kuu, Kitengo cha Kazi tarehe 8 Machi, 2012, kwa mujibu wa Sheria ya
Mahusiano Kazini, Namba 6 ya mwaka 2004. Chama cha Madaktari na
Serikali walifika katika Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (Commission for
Mediation and Arbitration) kwa ajili ya majadiliano. Kwa pamoja na kwa
ridhaa yao wote, pande hizo mbili ziliiomba Tume hiyo iwape fursa ya
kuzungumza wao wenyewe na wakimaliza mazungumzo wataenda kusajili
makubaliano yao. Tume ikawakubalia. Ni vizuri ikakumbukwa kuwa siku
ile ya tarehe 8 Machi, 2012 Mahakama Kuu Kitengo cha Kazi, ilitoa zuio
la mgomo pamoja na kuagiza kuwepo mazungumzo baina ya pande mbili.

Ndugu Wananchi;
Kati ya tarehe 10 Aprili, 2012 na tarehe 30 Mei, 2012, vilifanyika
vikao sita vya majadiliano kati ya Serikali na Chama cha Madaktari.
Katika mazungumzo hayo hoja au madai 12 ya madaktari yalizungumzwa.
Mambo hayo ni haya yafuatayo:

1.Posho ya kuitwa kazini (on call allowance) iwe asilimia 10 ya
mshahara.
2.Posho ya kufanya kazi katika mazingira hatarishi (Risk allowance)
iwe asilimia 30 ya mshahara.
3.Madaktari wapatiwe nyumba grade A au posho ya makazi ambayo iwe
asilimia 30 ya mshahara.
4.Posho ya kufanya kazi katika mazingira magumu iwe asilimia 40 ya
mshahara.
5.Madaktari walipwe posho ya usafiri ya asilimia 10 ya mshahara au
wakopeshwe magari.
6.Madaktari wanaoanza kazi walipwe mshahara wa shilingi 3,500,00/= kwa
mwezi.
7.Madaktari wapatiwe Green Card za Bima ya afya.
8.Hatua za kinidhamu zichukuliwe dhidi ya Watendaji Wakuu wa Wizara ya
Afya na Ustawi wa Jamii.
9.Viongozi wa Kisiasa kulazimisha kupewa rufaa nje.
10.Madaktari waliofukuzwa warudishwe kazini.
11.Huduma za afya ziboreshwe nchini.
12.Posho ya uchunguzi wa maiti iongezwe.

Ndugu Wananchi;
Katika mambo hayo 12 pande zote mbili zilifikia muafaka na kukubaliana
wa pamoja kwa mambo saba. La kwanza, ni kuhusu usafiri wa kwenda na
kurudi kazini. Serikali ilieleza kuwa upo utaratibu kwa mujibu wa
Waraka wa Utumishi wa Serikali Na. 3 wa mwaka 2011 wa kuwakopesha
wafanyakazi wa Serikali fedha za kununulia magari au pikipiki, samani
na matengenezo ya magari. Ilikubaliwa kuwa madaktari waitumie fursa
hiyo.
Jambo la pili, ni kuhusu madaktari kupatiwa Green Card za Bima ya
Afya. Jambo hili lilikubaliwa na Serikali na Wizara ya Afya
imekwishachukua hatua za utekelezaji wake.

