Monday, August 19, 2013

Dk Najimu: Mambo 5 ya kumsaidia mtoto afanikiwe



Dk Najimu: Mambo 5 ya kumsaidia mtoto afanikiwe
Kila mzazi anatamani sana na kupenda sana kuona mwanaye anafanikiwa maishani na siyo kumuona anaishia maisha ya kubangaiza ama ya kukatisha tamaa huku akujihusisha na makundi ya ovyo na tabia hatarishi kama vile ulevi/utumiaji wa madawa ya kulevya, wizi/ujambazi, uhuni, nk!

Je, mnajua wapi tunakosea?

Binafsi, ninaona mtoto akipata mambo makuu 5 yafuatayo, kutakuwa na uwezo mkubwa sana wa kufanikiwa:
1.       MAADILI:-Ni jukumu letu kwanza kuwa mfano wa uadilifu kwani mtoto huiga zaidi maisha ya mzazi/mlezi wake. Ni vigumu sana kumfundisha mtu kitu akakuelewa kama wewe mwenyewe kinakushinda. Mfundishe mtoto njia nzuri impasayo naye hataiacha hata akiwa mzee! Mtoto muadailifu ni kipenzi/kivutio cha kila mtu mwenye mapenzi mema(nia njema). (NB: Sitaki kuongea sana hapa, ila ninao ufafanuzi wa kutosha).

2.       UFADHILI:- (Upendo na matunzo ya dhati): Laiti mtoto akijengewa misingi mizuri ya kupendwa na kutunzwa vema hali hiyo itamjengea kuwa na upendo kwa watu wengine (kuwajali wengine) na kujiamini kusiko na kifani. (NB: Kuna watoto wengi wanaharibika baada ya kuona hakuna mtu/jamii inayowapatia mapenzi/matunzo ya dhati). Pia hapa sitaki kuongea sana lakini ninao ufafanuzi wa kutosha.

3.       HAMASA:-Mtoto akipata hamu au shauku ya kutosha ya kuwa mtu fulani, kutimiza ndoto fulani maishani mwake, au kufika mahali fulani basi huyo atakuwa kama maji ya mafuriko na hutohitaji kama mzazi kumlazimisha kufanya jambo fulani bali mwenyewe atakuwa akijituma kupita kiasi hadi wewe mwenyewe ufurahi. Ila hapa jambo la kuzingatia ni kumpatia mtoto exposure ya kutosha asije kutamani kutimiza ndoto za kijinga(ama ndoto duni) kutokana na upeo mdogo. (NB: pia hapa ninao ufafanuzi wa kutosha lakini acha niishie hapo).

4.       UDADISI:- Mtoto akijengewa mazingira mazuri ya kuhoji na kujibiwa ama kuelekezwa njia sahihi za kutafuta majibu sahihi, yeye mwenyewe basi atakuwa amejengewa hazina kubwa maishani mwake. Na hatua hiyo itamfanya ajitambue na ajiamini sana kwani atakuwa kwenye nafasi nzuri ya kujiuliza, kuwauliza wengine na kutafakari changamoto mbalimbali zinazomkabili na zinazoikabili jamii yake na hatimaye kupata ufumbuzi murua(yakinifu). Mtu mdadisi hababaiki kijinga jinga. (NB: pia hapa ninao ufafanuzi mkubwa na wa kutosha lakini acha niishie hapo).

5.       KUJIAMINI:- Endapo mtoto atapatiwa kiwango cha kutosha cha mambo manne niliyoyataja hapo juu kwa maana ya maadili, ufadhili, hamasa na udadisi basi kujiamini kutakuwa ni tunda la hayo mazao. Na mtu mwenye kujiamini kwa kiwango cha kujitosheleza ni mtu ambaye anao uhakika kuwa mambo yatamnyokea ingawaje anaweza kupitia misuko suko ya hapa na pale katika kuelekea kutimiza ndoto zake. (NB: Pia hapa ninaoufafanuzi mzuri mno lakini acha niishie hapo).

Mwisho nawatakia malezi mema ya watoto wetu wazazi wenzangu! Ruksa kukosoa ama kuongeza ulilo nalo.

Dk. Najimu Mohamed (MD) (aka Benjamin Najimu)
(16/8/2013, 5:40 AM).



0 comments:

Post a Comment