Tuesday, May 15, 2012

POLISI 700 WAGHUSHI VYETI

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa, Dickson Maimu.

MAMLAKA ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), imebaini zaidi ya polisi 700 na wanajeshi wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) 248 wakiwa wameghushi vyeti vya shule. 

Mkurugenzi Mkuu wa NIDA, Dickson Maimu alisema jana Dar es Salaam alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu sababu za kuchelewa kutoa vitambulisho vya Taifa vilivyotarajiwa kuanza kutolewa mwanzoni mwa mwezi huu. 

Kutokana na udanganyifu huo, Maimu alipendekeza kiundwe chombo maalumu cha kuchunguza hali hiyo. 

"Katika uzoefu tuliopata katika majaribio ya utoaji vitambulisho, tumebaini baadhi ya waombaji ambao wameonekana kutumia vyeti visivyo vyao, hivyo tumeona kuwapo haja ya kuwa na chombo maalumu cha uchunguzi, ili kujihakikishia kunakuwa na taarifa sahihi," alisema Maimu. 

Kuhusu kuchelewa kutoa vitambulisho hivyo, alisema kulitokana na mabadiliko makubwa katika mfumo wa daftari la kielektroni la anuani za makazi na simbo za posta na Daftari la Kudumu la Wapiga Kura la Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC). 

"Mradi wa anwani za makazi na simbo za posta, unasimamiwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na unalenga kuhakikisha kuwa anwani za makazi na simbo za posta zinawekwa nchi nzima. NIDA imekuwa ikishirikiana kwa karibu na TCRA katika utekelezaji wa mradi huu, kwani kimsingi mdau mkuu wa matumizi ya simbo za posta ni NIDA. 

"Lakini wakati tunaendelea na utekelezaji huu, kumekuwa na mabadiliko ya majina ya mikoa, wilaya, kata na vijiji, kutokana na uamuzi wa Serikali kufanya marekebisho katika Serikali za Mitaa, kwa kuongeza mikoa mipya ambayo haikuwapo wakati tunasaini mkataba na mkandarasi," alisema. 

Kutokana na changamoto hizo, alisema Mamlaka hiyo imeona ni busara kuzindua mradi ukiwa tayari umetatua changamoto hizo jambo ambalo litachukua zaidi ya miezi miwili au pungufu. Sababu nyingine ya kuchelewa kwa vitambulisho hivyo kwa mujibu wa Maimu ni kufanya usajili wa pamoja na NEC. 

Alisema Serikali imeamua kuwa vitambulisho vya Taifa vitolewe sambamba na uandikishaji wa wapigakura ili kupunguza gharama kwa Serikali na usumbufu unaoweza kutokea kwa kuita watu walewale kujiandikisha mara nyingi ndani ya kipindi kifupi. 

"Baada ya kutambua umuhimu wa kupunguza gharama za uendeshaji na adha kwa wananchi, Mamlaka imefanya majadiliano na NEC na kukubaliana kuwa usajili ufanyike kwa kushirikiana katika nyanja za vifaa, watumishi na wakandarasi," alisema Maimu. 

Mkurugenzi huyo alisema mabadiliko hayo pia yamelazimu kufupisha ratiba ya awali ya kuandikisha watu kutoka miaka minne hadi mwaka mmoja na nusu. 

Alisema ni lazima sasa kutumia vitambulisho kwa ajili ya kupigia kura ya maoni rasimu ya Katiba mpya mwaka 2014. Hata hivyo, alisema hiyo itawalazimu kubadilisha utaratibu wa kukusanya taarifa na umuhimu wa kuongeza vifaa ambavyo awali NIDA haikuvipanga ili kuwezesha kuchapisha vitambulisho vya kupigia kura sambamba na uandikishaji wa vitambulisho vya utaifa kwa muda mfupi. 

Maimu alisema pamoja na mabadiliko yaliyopo, usajili utaendelea kama kawaida, kwa kuanzia na wananchi wa Dar es Salaam hivi karibuni na utatanguliwa na ujazaji madaftari ya wakazi, kabla ya kujaza fomu za usajili. 

Alitoa mwito kwa taasisi zote za Serikali zinazohusika na utoaji nyaraka za taarifa binafsi za umri, uraia na nyinginezo, kufuata sheria za nchi katika utoaji kwa watu sahihi.

CHANZO: HABARILEO



0 comments:

Post a Comment