Jambo la tatu, ni kuhusu hatua za kinidhamu kuchukuliwa dhidi ya
Watendaji Wakuu wa Wizara ya Afya. Kwa pamoja walikubaliana kuwa suala
hilo liko nje ya mamlaka ya Kamati yao ya pamoja, waziachie mamlaka
husika za uteuzi. Uongozi wa juu wa Wizara umebadilishwa na sasa kuna
uongozi mpya. Lakini, jambo la kustaajanisha hata Waziri mpya wa Afya
alipowataka waonane kuzungumzia hoja walikataa kumuona. Kwanza
walisema hawaoni sababu kwa vile wameyazungumza na Kamati yake kwa
miezi mitatu bila ya mafanikio
Jambo la nne walilokubaliana ni kuhusu viongozi kulazimisha kupewa
rufaa ya kutibiwa nje. Walikubaliana mambo mawili. Kwanza, kwamba
maelekezo ya Waziri Mkuu, Mhe. Mizengo Pinda kuwa madaktari wazingatie
maadili ya kazi zao na kukataa kutoa rufaa kwa mtu asiyestahili awe
kiongozi au asiwe kiongozi. Pili, walikubaliana kuwa hospitali
zilizopo ziboreshwe ili viongozi watibiwe hapa nchini. Ukweli ni
kwamba kufanya hivyo ndiyo sera ya Serikali. Nililieleza hili mwezi
Desemba 30, 2005 katika hotuba yangu ya kuzindua Bunge baada ya
kuchaguliwa kwa mara ya kwanza kuongoza nchi yetu.

Tumeiongeza sana bajeti ya sekta ya afya kutoka shilingi bilioni 300
2005/2006 hadi shilingi trilioni 1.2 mwaka 2011/12 na imekuwa ya tatu
baada ya miundombinu na elimu. Tumeziimarisha hospitali za Mikoa kwa
vifaa tiba na wataalamu wa afya. Kazi inaendelea katika hospitali za
Wilaya. Tumewekeza katika Hospitali ya Muhimbili. Hospitali hiyo
ilivyo leo sivyo ilivyokuwa miaka sita nyuma. Na kazi inaendelea hasa
katika maeneo ambayo tunapeleka wagonjwa nje. Matunda yake yanaanza
kuonekana kwa upande wa figo, moyo, kinywa na mipango inaendelea kwa
upande wa ubongo na mishipa ya fahamu. Tunaendelea kuimarisha mafunzo
ya madaktari na madaktari bingwa, yote kwa nia hiyo hiyo. Hivi sasa
Chuo Kikuu cha Sayansi ya Tiba,Muhimbili kinachukua wanafunzi wengi
zaidi ya ilivyokuwa siku za nyuma na makazi mapya ya chuo yanaendelea
kuandaliwa ili kuchukua wanafunzi wengi zaid. Mwaka 2005 tulikuwa na
madaktari bingwa 46 mwaka huu tunao 520.

Ndugu Wananchi;
Jambo la tano ambalo pande zote mbili zilikubaliana ni kuhusu
madaktari waliofukuzwa. Hawa ni wale Interns waliokuwa wamerudishwa
Wizarani kutoka Muhimbili na kupangiwa hospitali za Temeke, Ilala,
Mwananyamala na Lugalo. Hili ni jambo ambalo lilikuwa limemalizika
kitambo na wote walikuwa wamerudi Muhimbili.

Jambo la sita ni kuhusu mapendekezo mbalimbali yaliyotolewa na
madaktari kuhusu kuboresha huduma ya afya. Mapendekezo hayo yalihusu
kutathmini sera na mpango wa afya ya msingi, bajeti ya afya kuwa
asilimia 15 ya bajeti ya Serikali, kuwepo na utaratibu mzuri wa
kuajiri madaktari na kuboresha viwango vya ubora wa madaktari na
kadhalika. Serikali imeyaafiki mapendekezo hayo na yatafanyiwa kazi.

Jambo la saba, ambalo pande zote walilokubaliana ni kuhusu kuongeza
posho ya uchunguzi wa maiti. Hili ni jambo jipya halikuwepo mwazoni.
Hata hivyo, Serikali imelikubali na posho hiyo imeongezwa kutoka
shilingi 10,000/= hadi kufikia shilingi 100,000/= kwa daktari na
shilingi 50,000/= kwa wasaidizi wake.

