Tuesday, June 26, 2012

NINAVYOMKUMBUKA AMINA CHIFUPA NA SIKU YA DAWA ZA KULEVYA DUNIANI



  • Alifariki akiwa na umri wa miaka 26 tarehe 26
  • Alifariki siku ya kupiga vita dawa za kulevya
  • Alikuwa mwanaharakati wa kupinga biashara hiyo

Jumanne ya Juni 26, 2007 Haitosahaulika kwa baadhi ya sisi waTanzania kufuatia Taaarifa za kushtua, baada ya aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum, Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi(UVCCM) Amina Chifupa Mpakanjia kufariki dunia.

Amina Chifupa alifariki akiwa na umri wa miaka 26 majira ya saa 3:00 katika Hospitali Kuu ya Jeshi la Wananchi (JWTZ) Lugalo Dar es Salaam kwa maradhi ya mfadhaiko wa akili yaani "depression".
 
Majuma mawili kabla ya kifo chake Spika wa bunge la 9 Samuel Sitta aliwatangazia wabunge  kuhusu  kuugua kwa Amina na akawaomba wabunge wamwombee aweze kupona  haraka, hata mbunge wa jimbo la Mbinga Magharibi alipopata nafasi ya kuchangia hotuba ya bajeti ya Waziri Mkuu wa 2007/08 aliwasihi wabunge waendelee kumwombea Amina ili aweze kupona.

Kuugua kwa Amina kulianza kama mzaha huku kukigubikwa na habari za yeye kutalikiwa na mumewe Mpakanjia.

Ilidaiwa kwamba Mpakanjia alimtariki Amina baada ya kuwapo kwa habari kwamba ana uhusiano wa kimapenzi na Mbunge wa Kigoma Kaskazini Zitto Kabwe (CHADEMA) hali iliyowafanya wachunguzi wa mambo  kuamini kuwa ndiko kulikomsababishia ugonjwa wa mfadhaiko wa akili.
 
 
Taarifa za madaktari wa Lugalo zilionyesha kuwa Amina alifariki kutokana na shinikizo la damu na kisukari, magonjwa ambayo haikuwahi kushuhudia wakati wa uhai wake.

Wengine wanadai kilichomuua Amina, mmoja ni kujitoa kwake mhanga  katika vita dhidi ya mihadarati  kwa maana ya dawa za kulevya.

Kwa ufupi ni mbunge ambaye alisimama kidete kutoboa siri za biashara za mihadarati na kuna wakati alipata kutishiwa na Polisi na kulazimika kumpa ulinzi  kwa muda kutokana na vitisho hivyo.

Amina alifariki akiwa na msuguano na baadhi ya viongozi wa UVCCM ambao walituhumiwa  kumwona kuwa tishio  katika nafasi ya uenyekiti wa Umoja huo ngazi ya Taifa.

Amina alizaliwa Mei 20, 1981 mjini Dar es Salaam, alisoma Shule ya Msingi Ushindi, Mikocheni Dar (1988-1994) kabla ya kujiunga na masomo ya sekondari ya kidato cha kwanza hadi cha nne katika Shule ya Wasichana ya Kisutu, Dar (1995-1998). Elimu ya Juu ya Sekondari alisoma katika shule ya Makongo (1999-2001) kabla ya kujiunga na Chuo cha Uandishi wa Habri cha Royal (2001-2003) ambako alifuzu Diploma ya Uandishi wa Habari.

Mwaka 1999 alianza kazi ya Utangazaji wa Kituo cha Redio cha Clouds FM cha          Dar na aliwahi kuwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Mama Shughuli.

Katika CCM aliwahi kuwa Kamanda wa CCM wa umoja wa Vijana katika tawi la Mikocheni A jijini Dar na amekuwa Katibu wa Kamati ya Uchumi ya UVCCM mkoa wa Dar, aliwahi kuwa Mama Mlezi wa UVCCM na Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) matawi ya Bunju na Mbagala.

MAZISHI YAKE
Maelfu ya wakazi wa Jijini Dar es Salaam na vitongoji vyake siku ya Jumatano ya Juni 27, 2007 walifurika pembezoni mwa barabara za Bagamoyo na Kambarage wakiwa wameduwaa, wenye majonzi wakiupokea mwili wa aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum CCM Amina Chifupa.

