Tuesday, August 27, 2013

Redd’s Miss Tanzania 2013 uso kwa uso na waandishi wa habari



Redd's Miss Tanzania 2013 uso kwa uso na waandishi wa habari
 Na Mwandishi Wetu 

WAREMBO 30 wanaowania taji la Redd's Miss Tanzania 2013, kesho wanatarajiwa kukutana rasmi na waandishi wa habari, ili kila mmoja kutoa mtazamo wake,shughuli itakavyofanyika katika hoteli ya Giraffe iliyopo Kunduchi, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi wa Kampuni ya Lino ambao ni waandaaji wa Redd's Miss Tanzania, Hashim Lundenga alisema, mkutano kati ya waandishi wa habari na warembo ni muhimu kuwajengea uwezo zaidi wa kujiamini.

"Washiriki hao wataulizwa maswali mbalimbali na waandishi wa habari na wao wataeleza mtazamo wao kuhusu Redd's Miss Tanzania, hatutawafunga, wao waandishi watakuwa huru kila mmoja kumuuliza mshiriki yoyote swali analotaka," alisema.

Washiriki hao ambao leo walikuwa na semina maalumu na waandaaji wa mashindano haya ambao ni Kampuni ya Lino International Agency Limited.

Baada ya kukutana na waandishi wa habari, warembo hao wanatarajiwa kuanza ziara maalumu ya kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo nchini kwa lengo la kuhamasisha utalii wa ndani.

Warembo hao watakuwa kambini kwa muda wa siku 30 wakipata mafunzo mbalimbali yatakayotolewa na wataalamu kutoka katika sekta mbalimbali kama vile afya, ajira, ujasiriamali, uwekezaji na sekta ya utalii.

Brigitte Alfred ndiye Mrembo anayeshikilia taji hilo kwa sasa, baada ya kufanikiwa kulitwaa mwishoni mwa mwaka jana.

Meneja wa Redd's, Victoria Kimaro naye alisema kama wadhamini wapo tayari kuhakikisha shindano hilo linafanikiwa zaidi mwaka huu kuliko kipindi chote kile.

Kinywaji cha Redd's Original kinazalishwa na kusambazwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL).



0 comments:

Post a Comment