Ndugu Wananchi;
Kuna masuala matatu ambayo yamekuwa na muafaka kwa kiasi fulani na
kutoafikiana kwa baadhi ya mambo. La kwanza ni suala la kufanya kazi
katika mazingira hatarishi. Serikali imekubali hoja ya kuchukua hatua
ya kuwalinda madaktari wanaofanya kazi katika mazingira hatarishi.
Serikali iliwaeleza kuwa watumishi wa kada zote za afya watapatiwa
chanjo dhidi ya maambukizi ya Hepatitis B na fedha zimetengwa katika
bajeti ya 2012/13.

Aidha, Serikali imeeleza dhamira ya kurudisha posho ya mazingira
hatarishi kwa watumishi wa umma wanaostahili. Utekelezaji wake
utafanyika baada ya uchambuzi wa kina wa kubainisha mazingira
hatarishi ni yepi, viwango stahiki viwe vipi na nani hasa wahusike.
Madaktari wamekataa hili la kufanya uchambuzi, wanataka kiwango kiwe
kama wanavyotaka wao, yaani asilimia 30 ya mshahara na kianze mara
moja.

Jambo la pili ambalo wamekubaliana nusu nusu ni kuhusu nyumba za
kuishi. Serikali imekiri wajibu wake wa kuwapatia madakari nyumba za
kuishi. Aidha, imeeleza mpango ulioanza wa kujenga nyumba 700 za
madaktari kote nchini na kwamba hivi sasa ujenzi wa nyumba 90
unaendelea, 50 katika mkoa wa Mtwara na 40 katika mkoa wa Rukwa.

Kwa maeneo ambayo madaktari wanalipwa posho ya pango Serikali imesema
waajiri wataendelea kufanya hivyo kwa mujibu wa taratibu zilizopo kwa
watumishi wa umma wenye stahili ya kupewa nyumba. Jambo hilo
limekataliwa na Madakari na kutaka lazima walipwe asilimia 30 ya
mshahara kama posho ya nyumba. Serikali kwa upande wake imeona vigumu
kufanya hivyo na kuwasihi wakubali wanayotendewa wafanyakazi wengine
wote wa umma.

Jambo lingine ambalo lilikuwa na makubaliano ya nusu nusu ni kuhusu
posho ya kufanya kazi katika mazingira magumu. Pande zote mbili
ziliafikiana kuwa yapo baadhi ya maeneo nchini yanayo mazingira magumu
kwa watumishi wa umma hivyo hatua zichukuliwe kuwasaidia watumishi
hao. Serikali imekubali wajibu wa kuweka utaratibu wa kuboresha maisha
ya watumishi katika maeneo hayo. Kwa ajili hiyo, Serikali itatoa
mwongozo kwa mamlaka za ajira kuhusu namna ya kuwasaidia watumishi hao
kupunguza makali ya maisha katika kila eneo badala ya kutegemea posho
peke yake.

Kuhusu posho, Serikali imeeleza kuafiki kuwepo posho ya aina hiyo ila
itatekelezwa baada ya kufanya uchambuzi wa kuainisha mazingira husika,
kutambua watumishi waliopo na gharama zake.

Madaktari hawajakubali kusubiri zoezi la uchambuzi lifanyike, wanataka
Serikali ilipe posho hiyo sasa. Tofauti hapa si posho hiyo kuwepo,
bali ni rai ya Serikali ya kubaini maeneo yenyewe na kupanga aina ya
hatua na viwango vya posho kulingana na mazingira halisi ya maeneo.
Madaktari hawaoni haja ya kufanya hayo.

Ndugu Wananchi;
Mambo mawili hayakuwa na muafaka kabisa kati ya pande zetu mbili.
Jambo la kwanza ni posho ya kuitwa kazini (on call allowance). Kwanza
sina budi kueleza kuwa Serikali imekubali kuongeza posho hiyo. Tangu
Februari, 2012 posho iliongezwa kutoka shilingi 10,000/= hadi shilingi
25,000/= kwa daktari bingwa (Specialist), shilingi 20,000/= kwa dakari
mwenye usajili wa kudumu (Registrars) na shilingi 15,000/= kwa
madaktari waliohitimu ambao wapo katika kipindi cha mafunzo kazini
(Interns). Viwango hivyo vya posho vinatumika hivi sasa.

