Thursday, September 12, 2013

Abiria asiye na kitambulisho atazuiwa kusafiri ndani ya ziwa Victoria - SUMATRA



Abiria asiye na kitambulisho atazuiwa kusafiri ndani ya ziwa Victoria - SUMATRA
Mamlaka ya Uthibiti Usafiri wa nchi kavu na Majini (SUMATRA), imewataka abiria na wananchi wote wanaotumia vyombo vya usafiri wa majini kupitia bandari zote za Ziwa Victoria, kuwa na kitambulisho kinachoonyesha taarifa zao muhimu wakati wa kukata tiketi.

Akitoa taarifa hiyo mkoani Mwanza, Mhandisi Japhet Loisimaye Ole ambaye ni Afisa Mfawidhi wa SUMATRA Kanda ya Ziwa kwa niaba ya Msajili wa Meli SUMATRA, amesema kwamba utaratibu huu unalenga kuwa na taarifa sahihi kwa kila abiria katika meli ama boti, sambamba na kuzuia abiria kusafiri kwa kutumia tiketi yenye jina la mtu mwingine.

Amesema kwamba utaratibu huo kwa kanda ya ziwa utaanza kutumika rasmi kuanzia septemba tisa ambayo ni jumatatu ya wiki ijayo, ambapo wamiliki wa meli ama doti watalazimika kujaza taarifa sahihi katika orodha 
ya wasafiri kwa mujibu wa vitambulisho vyao.

Mhandisi Ole amebainisha kwamba kupitia utaratibu huo, Maafisa wa Bandari na Mialo yote iliyoko ndani ya ziwa Victoria watawaruhusu abiria wenye tiketi halali na vitambulisho husika pekee kuingia bandarini ama melini.

Ameainisha vitambulisho vinavyoweza kuwasilishwa ni pamoja na: Kitambulisho cha uraia, Kitambulisho ukaazi, Hati ya kusafiria (passport), Kitambulisho kupigia kura, Kitambulisho cha kazi, Leseni ya udereva pamoja na barua ya utambulisho inayotolewa na serikali za mitaa yenye picha.

 Amefafanua kwamba kwa upande wa watoto wadogo ambao wengi wao hawana vitambulisho vya aina yoyote, watatumia barua za utambulisho zinazotolewa na serikali za mitaa, barua ambazo sharti ziwe na picha ya mhusika.

Aidha amebainisha kwamba agizo hilo halitawahusu abiria wanaotumia usafiri wa meli ama boti zinazosafiri umbali usiozidi maili za majini 20 kati ya bandari moja na nyingine sambamba na vivuko, 'ferry'.

Katika hatua nyingine Mhandisi Ole amesema kwamba suala la kuonesha vitambulisho halina gharama yoyote na hivyo kuwataka kuonesha ushirikiano wao, huku akitoa onyo la kuwachukulia hatua kali wamiliki wa vyombo vya usafiri wa majini watakaokuwa wanasafirisha abiria kinyemela bila kufuata utaratibu huo.

Agizo hili ni sehemu ya utekelezaji wa Kanuni za Kuhakiki na Kusajiri Abiria (Merchant Shipping Counting and Registration of Person on Board Passenger Ships) kama zilivyoainishwa na tangazo la serikali Na: 142/2011, likiwa na lengo la kupata idadi na taarifa kamili za abiria, taarifa ambazo husaidia katika uokozi pindi chombo cha usafiri kinapopata dharura majini.

Albert G Sengo, MWANZA
via GSengo blog



0 comments:

Post a Comment