Mwili wake uliwasili nyumbani kwao Mkocheni saa 7:58 mchanaukiwa katika jeneza lililopambwa kitambaa kilichodariziwa na nakshi zenye rangi ya dhahabu ukitokea katika hospitali ya Lugalo, Dar es Salaam.
 
Mara baada ya kuwasili nyumbani hapo Mufti wa Tanzania Sheikh Issa Shaban Simba aliwaongoza mamia ya waombolezaji katika sala maalumu ya kumwombea marehemu na baadaye mwili huo ukaingizwa ndani ambako ulipokelewa kwa vilio vya nguvu kutoka kwa watu waliohudhuria.

Katika msiba huo siku hiyo wengi waliufananisha na msiba wa aliyekuwa mke wa watoto wa Malkia wa Uingereza, Marehemu Princess Diana au ule wa Waziri Mkuu Edward Moringe Sokoine.

Miongoni mwa waliohudhuria mwa waombolezaji waliojumuika  ni famila ya Chifupa, Mama Maria Nyerere, Mwanasiasa Mkongwe Mzee Rashid Kawawa (marehemu), Profesa Mark Mwandosya wakati huo akiwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Katibu wa CUF Maalim Seif Shariff Hamad, John Mnyika wakati huo akiwa Mkurugenzi wa Vijana CHADEMA, baadhi ya wabunge, viongozi wa vyama vya siasa na wananchi wa kawaida.

Nyumbani kwa mzee Khamis Chifupa, baba mzazi wa Amina watu walikuwa wamefurika licha ya ukubwa wa eneo la makazi hayo na hivyo kusababisha msongano.

Hali hiyo ilisababisha Meya Manispaa ya Kinondoni  wakati huo Salum Londa kuingilia kati  na kusaidia  kamati ya mazishi  kuwapanga na kuwatuliza waombolezaji.

Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Dar es Salaam wakati huo Hemed Mkali alisema kuwa kifo cha Amina kimedhihirisha kuwa kweli alikuwa anaumizwa  na matatizo ya dawa za kulevya nchini kwani kimetokea siku iliyotengwa na dunia kupiga vita dawa za kulevya.

Meya wa Jiji la Dar wakati huo Adama Kimbisa alisema Amina alikuwa kijana mwenye kusimamia  ukweli, haki na maadili. Kimbisa alisema katika vikao  mbalimbali jambo na kulitetea kwa kufuata  misingi ya haki.
Mkurugenzi wa Clouds FM Joseph Kusaga alimwelezea Amina Chifupa ilikuwa ni hazina kwa taifa hasa kwa wasichana wadogo kutokana na kipaji alichojaliwa kujiamini katika maisha yake tangu utotoni.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) wakati huo Profesa Mark Mwandosya alisema kifo cha Amina kimeacha changamoto kubwa kwa serikali na wadau wengine kushughulikia tatizo la kushamiri kwa dawa kulevya nchini.

Kwa upande wake Maalim Seif Shariff Hamad Katibu Mkuu wa CUF alisema Amina alishughulikia kero mbalimbali zinazoiathiri jamii bila kujali itikadi za kisiasa, alikuwa mwanasiasa chipukizi aliyejitolea kushughulikia kero za wananchi bila woga.

MWISHO
Amina atakumbukwa kwa ucheshi na uwezo mkubwa wa kujenga hoja mbalimbali ndani na nje ya Bunge. Katika kipindi kifupi akiwa Mwanasiasa kijana, aliweza kusimama na kujipembua na wabunge wengine kwa kusimama kidete kupiga vita biashara ya mihadarati ambayo alaiamini inaua vijana ambao ni viongozi wa kesho.   

Alipata Ubunge Desemba 28, 2005 akitakiwa kudumu katika bunge kwa miaka mitano hadi Desemba 27, 2010. Namba yake ya Usajili kama Mbunge ilikuwa ni 1313.

Alizikwa majira ya saa 10 jioni ya Juni 28, 2007 kijijini Lupembe Wilayani Njombe mkoa wa Iringa wakati huo, karibu kabisa na eneo alilokuwa akiishi bibi yake.

Spika wa Bunge la 9 Samuel Sitta aliongoza mazishi hayo ayaliyohudhuria na watu wa kada mbalimbali na watu mashuhuri. 

0 comments:

Post a Comment