Madaktari kwa upande wao hawakukubali uamuzi huo wa Serikali na
kusisitiza walipwe asilimia 10 ya mshahara. Ugumu wa kukubali
pendekezo la madakari ni kuwa sharti la malipo haya ni mtu kuitwa
kazini. Ukitaka ilipwe kiwango cha mshahara ina maana kuwa hata kama
daktari hakupangwa kuitwa au alipangwa na hakutokea aendelee kulipwa.
Hili haliwezi kuwa sahihi kufanya. Linaweza kuwafanya baadhi ya
madaktari kutokutimiza wajibu wao kwa vile wana hakika mwisho wa mwezi
malipo yako pale pale.

Ndugu Wananchi;
Jambo la pili ambalo muafaka haukufikiwa baina ya Serikali na
madaktari ni kuhusu mshahara wa kuanzia kazi wa daktari. Madaktari
wanataka uwe shilingi 3,500,000/= wakati Serikali inasema kiasi hicho
hatukiwezi. Serikali imeeleza utayari wake wa kuongeza mshahara kwa
kati ya asilimia 15 mpaka 20 kama ambavyo itafanya kwa watumishi wote
wa umma katika mwaka huu wa fedha. Kwa kiwango cha sasa cha mshahara
wao, daktari ataanzia kati ya shilingi 1,100,000/= na 1,200,000/=
kutegemea kiwango kipi hatimaye kitaamuliwa. Madaktari wamekataa
katakata na wameng'ang'ania shilingi 3,500,000/=.

Ndugu Wananchi;
Huo ndiyo mlolongo wa mambo yaliyozungumzwa na pande zote mbili na
matokeo ya mazungumzo yenyewe. Katika kikao cha sita kilichofanyika
tarehe 30 Mei, 2012, upande wa Chama cha Madaktari ulisema kuwa kwa
vile hoja ya nyongeza ya mshahara haina mabadiliko hawakuona haja ya
kuendelea na majadiliano mpaka watakapowasiliana na wenzao. Waliahidi
kutoa taarifa ndani ya wiki mbili. Tarehe 12 Juni, 2012, Rais wa MAT
aliandika barua kwa Katibu Mkuu Utumishi ambaye ndiye kiongozi wa
majadiliano kwa upande wa Serikali, kuwa Madaktari wameikataa taarifa
na ufafanuzi waliopewa kutoka Serikalini kwa ujumla wake.

Ndugu Wananchi;
Baada ya majibu yale ya madaktari, tarehe 19 Juni, 2012, Serikali na
Madaktari walikwenda kwa Msuluhishi (CMA) kutoa taarifa kuwa mgogoro
umekosa usuluhishi kama sheria inavyotaka. Kwa pamoja pande zote mbili
zilikubaliana suala hilo lifikishwe Mahakama Kuu Kitengo cha Kazi.
Wakati pande zote zinasuburi mgogoro huu kufikishwa ngazi hiyo ya juu,
upande wa Madaktari ukatangaza kuwepo kwa mgomo kuanzia saa sita ya
usiku tarehe 23 Juni, 2012. Hatua hiyo haikustahili kwani suala
lenyewe halijafika mwisho wa kushughulikiwa kwa mujibu wa Sheria za
Mahusiano ya Kazi nchini.

Ndugu Wananchi;
Tarehe 22 Juni, 2012, Mwanasheria Mkuu wa Serikali akaenda Mahakama
Kuu Kitengo cha Kazi kulifikisha suala la tishio la mgomo na kuomba
zuio la muda kufanywa. Mahakama Kuu ilikubali ombi hilo na kuagiza
kuwa mgomo usitishwe. Juhudi za kumtafuta Rais wa MAT, Dkt. Namala
Mkopi na viongozi wengine wa MAT hazikufanikiwa, Ofisi ya MAT ilikuwa
imefungwa na simu zote za viongozi wa MAT zilikuwa zimezimwa. Hatimaye
tarehe 25 Juni, 2012, alipatikana na kupewa amri hiyo ya Mahakama.
Tarehe 26 Juni, 2012, Dkt. Mkopi alifika Mahakamani ambapo alikana
kuwa yeye hahusiki na kuitisha huo mgomo lakini hakumtaja aliyehusika.
Pamoja na rai hiyo, Jaji alimuamuru Rais wa MAT akawatangazie
wanachama wake kusitisha mgomo. Dkt. Namala Mkopi hajafanya hivyo hadi
leo na mgomo umekuwa unaendelea kinyume cha Sheria.

Ndugu Wananchi;
Wagonjwa wanateseka na wengine kupoteza maisha kwa mgomo huu usiokuwa
halali kisheria ambao pia haustahili kuwepo hata kwa mujibu wa maadili
ya udaktari. Viongozi wa MAT na wenzao wanawaingiza Madaktari katika
mgogoro na Mahakama na waajiri wao isivyostahili. Ni vyema viongozi wa
Madaktari na madaktari wakatambua kuwa wanashiriki katika mgomo
usiokuwa halali ambao pia kiongozi wao mkuu amekana Mahakamani kuwa
hahusiki nao. Madaktari lazima watambue pia kwamba ajira zao
wanaziweka hatarini. Mfanyakazi ana kinga ya kutofukuzwa kazi na
mwajiri kwa kushiriki mgomo unaokubalika kisheria. Huu siyo.
Watapoteza ajira, hawana pa kukimbilia, hawana cha kiwalinda. Kwa
madaktari interns, wanahatarisha maisha yao kwani hawatapata cheti cha
kudumu wakishiriki mgomo usiokuwa halali. Lazima watafakari sana kwa
hayo wafanyayo.

Ndugu Wananchi;
Napenda kurudia maneno niliyoyasema tarehe 12 Machi, 2012, kuwa
kuboresha mishahara na maslahi ya wafanyakazi ni Sera ya Serikali yetu
kwa maelekezo ya Ilani ya Chama Tawala (CCM). Tumeitekeleza kwa
vitendo sera hiyo, hata hivyo ni ukweli ulio wazi kuwa nia yangu njema
tu pekee haitoshi, lazima uwezo wa kufanya hivyo uwepo. Kwa kulingana
na uwezo uliopo, tumeendelea kuboresha mishahara na maslahi ya
wafanyakazi hatua kwa hatua tangu tuingie madarakani. Tumefanya hivyo
kwa jumla kwa wafanyakazi wote na kwa kada mbalimbali za watumishi wa
umma.

Miongoni mwa wafanyakazi wa umma walionufaika na hatua hizo za
Serikali ni madaktari na watumishi wa kada nyingine za huduma ya afya.
Tena nadiriki kusema madaktari tumewapa upendeleo mkubwa kuliko
watumishi wengine wa umma. Upendeleo upo kwenye mafunzo ambapo
wanafunzi wa udaktari wanagharimiwa na Serikali kwa asilimia mia moja
wakati wanafunzi wenzao wa taaluma nyingine hawako hivyo.

Ndugu Wananchi;
Mwaka 2004/2005, mshahara wa kuanzia wa daktari ulikuwa shilingi
178,700/=, mwaka 2005/ 2006 tuliupandisha na kuwa shilingi 403,120/=.
Tuliendelea kuupandisha mwaka hadi mwaka mpaka kufikia shilingi
957,700/= wanazolipwa sasa. Kiasi hicho ni mara mbili ya mishahara ya
watumishi wa taaluma nyingine wenye shahada ya kwanza wanaoanza kazi
ambao kwa wastani hupata shilingi 446,100/=.

Tunafanya hivyo kwa kutambua na kuthamini nafasi maalum ya madaktari
katika jamii na ukweli kwamba bado tunayo safari ndefu ya kuziba pengo
la madaktari nchini. Lakini inaonekana juhudi zetu zote hizo
hazithaminiwi.

Ndugu Wananchi;
Sina budi kusisitiza kwamba tunapofanya hivyo tunaongozwa na uwezo
tulio nao wa kulipa. Kwa sasa hatuwezi kuwaahidi kuwa tunao uwezo wa
kuwalipa mshahara wa kuanzia wa shilingi 3,500,000/= na posho zote
zile.
Tukifanya hivyo malipo ya daktari anayeanza kazi yatakuwa shilingi
7,700,000/=. Kwa hakika kiasi hicho hatutakiweza. Si vyema kutoa ahadi
hewa kwa watu tunaowaheshimu na kuwathamini kama walivyo madaktari.
Kutokana na ukweli huo basi kama daktari anayeona kuwa hawezi kufanya
kazi Serikalini bila ya kulipwa mshahara huo awe huru kuacha kazi na
kwenda kwa muajiri anayeweza kumlipa kiasi hicho. Nasi tutamtakia kila
la heri. Hana sababu ya kugoma ili ashinikize kulipwa mshahara huo.
Asisumbuke, hatalipwa mshahara huo. Isitoshe, hana sababu ya kuendelea
kuwa na mgogoro na mwajiri ambaye hana uwezo wa kumlipa anachokitaka.
Huna sababu ya kumpa usumbufu mwajiri wa kukuandikia barua ya
kujieleza au kukuachisha kazi. Kwa nini upate usumbufu wa kupata barua
hizo na kuzijibu. Kwa nini upate usumbufu wa kuachishwa kazi na
kutakiwa kuondoka kwenye nyumba ya Serikali ndani ya saa 24. Jiepushe
na yote hayo kwa kujiondoa mwenyewe. Usipofanya hivyo, mwajiri anakuwa
hana jinsi bali kukuondoa kazini maana unakwenda kinyume na sheria za
kazi na maadili ya kazi ya udaktari.

Mamlaka za ajira zimeanza kuchukua hatua hizo na wataendelea kufanya
hivyo kwa wote wanaoendelea kugoma. Najua baada ya hatua hizo
kuchukuliwa kuna manun'guniko ya kuonewa. Hivyo, mlitegemea mwajiri
afanyeje? Ni bora kufanya hivyo ili ajue hana daktari aweze kufanya
utaratibu wa kuziba hilo pengo na huyo ajae awe na mahali pa kuishi.
Vinginevyo atakuwa anajidanganya kuwa anae daktari ambae hayupo kazini
na wala hataki kufanya kazi.

Ndugu Wananchi;
Napenda kuwathibitishia kwamba dhamira ya Serikali ya kuboresha
maslahi ya watumishi wa umma wakiwemo madaktari iko wazi. Tumekuwa
tunafanya hivyo, na tutaendelea kufanya hivyo kulingana na uwezo wa
kibajeti. Ni vyema watumishi wa umma wakatambua kuwa hatuwezi kutumia
fedha zote au kiasi kikubwa mno cha pesa za umma kulipana mishahara.
Tukifanya hivyo, Serikali itashindwa kutoa huduma muhimu kwa wananchi
ambao ndiyo wengi na wanastahili kuhudumiwa. Hata hizo huduma za afya
tunazosema ni duni tuziboreshe, hatutaweza kuziboresha kama tutatumia
sehemu kubwa ya pesa za Serikali kuwalipa mishahara wafanyakazi.

Hivi sasa matumizi ya mishahara ni asilimia 48 ya bajeti ya Serikali.
Kiwango hicho ni kikubwa mno. Uwiano mzuri ni kuwa na matumizi ya
mishahara yasiyozidi asilimia 35 ya bajeti na asilimia 65 zitumike
kugharimia huduma na shughuli nyingine za maendeleo ya wananchi na
taifa. Sisi tumezidi kwa asilimia 13. Hivyo, hatuna budi tukubali
kujinyima kwa manufaa ya walio wengi.

Suala la Dkt. Steven Ulimboka

Ndugu Wananchi;
Kabla ya kumaliza hotuba yangu, napenda kuungana na Watanzania
wenzangu wote kuelezea masikitiko yangu makubwa na kuhuzunishwa kwangu
na kitendo cha kinyama alichofanyiwa Dkt. Steven Ulimboka usiku wa
tarehe 26 Juni, 2012. Kitendo hicho ni kinyume kabisa na mila na
desturi zetu. Watanzania hatujayazoea mambo hayo. Nimeelekeza vyombo
vyetu vya ulinzi na usalama kufanya uchunguzi wa kina ili ukweli
ujulikane. Nimesema kuwa ningependa ukweli huo ujulikane mapema ili
tuondoe wingu baya la kutiliana shaka na kulaumiana kunakoendelea hivi
sasa.

Natambua kuwa Serikali nayo inatajwa katika orodha ya wanaotiliwa
shaka. Mimi nimeshangazwa sana na hisia hizo kwani siioni sababu ya
Serikali kufanya hivyo. Dkt. Ulimboka alikuwa mmoja wa kiungo muhimu
katika mazungumzo baina ya Serikali na Madkatari. Ni kweli kwamba yeye
si mtumishi wa Serikali, hivyo hakustahili kuwa sehemu ya majadiliano
haya. Kulikuwa na rai ya kutaka asiwepo, lakini nilisema wamuache
maadam Madaktari wanamuamini kuwa anaweza kuwasemea vizuri zaidi
kuliko wao wenyewe walioajiriwa na Serikali.

Ndugu Wananchi;
Kama nilivyoeleza, mazungumzo yalienda vizuri na mafanikio makubwa
yamepatikana. Yapo maeneo machache na hasa eneo la mshahara ambalo
hatukuweza kukubaliana. Hapo tulipofikia si pabaya na tulikubaliana
sote kurudi kwenye mkondo wa Sheria kusaidiwa. Kwa nini Serikali
imdhuru Dkt. Ulimboka? Na, kuhusu mgomo, Mahakama Kuu imekwishatoa
amri ya kusitisha mgomo. Anayekaidi amri ya Mahakama ananunua ugomvi
na mhimili huo wa dola ambao wenyewe una mamlaka ya kumtia adabu mtu
huyo. Hivi baada ya kufika hapo Serikali iwe na ugomvi na Dkt. Steven
Ulimboka kwa sababu ipi na jambo lipi hata iamue kumdhuru? Kama kuna
mtu wa Serikali kafanya, itakuwa kwa sababu zake binafsi na siyo za
Serikali au kwa kutumwa na Serikali.

Ndugu Wananchi;
Kwa niaba yangu na kwa niaba ya Serikali natoa mkono wa pole kwa Dkt.
Steven Ulimboka na kumuombea apone haraka ili aungane na familia yake
na Watanzania wenzake katika ujenzi wa taifa. Kwa namna ya pekee
namshukuru na kumpongeza Bwana Juma Mgaza, kwa moyo wake wa huruma na
upendo na kwa hatua alizochukua za kumsaidia Dkt. Ulimboka.

Naomba kumaliza kwa kuwasihi madaktari kuacha mgomo na kurejea kazini.
Watanzania wenzenu wanateseka na kupoteza maisha. Muwe na moyo wa
huruma na upendo na msaada kwa wagonjwa kama kiapo chenu
kinavyowataka.


Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania!
Asanteni kwa Kunisikiliza.

0 comments:

Post a Comment